UCHAMBUZI WA MALOTO: Upacha wa CCM na wasanii wa Bongo Movie, Bongo Flava

Januari 16, 2025 watu maarufu, hasa wasanii wa makundi yote wakiwamo waigizaji wa filamu na tamthiliya (Bongo Movie), wanamuziki, wachekeshaji, na wenye ushawishi mitandaoni (influencers), walionekana kwenye treni ya SGR.

Walikuwa wakitokea Dar es Salaam, kwenda Dodoma, kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), uliofanyika Januari 18 na 19, 2025 kwenye ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete.

Hoteli za Jiji la Dodoma zilifurika wasanii utadhani nao ni wajumbe wa Mkutano Mkuu CCM.

Kisha tena, Februari 3 na 4, 2025, Dodoma ikapokea ugeni wa wasanii lukuki. Walifika kwa ajili ya sherehe za CCM kutimiza miaka 48 ya kuzaliwa. Walivaa nguo za kijani, njano na nyeusi. Walijipambanua dhahiri kuwa wafuasi wa chama hicho.

Kisiasa, kuna nadharia inaitwa “celebrity politics” – “siasa zenye kuegemea watu mashuhuri.” Wakati mwingine huitwa “political star power” – “nguvu ya watu mashuhuri kwenye siasa.” CCM inacheza karata hii kwa nguvu kubwa hadi kupitiliza. Inafuja.

CCM ina bendi yake rasmi ya muziki, Tanzania One Theatre (TOT). Imekuwa ikifanya kazi za kampeni kwenye mikutano ya hadhara, hadi utunzi wa nyimbo za mapambio ya chama. TOT chini ya marehemu John Komba, ilitia fora.

Hata kabla ya uchaguzi mkuu wa kwanza uliohusisha vyama vingi vya siasa, Komba alishakuwa maarufu nchi nzima. TOT ilijulikana kila mahali. Hata vyama vya upinzani vilijitutumua kupitia ngoma za asili na wanamalenga, lakini CCM na TOT yao walikuwa mbele ya muda.

Uchaguzi Mkuu 1995 na 2000, TOT ilikuwa kitovu cha burudani kwenye mikutano ya kampeni za CCM, kumnadi aliyekuwa mgombea urais, Benjamin Mkapa. Karata ya “political star power”, CCM waliicheza kupitia wanamuziki wa Taarab na Dansi.

Komba mwenyewe, halafu Khadija Kopa, marehemu Ramadhan Masanja “Banza Stone”, Abdul Misambano, na wengine. CCM iliweza kuvuna nguvu ya watu maarufu na kuiegemea kama mtaji wake wa kisiasa.

Kuanzia miaka ya 1990, muziki wa Rap ulianza kuteka kundi kubwa la vijana. Rap halafu ikaja R&B (Rhythm and Blues), asili yake ni Marekani. Ulipotua Tanzania, na mahadhi hayo kuimbwa kwa Kiswahili na kuchomeka vionjo vya Kitanzania, ikawa sababu ya kuzaliwa jina la Bongo Flava.

Hadi mwanzoni mwa miaka ya 2000, Bongo Flava siyo tu ulishakuwa muziki wa kibiashara, bali wanamuziki wa mahadhi hayo walishaanza kutengeneza majina na maisha, vilevile walishajenga ushawishi mkubwa kwenye jamii.

Uchaguzi Mkuu 2005, CCM walikuwa mbele ya nyakati kuwawahi wanamuziki wa Bongo Flava na kuwatumia kwenye kampeni za mgombea urais wao, Jakaya Kikwete. Wanamuziki, Juma Kassim Ally Kiroboto “Juma Nature” na Albert Kenneth Mangweha “Ngwair”, walikuwa vinara wa Bongo Flava kumnadi Kikwete.

Uchaguzi Mkuu 2010, CCM iliendelea kunufaika kupitia nguvu ya watu maarufu, kupitia wanamuziki Lawrence Marima “Marlaw”, Diamond Platnumz na timu yote ya Tanzania House of Talents (THT). Nyakati zote, bendi ya TOT iliendelea, Komba na Khadija Kopa, kama ada.

Uchaguzi Mkuu 2015, CCM iliendelea kuvuna kundi kubwa la wanamuziki, ambao walipanda jukwaani kurap na kuimba, kuifanyia kampeni. Hata wapinzani, hasa Chadema, kupitia mgombea urais wake, Edward Lowassa, ilipata wasanii maarufu wachache.

Emmanuel Elibariki “Nay wa Mitego”, Kala Jeremiah na Juma Nature, ambaye baadaye alihamia kambi ya mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli. Angalau upinzani uliweza kucheza karata ya nguvu ya watu mashuhuri kwenye siasa.

Chadema, walinufaika pia kupitia mmoja wa waasisi wa Bongo Flava, Joseph Mbilinyi “Sugu”, vilevile mwanamapinduzi wa Bongo Flava, Joseph Haule “Prof Jay”, ambao siyo tu walipanda majukwaani kumnadi Lowassa wa Chadema, bali pia wao wenyewe waligombea ubunge na kushinda.

Sugu, aliingia bungeni mwaka 2010, jimbo la Mbeya Mjini, akatetea kiti hicho mwaka 2015, wakati Prof Jay, alishinda ubunge kwa mara ya kwanza mwaka 2015, jimbo la Mikumi. Wakati huohuo, ACT-Wazalendo, walimpata mmoja wa magwiji wa Rap, Suleiman Msindi “Afande Sele”, na nyota wa muziki wa asili, Vitali Maembe.

