Mwanamke mmoja aliyefika hospitali kwa ajili ya kujifungua, inadaiwa amefariki dunia katika Jimbo la Imo nchini Nigeria baada ya daktari kufanya upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni (CS) kwa msaada wa maelekezo ya video ya mtandao wa YouTube Februari 4 mwaka huu.
Kwa mujibu wa mtandao wanahabari wa News360 nchini humo, umeeleza kuwa njia hiyo ya kujifungua kwa upasuaji, mtoto hutolewa kupitia upasuaji kwenye tumbo na mfuko wa uzazi wa mama.
Mume wa marehemu, Onyekachi Eze akiwa ameandamana na mtayarishaji maarufu wa filamu za Nollywood, Stanley Ontop, alitembelea Kituo cha Polisi cha Jimbo la Imo siku ya Jumanne ili kuripoti tukio hilo.
Eze alifichua kuwa mkasa huo ulitokea katika Hospitali ya Lebechi huko Owerri, mji mkuu wa Jimbo la Imo.
Akiwa anasimulia tukio hilo, Eze alisema, “Nilimpeleka mke wangu hospitalini alipokuwa katika uchungu wa kujifungua na daktari akasema anahitajika kufanyiwa upasuaji kwa sababu alikuwa akivuja damu.”
“Hivyo basi, daktari wa kike alimwita daktari mwingine ili afanye upasuaji huo. Mbele yangu, walikuwa wakitumia simu zao kutazama video ya YouTube jinsi ya kufanya upasuaji huo, nikampoteza mke wangu pamoja na mtoto wangu katika mchakato huo,” amesimulia.
Muda mfupi baada ya ripoti hiyo, Stanley alionyesha video inayoonyesha mmiliki wa hospitali hiyo akikamatwa na polisi baada ya madaktari hao kutoroka.
Akiandika maelezo ya video hiyo alisema, “Mmiliki wa hospitali ambako madaktari walikuwa wakitazama YouTube ili kujifunza jinsi ya kufanya upasuaji kwa mwanamke mjamzito amekamatwa.
“Wauguzi pia wamekamatwa, lakini madaktari waliokuwa wakijianda kufanya upasuaji huo wametoroka na wanatafutwa na polisi,” ameandika Eze.