Utapeli mitandaoni watikisa, Mo alia kudukuliwa

Dar es Salaam. Kufuatia matukio ya udukuzi wa akaunti za mitandaoni yanayosababisha utapeli, wananchi wametakiwa kujifunza elimu ya mitandao ili kuepuka kuingia kwenye majanga.

Hayo yanakuja kufuatia tangazo la mfanyabiashara Mohammed Dewji maarufu Mo, lililotolea leo Februari 6, akiwaomba radhi wasomaji wake kwa machapisho ya ulaghai yaliyochapisha kwenye ukurasa wake wa X yakijaribu kuwadanganya watu baada ya kudukuliwa Februari 5 saa 10:00 jioni na Februari 6 saa 8:00 asubuhi.

“Huu ulikuwa udukuzi wa kulengwa, ambapo wadukuzi walijifanya kuwa timu rasmi ya msaada wa jukwaa. Kwa msaada wa haraka kutoka kwa timu ya usimamizi ya X, tatizo hili limeshughulikiwa na sasa tumerejesha udhibiti kamili wa akaunti yetu,” limeeleza tangazo hilo.

Amewasihi watumiaji wa mitandao kuwa makini na kipaumbele kuwekwa kwenye usalama wa mtandaoni.

“Jihadharini na viungo vya ulaghai na hakikisha unathibitisha uhalisia wa ujumbe wowote unaopokea,” amesema.

Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jamii Forums, Maxence Melo amesema elimu inatakiwa kutolewa kwa watumiaji wa mitandao ili kuepuka kudukuliwa.

“Udukuzi wa mitandao ni tatizo kwa watu wengi, bila kujali kwamba wana vipato au vipi na hii ni kutokana na ukosefu wa elimu mitandaoni.

“Unakuta mtu anatumia nywila muda mrefu bila kuibadilisha au anatengeneza nywila ambayo siyo imara, wakati inatakiwa kuwa imara na iwe na njia ya pili ya uthibitisho kwa kutuma ujumbe wenye jukwaa lingine ili kuthibitisha,” amesema.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA), Jabir Bakari amesema katika taarifa wanazotoa kila baada ya siku 90, inaonekana kadi za simu zimeongezeka hadi kufikia milioni 86, hivyo watumiaji mitandao wameongezeka.

Hata hivyo, amesema uhalifu umepungua.

“Kama hakuna hatua zinazochukuliwa uhalifu usingepungua,” amesema.

Amesema kutokana na maendeleo ya teknolojia, uhaliu pia umehamia huko.

“Tuko kwenye uchumi wa kidigiti, hivyo watu wote hata kama ni mama lishe wanatumia mitandao, hivyo hivyo kwa wahalifu, wanatafuta fedha huko.

“Kikubwa ni elimu, usifanye hiki au hiki, maelekezo yanatolewa mara kwa mara hata kwa ujumbe wa simu na polisi au watoa huduma za simu,” amesema.

Hata alipoandikiwa ujumbe hakujibu.

Hivi karibuni, Bunge limeiagiza Serikali kutumia vyombo vingine ikiwemo Jeshi la Polisi, kudhibiti utapeli na uhalifu wa kimtandao, jambo ambalo limetajwa bado ni janga kubwa linalohitaji hatua madhubuti ili kulidhibiti.

Akiwasilisha taarifa ya miundombinu kwa kipindi cha Februari 2024 hadi Januari 2025 bungeni jijini Dodoma Februari 3, 2025, Mwenyekiti Selemani Kakoso alisema tatizo la utapeli na uhalifu mwingine wa kimtandao ni janga kubwa nchini.

Amesema tatizo hilo limeendelea kuwepo nchini akisema jambo hilo linapaswa kupatiwa ufumbuzi wa kina kwani linatokana na maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) hivyo linaathiri uchumi, jamii, ustawi na maadili.

Kutokana na hilo, Bunge limeazimia mambo matano ikiwemo kuhakikisha TCRA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi inaweka mikakati madhubuti inayozihusisha kampuni za simu kukabiliana na uhalifu wa kimtandao.”

“Iimarishe udhibiti wa uhuru wa mitandao kwa kuzingatia umuhimu wa demokrasia yenye mipaka. Serikali ihakikishe Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na Taasisi ya eGA (Mamlaka ya Serikali Mtandao) wanashirikiana kwa pamoja kutatua matatizo ya Tehama nchini,” amesema Kakoso.

Related Posts