Viongozi duniani wamlilia mtukufu Aga Khan IV

Dar es Salaam. Kiongozi Mkuu wa 49 wa Madhehebu ya Shia Ismailia na mwanzilishi wa Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN), Mtukufu Aga Khan, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 88.

Mtukufu Aga Khan, anayefahamika kama Karim Al-Hussaini Aga Khan IV, alifariki dunia Februari 4, 2025, jijiji Lisbon, Ureno akiwa amezungukwa na familia yake.

Taarifa iliyotolewa na shirika lake la misaada, Aga Khan Development Network, ilisema kiongozi huyo alifariki dunia kwa amani jijini Lisbon, Ureno akiwa na familia yake.

Mwana Mfalme Rahim Al-Hussaini ameteuliwa kuwa Aga Khan wa V kushika nafasi hiyo kufuatia kifo cha Mtukufu Aga Khan IV.

Mwana Mfalme Rahim Al-Hussaini aliyeteuliwa kuwa Imam wa 50 wa madhehebu ya Ismailia.

Mwana Mfalme Rahim anakuwa Imamu wa 50 wa madhehebu ya Shia Ismailia, ametangazwa kurithi nafasi ya baba yake Aga Khan wa IV baada ya kufunguliwa kwa wosia wa marehemu baba yake.

Katika kipindi cha miaka 1,400 ya historia yao, waumini wa Ismailia wameongozwa na Imamu wa moja kwa moja wa kizazi cha urithi. Waismailia wanaishi katika zaidi ya nchi 35 na idadi yao inakadiriwa kuwa kati ya milioni 12 hadi 15.

Viongozi, marais wamlilia

Kufuatia kifo cha Mtukufu Aga Khan, viongozi na marais kadhaa duniani, akiwamo Rais Samia Suluhu Hassan wametoa salamu za pole, wakimwelezea kwa sifa kemkem.

Akitoa salamu za pole jana, Rais Samia aliandika: “Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mwana Mfalme Karim Al-Husseini, Aga Khan IV, kiongozi mkuu wa kiroho wa dhehebu la Kiislamu la Ismailia ulimwenguni na mwanzilishi wa Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan.

“Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ninatoa salamu za pole kwa familia ya mwana mfalme Aga Khan, Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan na Jumuiya ya Waislamu wa Ismailia.

“Tunaungana nanyi kuomboleza kuondokewa na kiongozi mkubwa na mwenye maono, ambaye kazi yake imegusa maisha ya mamilioni ya watu duniani,” aliandika Rais Samia kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Mbali na Rais Samia, Rais wa Kenya, Dk William Ruto naye alitoa salamu za pole kufuatia kifo hicho kupitia mtandao wa X:

“Ni kiongozi mkubwa ambaye alienda mbali kwa kufanya yaliyodhaniwa kuwa hayawezekani, aliyafanya kwa kusaidia jamii iliyokuwa hatarini, kwa shughuli za kujitolea na misaada kupitia ujenzi wa shule na hospitali.

“Tumesikitishwa sana na kifo cha Mtukufu Aga Khan, kiongozi wa kiroho wa Waislamu wa Ismailia… Tupo pamoja na familia ya mwana mfalme na jumuiya ya Ismailia kwa ujumla,” alisema.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), António Guterres alieleza kumkumbuka Mtukufu Aga Khan IV kama kiongozi wa kiroho ulimwenguni na mhamasishaji wa amani, maendeleo na mshikamano.

“Kwa miongo kadhaa Aga Khan amekuwa akijitoa kuboresha ustawi wa maisha ya watu duniani, hususan walioko hatarini kukosa huduma za kibinadamu kwa kusaidia upatikanaji wa elimu na misaada ya kiutamaduni,” alisema Guterres, kupitia msemaji wa UN, Stéphane Dujarric.

“Uongozi wa Taasisi ya Aga Khan ulienda mbali zaidi ya imani ya madhehebu ya Shia Ismailia. Alikuwa daraja la kutuelimisha kati ya utamaduni na maendeleo ya dunia. Jitihada zake kupambana na umaskini, kuleta usawa wa kijinsia na kuchochea maendeleo endelevu ni miongoni mwa alama alizotuachia.”

Mtukufu Aga Khan alizaliwa mjini Geneva, Uswisi, Desemba 13, 1936. Alitangazwa kuwa na afya njema licha ya kuzaliwa kabla ya wakati.

Mtukufu Aga Khan wa IV enzi za uhai wake

Aliitwa Prince Karim Al-Husseini, baadaye alijulikana kama Aga Khan IV na Imamu wa 49 wa Waismailia wa Nizari.

Prince Karim Al-Husseini alipata wadhifa wa Imamu na cheo cha Aga Khan, akiwa na umri wa miaka 20, kufuatia kifo cha babu yake, Aga Khan III. Alirithi nafasi hiyo badala ya baba yake, Prince Aly Khan na mjomba wake, Prince Sadruddin Aga Khan.

