AKILI ZA KIJIWENI: Naogopa kumwekea dhamana Mutale

BAADA ya dirisha dogo la usajili, Joshua Mutale anaonekana kucheza vizuri sana tofauti na ilivyokuwa hapo mwanzoni hadi akajikuta anawaudhi mashabiki wa Simba.

Wakati anasajiliwa, mashabiki wa Simba hapa kijiweni walitutambia kweli wakisema wamenasa bonge la winga ambaye atawafanya mabeki wa timu pinzani walale na viatu kutokana na chenga na kasi yake

Basi tukasubiria mechi za mashindano zianze tuone ukweli au uongo wa hicho walichokuwa wanatuaminisha maana soka ni mchezo unaochezwa hadharani na si unakumbuka ile kauli muwamba ngoma huvutia kwake.

Msimu ulipoanza jamaa akapewa sana nafasi lakini kiwango chake hakikuwa kinawavutia wengi kiasi ambacho ilionekana wazi hatokuwa na maisha marefu ndani ya kikosi cha lunyasi kilichosheheni kweli hivi sasa.

Ikaripotiwa vigogo wa timu hiyo wamepanga kumuonyesha mlango wa kutokea Mutale dirisha dogo ili nafasi yake ichukuliwe na mchezaji mpya wa kigeni kwa vile Simba tayari imeshatimiza idadi ya wachezaji 12 ambao sio raia wa Tanzania.

Hata hivyo, dirisha dogo jamaa hakuondoka na Simba ikaamua kubaki naye na hilo ni kama linaonekana kuanza kumbadilisha taratibu Mutale kwani tangu hapo amekuwa akionyesha kiwango bora katika mechi za timu hiyo.

Mutale anapambania vyema namba hivi sasa, anapiga pasi zinazofika, anapokonya mipira, ana chenga za maudhi na amekuwa akisaidia katika kufungua ukuta wa timu pinzani katika mechi ambazo Simba inacheza za mashindano tofauti.

Baada ya dirisha dogo kufungwa, Mutale amecheza dhidi ya Kilimanjaro Warriors na baadaye alicheza katika mechi ya ugenini dhidi ya Tabora United ambazo zote alikiwasha kweli.

Lakini tunakumbushana hapa kuwa tulikubaliana mechi mbili ni chache na hazitoshi kumpima mchezaji hivyo tunataka kumtazama zaidi Mutale ili tujiridhishe kama kiwango chake kimepanda kwa sababu ya kukoswakoswa na panga la kufyekwa kwenye dirisha dogo au nguvu za soda tu.

Related Posts