AKILI ZA KIJIWENI: Yanga, Singida kuna ‘udugu’ unaendelea?

RAHA ya udugu ni kusaidiana na kama hamuwezi kufanya hivyo basi hamstahili kuwa ndugu au udugu wenu ni wa mashaka.

Kijiweni kwetu hapa tunajiuliza kutokana na yanayotokea kwa Yanga na Singida Black Stars, vipi, kuna kaudugu?

Ni hivi. Klabu hizi zimekuwa zikisaidiana mambo mbalimbali hasa wakati wa shida pindi upande mmoja kunapokuwa na pengo la mtu wa nafasi fulani bila tatizo.

Licha ya kuwa hata klabu nyingine zimekuwa zikipeana wachezaji kwa mkopo au kuuziana, kwa klabu hizi mambo yamekuwa yakienda hivyo hivyo inapotokea uhitaji wa namna hiyo.

Hapa kijiweni tunarejelea tukio la Simba ilipomchukua Kocha Juma Mgunda kutoka Coastal Union kwenda kuifundisha timu hiyo baada ya kuondokewa na kocha wake Maki Zoran katikati ya msimu.

Nao Yanga ilikuwa na shida ya kipa ikapewa Abubakar Khomein, ikahitaji kiungo wakati wa dirisha kubwa la usajili ikapatiwa Duke Abuya na dirisha dogo mwezi uliopita ikawa na mahitaji ya beki wa pembeni ikapatiwa Israel Mwenda.

Kumbuka dirisha kubwa la usajili, Singida Black Stars ilikuwa na uhitaji wa mshambuliaji wa kati ikasaidiwa Joseph Guede ambaye hata hivyo, hakutoboa na akapewa mkono wa kwaheri.

Katika dirisha dogo la usajili, Yanga ilimleta kipa Amas Obasogie ambaye baada ya kugundua namba ya wachezaji wa kigeni imezidi ikampeleka Singida Black Stars.

Wakati ikimtambulisha kipa huyo ni chui, Singida katika akaunti yake ya Instagram waliandika bayana hivi; ‘Amas Obasogie ambaye pia ni Golikipa wa Timu ya Taifa ya Nigeria (The Super Eagles) “NI CHUI” kwa Makubaliano Maalum na Klabu ya Yanga.’

Hata juzi, Yanga baada ya kuondokewa ghafla na Kocha Sead Ramovic ambaye ametimkia huko Algeria anakokwenda kuitumikia CR Belouizdad, uongozi ukalazimika kusaka kocha mwingine kuziba nafasi yake.

Kwa kitendo cha kumnasa aliyekuwa Kocha wa Singida Black Stars Mualgeria Hamdi Miloud ndiyo kinazidi kutupa maswali hapa kijiweni kama huko kitaa mnavyojiuliza, hizi klabu zina ka udugu au vipi?

Related Posts