Alikabidhiwa wadhifa huo Oktoba 19, 1957 akiwa mjini Dar es Salaam katika eneo ambalo babu yake aliwahi kupewa zawadi kutoka kwa wafuasi wake, kiasi cha dhahabu na almasi zilizolingana na uzito wake.

Alikuwa mwanzilishi na mwenyekiti wa ‘Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan’ (AKDN), ambao ni mojawapo ya mitandao binafsi mikubwa ya maendeleo duniani.

Mbali na shughuli zake za kidini, Aga Khan alikuwa mfanyabiashara mashuhuri mwenye uraia wa Uingereza na Ureno, pamoja na mmiliki na mfugaji wa farasi wa mbio za kimataifa.

Tangu aliporithi nafasi ya Imamu wa Waismailia, Aga Khan IV, pamoja masuala ya kidini, alihusika pia katika masuala mbalimbali ya kiuchumi na kijamii.

Matukio haya ni pamoja na uhuru wa mataifa ya Afrika kutoka kwa wakoloni, kufukuzwa kwa jamii ya Kiasia kutoka Uganda, uhuru wa mataifa ya Asia ya Kati kama vile Tajikistan kutoka kwa Muungano wa Kisovieti na mengineyo.

Alhamisi ya Februari 27, 2014, alijipatia heshima ya kuwa kiongozi wa kwanza wa kidini kuhutubia kikao cha pamoja cha Bunge la Canada.

Kulingana na kitabu ‘The Divine Kingship of the Aga Khan: A Study of Theocracy in East Africa’, Aga Khan inaelezwa yeye ni mzawa wa moja kwa moja wa Mtume Muhammad kupitia kwa binamu na mkwe wake, Ali, ambaye Waismailia wa Nizari wanamtambua kama Imamu, pamoja na mkewe Fatima, binti wa Mtume Muhammad kutoka katika ndoa yake ya kwanza.

Aga Khan IV alikuwa mtoto wa kwanza wa Prince Aly Khan (1911–1960) na mke wake wa kwanza, Princess Taj-ud-dawlah Aga Khan, ambaye hapo awali alijulikana kama Joan Yarde-Buller (1908–1997).

Mwaka 1949, wazazi wake walitalikiana. Baada ya talaka hiyo, baba yake, Prince Aly Khan, alifunga ndoa na mwigizaji maarufu wa Marekani, Rita Hayworth, na wakapata binti mmoja, Princess Yasmin Aga Khan.

Prince Karim alitumia sehemu kubwa ya utoto wake jijini Nairobi, Kenya, ambako alisoma. Baadaye, alihudhuria chuo kijulikanacho kama ‘Institut Le Rosey’ huko Uswisi kwa miaka tisa, ambayo ni shule ya bweni ghali zaidi duniani.

Baada ya kuhitimu huko alipata nafasi ya kusoma katika Taasisi ya Teknolojia ya Massachusetts (MIT) kwa masomo ya sayansi, lakini babu yake, Aga Khan III, alikataa pendekezo hilo na badala yake Prince Karim alijiunga na Chuo Kikuu cha Harvard, ambako alichaguliwa kuwa mwanachama wa ‘The Delphic Club’ na akajikita katika historia ya Kiislamu.

Alimaliza masomo yake Harvard mwaka 1959, miaka miwili baada ya kuwa Imamu wa Waismailia, akiwa na Shahada ya Kwanza ya Sanaa katika Historia na pia alikuwa sehemu ya timu ya soka ya chuo hicho, ‘Harvard Crimson’.

Baada ya kuchukua nafasi ya uimamu, Aga Khan IV alitangaza azma yake ya kuendeleza kazi aliyoianza babu yake ya kujenga taasisi za kisasa, ili kuboresha maisha ya wengine.

Sherehe za Takht Nashini za kumtambulisha Imam mpya zilifanyika katika maeneo mbalimbali kati ya mwaka 1957 na 1958.

Katika kipindi hicho, Aga Khan alisisitiza umuhimu wa kudumisha uhusiano mzuri kati ya jamii mbalimbali—ujumbe uliokuwa na maana kubwa kutokana na mvutano wa kikabila uliokuwepo Afrika Mashariki wakati huo, kati ya watu weusi na Waasia wa Kusini.

Mwaka 1972, chini ya utawala wa Idi Amin wa Uganda, watu wenye asili ya Kiasia, wakiwamo Waismailia wa Nizari, walifukuzwa nchini humo. Waasia wa Kusini, ambao baadhi ya familia zao zilikuwa zimeishi Uganda kwa zaidi ya miaka 100, walipewa siku 90 kuondoka.

Aga Khan alimwomba rafiki yake wa muda mrefu, Waziri Mkuu wa Canada, Pierre Trudeau, kusaidia. Serikali ya Trudeau ilikubali kuwapokea maelfu ya raia hao.

Aga Khan pia alichukua hatua za haraka kuratibu makazi mapya kwa Waismailia wa Nizari waliotoka Uganda, Tanzania, Kenya na Burma kwenda mataifa mengine.

