Mabeki wataamua matokeo Fountain Gate vs Simba

Safu za ulinzi za Fountain Gate na Simba zitalazimika kufanya kazi ya ziada wakati timu hizo zitakapokutana leo kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati kuanzia saa 10 jioni.

Makali ya kufumania nyavu ambayo safu za ushambuliaji ya kila timu imeonyesha katika mechi zilizopita, ni mtego kwa mabeki na kipa wa kila upande wakati timu hizo zitakapocheza leo ambao wanapaswa kuonyesha viwango bora vinginevyo watakaoshindwa kufanya vizuri, watajikuta wanaliweka lango lao matatani.

Timu zote mbili kila moja imekuwa na wastani wa kufunga bao kwenye kila mechi ya ligi msimu huu jambo ambalo linaashiria kwamba washambuliaji wamekuwa wakitimiza vyema majukumu yao.

Simba katika mechi 16 za ligi imefunga mabao 34 ikiwa ni wastani wa mabao mawili kwa mchezo na Fountain Gate imefunga mabao 24 ikiwa ni wastani wa bao 1.5.

Mchezo wa kwanza uliozikutanisha timu hizo katika msimu huu uliochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex ulimalizika kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao 4-0.

Ukiondoa mechi iliyopita, Fountain Gate imekuwa haina historia nzuri pindi ikutanapo na Simba kwani haijawahi kuonja ladha ya ushindi kwenye mechi baina yao katika Ligi Kuu kwani katika mechi tano ambazo zimewahi kukutana hapo nyuma, Simba imepata ushindi mara nne na zimetoka sare moja.

Zinakutana timu mbili ambazo zimekuwa na mwenendo tofauti katika mechi za ligi hivi karibuni ambapo Simba imekuwa katika kiwango bora sana huku Fountain Gate yenyewe ikienda kwa kusuasua.

Matokeo ya mechi 10 zilizopita za ligi ambazo kila timu imecheza msimu huu, yanathibitisha kutofautiana kwa kiwango baina ya Simba na Fountain Gate.

Wenyeji Fountain Gate katika mechi 10 zilizopita za ligi, imepata ushindi mara mbili tu, ikitoka sare moja wakati huo Simba ikiwa imepata ushindi katika mechi zote 10 mfululizo.

Ushindi katika mechi ya leo utaifanya Simba kufikisha pointi 46 na hivyo kuzidi kujikita katika nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa ligi huku kwa Fountain Gate, ushindi utaifanya ifikishe pointi 23 na hivyo kuendelea kubaki katika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi.

Kocha msaidizi wa Simba, Darian Wilken alisema kuwa timu yake ipo tayari kwa mchezo huo.

“Tunafahamu taarifa za kutosha kutokea kwa wapinzani wetu ikiwemo kocha wao mpya mwenye uzoefu pamoja na kufanya usajili wa wachezaji wapya. Kwa hiyo itakuwa mechi ya ushindani zaidi tofauti na ile ya mzunguko wa kwanza,” alisema Wilken.

Kocha wa Fountain Gate, Robert Matano alisema anaamini mechi hiyo itakuwa nzuri na ngumu kwa kila upande.

“Mimi sio mgeni kwa mpira ni mkongwe. Tunakaribisha wageni wetu Simba na tunatarajia mchezo utakuwa mzuri kwetu sote. Maandalizi ya timu ni mazuri. Tunajua Simba ni timu kubwa tunawaheshimu lakini sisi pia tuko tayari,” alisema Matano.

Mechi nyingine leo itakuwa ni baina ya Azam FC dhidi ya KMC, Dodoma Jiji dhidi ya Pamba na Tanzania Prisons dhidi ya Mashujaa.

Related Posts