BAADHI ya mashabiki wa soka wakiwamo wa Yanga jana walishindwa kuvumilia na kujikuta wakimpa Selemani Rashid ‘Bwenzi’ wa KenGold fedha baada ya kufunga bao safi wakati timu yake ikilala kwenye Uwanja wa KMC Complex, huku akisema alimshtukia kipa Diarra Djigui akiomba maji akamtungua kwa shuti la mbali kutokea katikati ya uwanja.
Kiungo huyo alifanya maajabu baada ya kufunga bao la kuvutia kwa shuti kali kutoka katikati ya uwanja wakati wachezaji wa timu zote mbili wakiwa wamezubaa wakijiandaa Kengold ianzishe mchezo baada ya Yanga kufunga bao la sita katika mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara.
Badala ya Bwenzi kuanzisha mpira kwa kumpasia mchezaji mwenzake, yeye aliamua kuupiga moja kwa moja langoni kwa Yanga baada ya kumuona kipa Diarra hayupo katika eneo lake.
Hili ndio bao ambalo hadi sasa limefungwa kutoka umbali mrefu zaidi, lakini likiwa bao la tano anafungwa kipa Diarra katika Ligi Kuu Bara msimu huu.
Baada ya bao hilo, Bwenzi amesema aliyatumia vyema makosa aliyokuwa anayafanya kipa huyo wa Yanga na yeye kila siku amekuwa ni mtu wa kujaribu.
“Hii ni moja ya jambo ambalo nimekuwa nikijifunza mazoezini. Diarra ni kipa mzuri lakini kama walivyo wazuri wengine wanachangamoto zao, ndiyo nilichokifanya niliangalia madhaifu yake nikayatumia unajua pale alikuwa mbele sana, ni goli zuri lakini makosa yake ndiyo yamechangia.
“Mimi kama mchezaji nilipokuwa naagalia niliona kama vile alikuwa anaomba maji, hivyo alishaondoka langoni kwake ndiyo maana nikaamua kujaribu na kweli nimefanikiwa kufunga,” alisema Bwenzi ambaye baada ya mechi baadhi ya mashabiki walionekana kumpongeza wakiwemo waliovaa jezi za Yanga.
Tayari mashabiki wameanza kugawanyika kutokana na ubora wa bao hilo baadhi wakiamini kuwa linaweza kuwa bora kwa msimu huu, huku wengine wakiamini kutokuwa makiniĀ kwa Diarra kumechangia kwa sehemu kubwa staa huyo kufunga bao hilo ambalo ni la 12 kwa KenGod msimu huu ikiwa inashika nafasi ya mwisho kwenye msimamo na pointi sita.
Yanga ambayo hadi sasa imeruhusu mabao saba kwenye Ligi Kuu Bara ikiwa inashika nafasi ya pili kwa timu iliyofungwa mabao machache baada ya Simba ambayo imefungwa matano, imekuwa na kasi nzuri ya kufunga mabao ambapo hadi sasa ndiyo inaongoza kwa kupachika mengi ikiwa imeshafunga mabao 42 ikifuatiwa na Simba iliyofunga 34 na leo inacheza dhidi ya Fountain Gate kwenye Uwanja wa Kwaraa Manyara.