Simba, Fountain Gate mambo ni mawili tu!

KUNA mambo mawili yanayotazamwa leo katika mchezo wa Ligi Kuu Bara pale Fountain Gate itakapoikaribisha Simba kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo mkoani Manyara.

Jambo la kwanza ni mwanzo wa kocha Robert Matano utakuwaje baada ya mtangulizi wake Mohamed Muya aliyeondoka mwishoni mwa mwaka jana kuonekana kuna sehemu amekwama kwani rekodi zinaonyesha mechi kumi za mwisho timu hiyo imeshinda mbili tu tena zote nyumbani huku ikipoteza saba na sare moja.

Kitu cha pili ni mwendelezo bora walionao Simba uliowafanya kuwa timu iliyoshinda mechi zote za ugenini katika ligi msimu huu ambazo ni nane, pia imefunga mabao mengi zaidi (15) na kuruhusu mawili.

Katika kushinda ugenini, sio wao peke yao, bali hata Yanga imefanya hivyo lakini imecheza mechi saba.

Katika mambo hayo mawili, majibu yake yatafahamika baada ya mchezo huo uliopangwa kuchezwa kuanzia saa 10:15 jioni huku Simba ikisaka ushindi utakaowafanya kuendelea kukaa kileleni huku Fountain Gate ikipambania kupanda juu zaidi kwenye msimamo kwani kabla ya mechi za jana, ilikuwa nafasi ya sita na pointi 20.

Ukiweka kando namna ambavyo nyota wa Simba wanavyopambana kusaka ushindi kwa kufunga mabao, pia safu yao ya ulinzi imekuwa imara kulinda nyavu zao zisitikiswe, hivyo ni timu inayofunga na kuzuia kikamilifu.

Matokeo ya mchezo wa kwanza Simba ilipokuwa nyumbani ilishinda 4-0 dhidi ya Fountain Gate kupitia wafungaji Edwin Balua, Steven Mukwala, Jean Charles Ahoua na Valentino Mashaka. Hiyo inatoa picha kwamba wapo imara lakini safari hii kutakuwa na mabadiliko kutokana na maboresho yaliyofanyika kipindi cha usajili wa dirisha dogo.

Simba iliyomuongeza Elie Mpanzu katika dirisha dogo, wanaoongoza kwa mabao ndani ya kikosi hicho ni Jean Charles Ahoua na Leonel Ateba, kila mmoja akifunga saba kitu ambacho Fountain Gate wanapaswa kuwa makini nacho ili kuzuia mvua ya mabao.

Lakini ubora wa Simba unafanya mchezaji yeyote kuwa na uwezo wa kufunga, ni mtihani mwingine kwa Fountain Gate inapokwenda kukabiliana nayo.

Mabao 34 waliyonayo Simba yamefungwa na wachezaji 11 tofauti, ambapo washambuliaji wamefunga 13, viungo (15) na mabeki (6). Hii inaashiria kwamba washambuliaji na viungo wakipata nafasi wanafanya kweli na hata mabeki kwani nao wamechangia mabao sita.

Katika ulinzi pia, Simba ndiyo timu iliyoruhusu mabao machache zaidi (5), hivyo ni timu inayofunga sana na kuzuia vizuri. Kumbuka kipa wao namba moja Moussa Camara ndiye kinara wa clean sheet akiwa nazo 13 katika mechi 16.

“Kushinda mechi hasa hizi za ugenini inatokana na namna tunavyopanga mikakati yetu, huwa tunaangalia uwanja tunaokwenda kucheza unaruhusu mbinu gani za ushindi.

“Viwanja vingi vya ugenini haviruhusu kucheza soka la pasi nyingi, hivyo tunajua namna ya kucheza mechi zao, nadhani hiyo inatusaidia,” alisema kocha wa Simba, Fadlu Davids ambaye ameiongoza timu hiyo kukusanya pointi 43 baada ya kucheza mechi 16.

Wakati Simba ikiwa imara katika kufunga na kuzuia, wapinzani wao wana matatizo katika maeneo hayo.

Mbali na kufunga mabao 23 yakionekana kuwa mengi kuzidi baadhi ya timu nyingine, Fountain Gate ndiyo timu iliyoruhusu mabao mengi zaidi kabla ya mechi za jana ambayo ni 32. Hiyo ni ishara kuwa safu yao ya ulinzi inayoongozwa na nahodha Laurian Makame na Joram Mgeveke lazima iwe makini.

Fountain Gate ambayo mara ya mwisho kucheza mechi ya ligi ilikuwa Desemba 29, 2024 ilipofungwa 5-0 na Yanga, imekuwa na muda mwingi wa kujiandaa na mchezo huu hali inayompa matumaini kocha Matano.

“Sisi tunajiandaa kivyetu na wao (Simba) wanajiandaa kivyao, naona mchezo utakuwa mzuri na mgumu kwani tunakutana na timu yenye uzoefu mkubwa.

“Nimekaa na wachezaji wangu na kuwaandaa kwa ajili ya mchezo huo, mashabiki waje kutusapoti, tunaamini tutafanya vizuri,” alisema kocha huyo raia wa Kenya.

Kabla ya mchezo huo wa jioni, mapema saa 8 mchana zitapigwa mechi mbili. Tanzania Prisons inayofundishwa na Amani Josiah ambaye ataiongoza timu hiyo kwa mara ya kwanza mechi za ushindani, itaikaribisha Mashujaa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, huku Dodoma Jiji ikiwa mwenyeji wa Pamba Jiji kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Mara ya mwisho Mashujaa na Tanzania Prisons zilipokutana matokeo yalikuwa 0-0, hii ni nafasi nyingine kwao kujiuliza kwani Prisons haipo sehemu salama zaidi kulinganisha na Mashujaa.

Prisons imekusanya pointi 14 na kushika nafasi ya 13, wakati Mashujaa ni ya saba ikiwa na pointi 19, hii ni kabla ya mechi za jana ambapo timu zote zilikuwa zimecheza mechi 16.

Kwa rekodi, timu hizo zimekutana mara tatu, moja msimu huu ambapo hazikufungana lakini msimu uliopita kila moja ilishinda nyumbani kwa mwenzake.

Dodoma Jiji na Pamba Jiji unaweza kuiita Dabi ya Majiji, mchezo wa kwanza walitoka 0-0. Fred Felix Minziro na vijana wake wa Pamba Jiji, wamefanya maboresho kipindi cha dirisha dogo wakisajili wachezaji kadhaa akiwamo kipa Mohamed Kamara, Francois Bakari, Mathew Tegis, Abdulaye Camara, Modou Camara na Shassir Nahimana.

“Mapumziko tumeyatumia vizuri, tumepata maingizo mapya hivyo tunaamini mchezo utakuwa mzuri,” alisema Minziro.

Hata Dodoma Jiji nayo imejiimarisha kwa kuwashusha Abdi Banda na Mukrim Issa.

Mwisho kabisa, Azam itaikaribisha KMC kwenye Dimba la Azam Complex, saa 1:00 usiku.

Ni mchezo wa KMC kujiuliza ilikuwaje duru la kwanza ikiwa nyumbani ilichapwa 4-0 na Azam.

Azam yenye pointi 36 ikishika nafasi ya tatu kwenye msimamo, inapambana kupanda juu zaidi ikiachwa pointi sita na Yanga kabla ya mchezo wa jana huku pia ikizidiwa pointi saba nyuma ya Simba.

Related Posts