Wengi wao walipata makazi mapya Asia, Ulaya, na Amerika Kaskazini. Changamoto nyingi za awali za kuhamia zilitatuliwa haraka kutokana na elimu yao ya hali ya juu na viwango vikubwa vya kusoma na kuandika, pamoja na juhudi za Aga Khan na nchi zilizowapokea, pamoja na msaada wa mipango ya jamii ya Waismailia wa Nizari.

Aga Khan aliwahimiza Waismailia wa Nizari waliokaa katika mataifa yaliyoendelea kuchangia maendeleo ya jamii katika nchi zinazoendelea kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo.

Aga Khan na vyombo vya habari

Mwaka 1959, Aga Khan alianzisha kampuni ya vyombo vya habari nchini Kenya, Nation Media Group (NMG), ambayo inamiliki miongoni mwa magazeti mengine Daily Nation na Sunday Nation.

NMG ilianzishwa kama East African Newspapers (Nation Series) Ltd, chini ya Aga Khan Fund for Economic Development. Mwaka 1999, NMG ilizindua NTV, kituo cha habari nchini Kenya na Easy FM (sasa Nation FM).

Kufikia mwaka 2007, NMG lilikuwa shirika kubwa zaidi la vyombo vya habari vya kibinafsi katika Afrika Mashariki na Kati, likiwa na ofisi nchini Kenya, Uganda na Tanzania likiwa na magazeti kama The EastAfrican, Daily Nation, Business Daily Africa, Daily Monitor, The Citizen, Mwananchi na Taifa Leo.

Kufikia mwaka 2016, NMG ilimiliki asilimia 76.5 ya hisa katika kampuni ya Monitor Publications Limited na kituo cha redio cha 93.3 KFM kilichoko Kampala, Uganda. Pia inamiliki vituo viwili vya televisheni nchini humo, NTV Uganda na Spark TV.

NMG pia inamiliki Mwananchi Communications Limited nchini Tanzania.

Machi 2016, NMG ilizindua mashine mpya ya kisasa ya uchapishaji katika Barabara ya Mombasa, Nairobi. Kiwanda hicho kipya kina uwezo wa kuchapisha magazeti 86,000 kwa saa.

Katika miaka ya 1990, Aga Khan alikuwa na kundi la hoteli za kifahari za Italia, lililojulikana kama Ciga. Kupitia taasisi yake ya kibiashara yenye faida kubwa, AKFED, Aga Khan alikuwa mshiriki mkuu katika mtandao wa hoteli za Serena.

Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan

Aga Khan alikuwa mwanzilishi wa Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN), unaoratibu shughuli za zaidi ya mashirika na taasisi 200, yakiwa na jumla ya wafanyakazi 80,000, wengi wao wakiwa katika nchi zinazoendelea.

AKDN hupata ufadhili kutoka kwa wafuasi wake pamoja na washirika wa maendeleo, zikiwamo Serikali mbalimbali na mashirika ya kimataifa.

Mashirika yanayohusiana na AKDN yanafanya kazi katika nyanja za afya, elimu, utamaduni, maendeleo vijijini, ujenzi wa taasisi na ukuzaji wa maendeleo ya kiuchumi.

Mtandao huu umejikita katika kuboresha hali ya maisha na fursa kwa watu maskini, bila kujali dini, asili wala jinsia zao.

AKDN inajumuisha Chuo Kikuu cha Aga Khan, Chuo Kikuu cha Asia ya Kati, Mfuko wa Aga Khan wa Maendeleo ya Kiuchumi, Mfuko wa Aga Khan wa Utamaduni, Wakfu wa Aga Khan, Huduma za Afya za Aga Khan, Huduma za Elimu za Aga Khan, Huduma za Mipango na Ujenzi za Aga Khan, na Wakala wa Aga Khan wa Mikopo Midogo. Aga Khan pia ni mwenyekiti wa Bodi ya Magavana ya Taasisi ya Mafunzo ya Ismailia, aliyoiunda mwaka 1977. Aidha, ni Makamu wa Rais wa Jumuiya ya Madola ya Kifalme.

Pia ipo Focus Humanitarian Assistance, ambalo ni tawi la AKDN, inahusika na kutoa msaada wa dharura wakati wa majanga.

Miongoni mwa majanga ya hivi karibuni ambayo Focus ilihusika katika kutoa msaada ni tetemeko la ardhi la mwaka 2005 nchini Pakistan na tsunami ya Asia Kusini.

Miradi muhimu ya hivi karibuni inayohusiana na maendeleo na inayoongozwa na Aga Khan ni pamoja na Ujumbe wa Imamat ya Ismailia na Kituo cha Kimataifa cha Uendelevu wa Tamaduni cha Ottawa, Jumba la Makumbusho la Aga Khan huko Toronto, Hifadhi ya Al-Azhar jijini Cairo, ukarabati wa Bagh-e Babur jijini Kabul na mtandao wa shule za bweni zinazotumia mtalaa wa Kimataifa, zinazojulikana kama Aga Khan Academies.

Related Posts