Wananchi walia kupanda gharama za maisha Goma, bei ya maharage yapaa

Goma. Wiki moja baada ya kundi la waasi la M23 kuuteka mji wa Goma ambao ni mji mkuu wa Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), gharama za maisha zikiwemo za vyakula zimepanda na kusababisha kadhia kwa wananchi.

Kutokana na kupanda kwa bei na kuongezeka kwa wakimbizi, lishe ya msingi imekuwa nje ya uwezo wa wengi, na mamia ya maelfu ya watu mjini humo wanaweza kukumbwa na njaa kali, kulingana na shirika la kupambana na umasikini, ActionAid.

Wafanyakazi wa shirika hilo waliotembelea masoko matatu ya Virunga, Lenine na Kituku mjini Goma, wameripoti kupanda kwa bei ya baadhi ya bidhaa za chakula, ikiwemo unga, maharage, na mafuta, kwa kiwango cha kati ya asilimia 18 na 160 kati ya Januari 25 na Januari 31.

Usiku wa Januari 26, wapiganaji wa M23 wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda walivamia Goma na kutangaza kuwa wako madarakani.

Kulikuwa na mapigano ya hapa na pale kati ya waasi na jeshi la DRC katika siku zilizofuata, huku huduma za umeme, maji, na intaneti zikikatwa na biashara kufungwa.

Zaidi ya wiki moja baadaye, umeme umeanza kurejea kwa kiasi kikubwa na bidhaa za chakula zinapatikana sokoni, wakazi wa Goma wameiambia Al Jazeera.

Hata hivyo, walithibitisha kuwa bei za bidhaa kadhaa zimeongezeka mara mbili au hata mara tatu tangu waasi walipochukua mji huo.

“Ninaomba viongozi wapya wafanye kila wawezalo kurejesha utulivu hapa,” amesema Julienne Anifa, mama wa watoto saba aliyekuwa akinunua bidhaa katika Soko la Alanine mjini Goma.

“Tunaponunua bidhaa mbalimbali kwa bei ya juu, hali hii inatuathiri kiuchumi hasa katika kipindi hiki cha vita,” amesema.

Mmoja wa wafanyakazi wa kujitolea wa ActionAid katika wananchi wa Goma, ambaye alizungumza kwa masharti ya kutobainishwa kwa ajili ya usalama wake, alisema: “Kila kitu kimepanda bei. Awali tulikuwa tunanunua ndoo ya mchele kwa Dola 20 (Sh 50,925), sasa ni angalau dola 23 (Sh58,564). Chupa kubwa za maji ya kunywa nazo zimepanda bei mara mbili kutoka dola 1 (2,546.28) hadi dola 2 (5092.56).

“Wakati wa mapigano, vitu ambavyo ungeweza kununua kwa dola 2 vilikuwa ghafla vinauzwa kwa dola 6 kwa sababu chakula kilikuwa hakiletwi mjini. Sasa bei zimepungua kidogo, lakini bado ni ghali sana kwa watu wengi,” ameongeza.

ActionAid ilitahadharisha Jumatatu wiki hii kwamba kupanda kwa gharama za maisha kunasababisha familia nyingi kukosa chakula, na hivyo kuhatarisha mamia ya maelfu ya watu kwa utapiamlo.

“Hatuna kipato watu hawawezi kwenda kazini kwa sababu ya machafuko, hivyo kupata pesa ni ngumu. Kila mtu hana hela,”amesema mmoja wa wajitolea wa ActionAid katika jamii.

Kabla ya kuzuka upya kwa mgogoro huu, takriban robo ya watu milioni 25.5 nchini humo tayari walikuwa katika viwango vya hatari na dharura vya usalama wa chakula, kwa mujibu wa Integrated Food Security Phase Classification (IPC).

 Kwa mujibu wa Shirika la Chakula Duniani (WFP), Katika kipindi cha miezi mitano ijayo, watoto milioni 4.5 wenye umri wa chini ya miaka mitano pamoja na wanawake milioni 3.7 wajawazito na wanaonyonyesha wanaweza kukumbwa na utapiamlo.

WFP pia ilitoa tahadhari kuhusu kuongezeka kwa idadi ya watu wanaokimbia makazi yao, ikisema mamia ya maelfu ya watu wanaweza kuhama kutoka kambi za wakimbizi mashariki mwa DRC.

Kambi za wakimbizi wa ndani mjini Goma zilikuwa tayari zinategemea msaada wa kibinadamu hata kabla ya kuzuka kwa mapigano Januari 26 mwaka huu. Hata hivyo, mapigano hayo yamevuruga shughuli muhimu za mashirika ya misaada, na kuwaacha makumi ya maelfu bila msaada wowote.

“Tunahitaji msaada wa haraka na kwa kasi. Lakini kwa sasa juhudi za misaada zinazuiwa,” amesema Yakubu Mohammed Saani, mkurugenzi wa ActionAid nchini DRC.

DRC yaagiza M23 kuondoka Goma

Katika hatua nyingine, Serikali ya DRC imelitaka kundi la waasi la M23 pamoja na majeshi ya Rwanda kuondoka katika mji wa Goma, mashariki mwa nchi hiyo.

“Tunahitaji kuona hatua halisi, na kile tunachomaanisha ni kuwa na ushahidi kwamba hii si suluhisho la juujuu tu,” Waziri wa Mambo ya Nje Therese Kayikwamba Wagner aliambia kituo cha televisheni cha Afrika Kusini, Newzroom Afrika.

M23 ilitangaza usitishaji mapigano Jumatatu baada ya wiki mbili za mapigano na jeshi la Congo kwa ajili ya udhibiti wa Goma.

Inakadiriwa kuwa zaidi ya watu 2,000 wameuawa kwenye mapigano hayo na wengine 2,880 wamejeruhiwa.

Wagner aliongeza kuwa vikosi vya Rwanda na waasi wa M23 wanadaiwa kukata maji, umeme na kuzuia njia zote zinazoelekea ndani na nje ya Goma.

Rais wa Rwanda, Paul Kagame, amekanusha mara kwa mara madai kuwa nchi yake inaunga mkono waasi wa M23.

Akikwepa kuthibitisha au kukanusha uwepo wa wanajeshi wa Rwanda huko Goma kama inavyodaiwa Congo, Rais Kagame aliambia CNN kwamba hajui kama vikosi vya nchi yake vipo Goma, ambako kuna mapigano kati ya kundi la waasi wa M23 na wanajeshi wa Congo.

M23 inadai kuwa mapambano yake yanatokana na malalamiko ya ubaguzi dhidi ya jamii ya Watutsi katika eneo hilo.

Msemaji wa Serikali ya Congo, Patrick Muyaya, Jumanne wiki hii alitoa tangazo la usitishaji mapigano la waasi kuwa ujumbe wa uongo.

Imeandaliwa kwa msaada wa Mashirika ya habari.

Related Posts