Waziri wa Madini na Rasilimali za Petroli wa Afrika Kusini, Gwede Mantashe ametoa wito kwa nchi za Afrika kusimamisha mauzo ya madini kwenda Marekani.
Mwito huo umetolewa baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kutangaza mipango ya kuikatia misaada Afrika Kusini kutokana na sera zake za unyakuzi wa ardhi. Jumapili iliyopita, Trump alidai kwamba matabaka fulani ya watu nchini Afrika Kusini yanabaguliwa na kunyanyaswa.
Akizungumza katika Kongamano la Uwekezaji wa Madini ya Afrika la Indaba mjini Cape Town, Waziri Mantashe amesema kuwa, mataifa ya Afrika hayapaswi kuogopa vitisho vya Marekani. “Tuzuie madini kwenda Marekani,” alisema waziri huyo.
Aidha alieleza bayana kuwa, “Kama hawatupi pesa, tusiwape madini … sisi sio ombaomba, tutumie madini kwa manufaa yetu. Kama Afrika tutadumaa kwa hofu, tutaanguka na madini mlangoni kwetu.”
Afrika ina takriban asilimia 30 ya madini yote duniani. Baadhi ya madini hayo ni kama vile almasi na dhahabu ambayo ni vyanzo vya asili vya utajiri, na madini mengine hutumiwa viwandani kama vile viwanda vya betri na vyombo vya usafiri vya umeme.