Hiyo ni kuonyesha kuwa pamoja na CCM kuwa kinara wa kucheza karata ya “political star power”, kuna wakati, vyama vya upinzani, hasa Chadema na ACT-Wazalendo, vimewahi kunufaika na nguvu ya ushawishi kutoka kwa watu maarufu.

Kama Sugu na Prof Jay, kutoka kuwa nyota wa muziki hadi ubunge, kama Ronald Reagan, alishakuwa nyota wa filamu ya “The Bad Man”, baadaye akachaguliwa kuwa Gavana wa California, kisha Rais wa Marekani. Umaarufu wa sanaa hupalilia barabara ya kisiasa.

Ni sawa na Hamis Mwinjuma “MwanaFA”, ni stadi wa muziki wa Rap, aliyechaguliwa kuwa mbunge jimbo la Muheza, Tanga, na sasa ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Khadija Shaban “Keisha” ni mbunge Viti Maalumu CCM, naye ni mwanamuziki.

Komba, alikuwa mbunge kupitia CCM, vilevile mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) CCM. Hata Khadija Kopa, amepata kuwa mjumbe wa Nec. Mwenyekiti wa Aset, kampeni inayomiliki bendi ya African Stars “Twanga Pepeta”, naye ni mjumbe wa Nec CCM.

Inazidi kuimarisha hoja kwamba vyama vya siasa nchini, tangu mfumo wa vyama vingi, vimekuwa vikijaribu kucheza karata ya kuegemea watu mashuhuri. Faida yake kubwa ni kwamba watu maarufu wanaweza kushawishi chama au mgombea kuungwa mkono na jamii.

Watu maarufu wanapendwa na jamii. Ni rahisi watu wanaowapenda, wakavutiwa kumpigia kura mgombea au kukiunga mkono chama, kwa sababu ya ushawishi wa mtu maarufu wanayempenda.

Marekani, Oprah Winfrey, Beyonce Knowles na Shawn Carter “Jay Z”, ni miongoni mwa watu mashuhuri waliosimama kumuunga mkono Barack Obama, alipogombea urais wa nchi hiyo mwaka 2008. Mtaalamu wa Rock, Blues na Country, Hank Williams Jr, alitunga wimbo kumpigia debe, John McCain, aliyekuwa akichuana na Obama.

Kuna faida kubwa CCM inapata kupitia kuungwa mkono na watu maarufu. Kama ambayo chama cha Republicans Marekani, kilivyonufaika kupitia gwiji wa Hollywood, Arnold Schwarzenegger, akawa mpaka Gavana wa California, au siasa za India na nyota wa Bollywood, Amitabh Bachchan.

Political star power ina nguvu pale mtu maarufu anapokuwa huru. Nyota wa filamu au muziki, anafahamika hivyo, siku akitokeza kumuunga mkono mgombea fulani au chama chochote kutokana agenda au sera, inajenga ushawishi kwa jamii. Watu wanaompenda watavutiwa na msimamo au mtazamo wake.

Mkutano Mkuu CCM uliofanyika Januari 18 na 19, 2025, vilevile sherehe za maadhimisho ya miaka 48 ya CCM, kwa pamoja, matukio hayo mawili, yamewapambanua wasanii wengi wa Bongo Flava na Bongo Movie, katika upacha wa hali ya juu na CCM.

Mwanzoni CCM iliwatumia wanamuziki wa Bongo Flava kwenye kampeni, kuvuta watu wahudhurie mikutano kwa wingi, sasa hivi wanamuziki wa Bongo Flava wamekuwa CCM kuliko wanachama vindakindaki. Wanavaa sare za chama, wanaimba nyimbo, wanahudhuria vikao na wanalipwa posho kama wajumbe.

Bongo Movie, kadhalika. Ilipo CCM ndipo na wao wapo. Ni kama imekuwa fasheni kwa sasa wacheza filamu kuishabikia CCM. Wapo wasanii wanasema wanaiunga mkono CCM kwa sababu wanampenda Rais Samia Suluhu Hassan. Ni sawa. Ni haki. Inawezekana kumpenda na kumuunga mkono Rais Samia bila kuvalia nguo za CCM.

Matumizi ya sasa ya watu maarufu ni ufujaji. Alikiba atakuwa na kipya kipi wakati wa kampeni ikiwa anafahamika ni CCM? Vivyo hivyo Diamond Platnumz, AY, Madee, Chegge na wengine wengi.

Shabiki wa muziki wa Harmonize ambaye haipendi CCM, hatakuwa na kitu cha kumfanya abadili mawazo kupitia mwanamuziki huyo, maana anajua ni CCM kindakindaki. Hili ni kosa ambalo CCM wanafanya.

Kwa wanamuziki wenyewe, ipo namna wanashusha thamani yao. Mitandaoni kwa sasa wanaitwa chawa, wakati kazi zao ziliwapa heshima.

Upatikanaji kila mara kwenye matukio ya CCM, hadi mikutano, wakiwa wamevaa sare za chama, haiwapambanui kuwa wenye fikra huru. Inaonekana wanavutwa kwa pesa, au ni bendera fuata upepo.

Kwa CCM, watu maarufu ni mtaji mzuri kwenye kampeni. Mtaji huo utatengeneza faida kama haitawafuja watu maarufu ilionao. Isiwafanye watu maarufu kuwa tawi la CCM, iwaache wabaki kuwa watu wenye ushawishi kwenye jamii.

Siku wanaposimama jukwaani kuomba kura, wakiposti mitandaoni, au wakiimba nyimbo, zitakuwa na nguvu ya ushawishi.

Related Posts