Dar es Salaam. Serikali imesema upelelezi katika kesi ya kusambaza taarifa za uongo katika Mtandao wa X, inayomkabili wanasiasa mkongwe nchini, Willibrod Slaa (76), bado haujakamilika.
Wakili wa Serikali Agness Mtunguja ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Alhamisi Februari 6, 2025 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Mtunguja ametoa maelezo hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Rahim Mushi.
Wakati kesi hiyo inatajwa na kuahirishwa leo, Dk Slaa amefikisha siku 28 akiwa rumande kutokana na upelelezi wa shauri lake kutokukamilika, huku pia Serikali ikiwasilisha zuio la dhamana ya mshtakiwa huyo mahakamani hapo.
Zuio hilo liliambatana na kiapo kilichoandaliwa na mpelelezo wa kesi hiyo, Mrakibu mwandamizi wa Polisi (SSP), George Wilbroad Bagyemu.
Kwa mara ya kwanza Dk Slaa alifikishwa katika Mahakama hiyo, Januari 10, 2025 na kusomewa kesi ya shtaka moja la kusambaza taarifa za uongo katika mtandao wa X.
Slaa anadaiwa kutenda kosa hilo chini ya kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao namba 14 ya mwaka 2015.
“Shauri limeitwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado haujakamilika hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa,” amesema Wakili Mtunguja.
Hakimu Mushi baada ya kusikiliza kesi hiyo aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 19, 2025 itakapotajwa.
Kesi hiyo imeahirishwa kwa hakimu Mushi, kutokana na hakimu anayesikiliza shauri hilo, Beda Nyaki kuwa likizo.
Hata hivyo, mshtakiwa huyo hakuletwa mahakamani hapo na upande wa mashtaka hawakueleza sababu ya mshtakiwa huyo kutokuletwa.
Kutokana na mahtakiwa kutokuletwa mahakamani hapo, Wakili anayemtetea Dk Slaa, Sanga Melikior ameiomba Mahakama hiyo itoe hati ya wito ya kumuita mshtakiwa kutoka gerezani kwenda mahakamani kwa tarehe itakayopangwa.
Ombi hilo lilikubaliwa na kutolewa kwa hati hiyo kwamba tarehe ijayo mshtakiwa huyo ataletwa mahakamani hapo.
Pamoja na kesi hiyo kutwajwa katika mahakama hiyo, tayari Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP) amewasilisisha kusudio la kukata rufaa Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi uliotolewa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, ambao ulielekeza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kushughulikia suala la dhamana ya mwanasiasa huyo pamoja na mambo mengine.
Notisi hiyo ya kupinga uamuzi huo iliwasilishwa Mahakama ya Rufani na kusajiliwa katika mfumo Januari 30, 2025 na sasa inasubiriwa kupangiwa Jaji kwa ajili ya usikilizwaji.
Kutokana na DPP kuwasilisha kusudio hilo la kukata rufaa, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilimueleza mshtakiwa huyo kuwa, kwa sasa imefungwa mikono kuendelea na kesi ya msingi hadi hapo Mahakama ya Rufaa itakaposikiliza rufaa iliyokatwa na DPP na kuitolewa uamuzi.
Taarifa ya Serikali kukata rufaa iliwasilisha katika Mahakama ya Kisutu, Januari 31, 2025 na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Job Mrema.
Siku hiyo, Wakili Mrema aliileza mahakama hiyo kuwa, Serikali imekata rufaa Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu kuhusiana na maombi yaliyowasilishwa na Dk Slaa, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Mrema alidai upande wa mashtaka uliwasilisha notisi ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo, Januari 30, 2025 katika Mahakama ya Rufaa.
Wakili Mrema alitoa taarifa hiyo mbele ya hakimu Nyaki, baada ya Serikali kuitikia wito wa Mahakama uliowataka mawakili wa pande zote mbili yaani upande wa mashtaka na ule wa utetezi kufika siku hiyo Mahakama ya Kisutu kwa ajili ya kusikiliza maelekezo.
Kutokana na hali hiyo, mshtakiwa atakuwa anapelekwa mahakama ya Kisutu kwa ajili ya kutajwa kila baada ya siku 14 kwa sababu upande wa mashtaka uliweka zuio kwa mshtakiwa huyo kupewa dhamana.
Sababu za pingamizi hilo la Serikali, linatokana na uamuzi wa Mahakama Kuu uliotolewa na Jaji Arnold Kirekiano, Januari 30, 2025, ambao ulielekeza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kushughulikia suala la dhamana ya mwanasiasa huyo na kutoa uamuzi wa pingamizi la uhalali wa kesi ya jinai inayomkabili mahakamani hapo kwa haraka.
Mbali na maelekezo hayo kwa mahakama ya Kisutu, pia kupitia sakata la dhamana ya mwanasiasa huyo, Mahakama Kuu ilitoa maelekezo maalumu kwa mahakama zote za chini namna ya kushughulikia suala dhamana za washtakiwa wa kesi za jinai.
Dk Slaa ambaye amewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na mgombea urais kupitia chama hicho katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 alifungua mashauri hayo kutokana na mwenendo wa kesi ya jinai inayomkabili katika Mahakama ya Kisutu.
Katika mashauri hayo, mbunge huyo mstaafu wa jimbo la Karatu alikuwa akiiomba mahakama hiyo iitishe na kupitia mwenendo wa shauri dogo lililofunguliwa na Jamhuri kupinga dhamana yake na wa kesi ya msingi, kujiridhisha na usahihi na uhalali wake.