Ripoti ya CAG yaondoka na watumishi wa halmashauri 20

Dodoma. Jumla ya watumishi 294, wakiwamo wakurugenzi na waweka hazina wa halmashauri, wamechukuliwa hatua.

Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na watumishi 20 kufukuzwa kazi na watano kufungwa jela kufuatia taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya ukaguzi wa mwaka wa fedha 2022/23.

Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Festo Dugange ameyasema hayo leo Februari 6, 2025 wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Subira Mgalu.

Mbunge huyo amehoji Serikali inachukua hatua gani kwa maofisa masuuli na wahazini wa Serikali za Mitaa kutokana na ongezeko la hoja za ukaguzi za ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Akijibu swali hilo, Dk Dugange amesema taarifa za CAG zinaonesha mwenendo wa hati za ukaguzi kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa umeendelea kuimarika mwaka hadi mwaka.

Amesema katika kipindi cha miaka minne (2019/20 hadi 2022/23), hati Safi zimeongezeka kutoka 124 sawa na asilimia 67 mwaka 2019/20 hadi Hati 181 sawa na asilimia 98.4 mwaka 2022/23.

Aidha, amesema hati zenye shaka na hati mbaya zimepungua kutoka 61 sawa na asilimia 33 mwaka 2019/20 hadi hati 3 sawa na asilimia 1.6 mwaka 2022/23.

Amesema mwenendo huo mzuri wa hati za ukaguzi na utekelezaji wa mapendekezo ya ukaguzi umechangiwa na uchukuaji wa hatua za kisheria na kinidhamu kwa watumishi wanaosababisha hoja za ukaguzi au hasara kutokana na kutotekeleza wajibu wao kikamilifu au kujihusisha na vitendo vya ubadhirifu.

Amesema kufuatia taarifa ya CAG ya ukaguzi wa mwaka wa fedha 2022/23, jumla ya watumishi 294, wakiwemo wakurugenzi na waweka hazina, wamechukuliwa hatua mbalimbali zikiwemo kufukuzwa kazi (20), kifungo jela (5), kufikishwa mahakamani (30), kushushwa cheo (1), kupewa onyo (100), kukatwa mshahara (14) na kufikishwa polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa uchunguzi (114).

“Serikali inaendelea kuboresha mifumo ya udhibiti ili kuimarisha usimamizi wa rasilimali za umma na kupunguza hoja za ukaguzi, na itaendelea kuchukua hatua za kisheria kwa watakaokiuka taratibu zilizopo,” amesema.

Katika swali la nyongeza, Subira amesema kuwa ingawa Serikali inasema kuwa ubadhilifu umepungua,lakini bado dhana ya ubadhilifu na matumizi mabaya ya Serikali yamengezeka iko kwa wananchi.

“Je, Serikali ipo tayari kuunda kitengo kwa kushirikiana na ofisi ya CAG na Bunge kwenye kamati zake kuelimisha umma kujua tafsiri sahihi na hatua zilizochukuliwa,”amehoji.

Amehoji serikali iko tayari kufanya utafiti kujua tatizo nini ambalo linawafanya maofisa masuhuli kutojibu hoja za CAG ili iweze kuchukua hatua.

Akijibu maswali hayo, Dk Dugange amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua ili kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma.

“Kuhusu kitengo maalumu cha kutoa elimu kwa umma tunapokea mawazo hayo mazuri lakini halmashauri zetu zinaendelea kuelimisha wananchi kuwa serikali inachukua hatua juu hilo,”amesema Dk Dugange.

Amesema kumekuwa na matatizo katika utunzaji wa nyaraka katika halmashauri na hivyo wakati wa ukaguzi hazipatikani mara moja na hivyo kupatikana baada ya muda fulani.

“Tumeelekeza halmashauri zetu kuhakikisha nyaraka zote zinapatikana kwa wakati, wakati wakaguzi wa CAG wapo ili hoja zote zifungwe haraka iwezekanavyo badala ya kusubiri muda mrefu,”amesema Dk Dugange.

Related Posts