Nyumba 100 pembezoni hatarini kusombwa Bahari ya Hindi

Unguja. Takirban nyumba 100 zilizo pembezoni mwa Bahari ya Hindi kwenye Kijiji cha Nungwi Wilaya ya Kaskazini ziko hatarini kwa kusogelewa na bahari na wameiomba Serikali kuwanusuru na hatari hiyo.

Wakizungumza na Mwananchi digital kwa nyakati tofauti leo Februari 6, 2025, wakazi wa eneo hilo lililopo Mkoa wa Kaskazini Unguja wamesama hali hiyo inatokana na mabadiliko ya tabia nchi kiasi cha kutishia kugharimu maisha yao na shughuli za kiuchumi.

Mkazi eneo hilo, Khamis Hafidh Ali amesema mabadiliko ya tabianchi yanatishia maisha na shughuli za kiuchumi kwa wakazi hao wanaoishi pembezoni mwa bahari.

Amesema kuwa wanakadiria makazi yanayoathirika kutokakana na bahari kusogea zinaweza kufika nyumba zaidi ya 100 ambazo zipo pembezoni mwa bahari.

“Kwa miaka ya nyuma bahari ilikua umbili wa zaidi ya mita 100, sasa maji ya bahari yamefika katika makazi ya watu tufanyeje? Hali sio nzuri Serikali ije kwa ajili ya kuliona hili na kulitafutia ufumbuzi wa haraka kinyume na hapo hali itazidi kuwa mbaya kwetu,” amesema Khamis.

Hivyo, ameiomba Serikali kuliangalia vizuri suala hilo kwa lengo la kulitafutia ufumbuzi kwani wao hawawezi kukabiliana na hali hiyo bila msaada wao.

“Licha ya juhudi zinazochukuliwa bado  mabadiliko ya tabianchi yamebaki kuwa tatizo na hali ilivyo kwa sasa bila ya ushirikiano baina yetu na Serikali hatutaweza kukabiliana nalo tatizo hili,” amesema Khamis.

Alisema mwaka 1983 Serikali ilijenga ukuta katika ufukwe wa Nungwi ili kuzuia maji ya bahari yasifike katika maeneo ya watu, lakini jambo hilo  halikua suluhisho kwani ukuta huo ulianguka kutokana na nguvu ya maji ya bahari na kusababisha sehemu ya ardhi kumomonyoka na bahari kusogelea makazi ya watu.

Mkazi mwengine, Said Ali amesema mabadiliko ya tabianchi yanawaathiri katika shughuli za kiuchumi hasa kipindi cha upepo wa kusi na kaskazi zinapovuma.

Amesema upepo huo unapovuma kawaida wakazi wa kijiji hicho inawalazimu kusitisha shughuli zao katika maeneo ya bahari, kwani inakuwa ni hatari kwao.

“Katika kipindi hicho wakazi wa maeneo hayo tunaishi kwa hofu ya kuangukiwa na miti au kupata athari nyingine katika makazi yetu,” amesema Said

Amesema mbali na hayo, katika kipindi cha upepo huo husababisha magonjwa na njaa kwa sababu wakazi hushindwa kuendelea na shughuli zao zinazowapatia kipato.

Akitoa ufafanuzi wa maombi hayo, ofisa uhusiano halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja, Khamis Said Saleh amesema wilaya hiyo imeathirika na itaendelea kuathiriwa na hali hiyo endapo wakazi wa kijiji hicho hawatobadili mfumo wa maisha unaochangia kutokea kwa mabadiliko ya tabianchi.

Amesema, mabadiliko ya tabianchi yanahitaji mikakati ya muda mrefu, ikiwa pamoja na kuimarisha miundombinu, kulinda mazingira, na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu hatua za kukabiliana nazo.

Hata hivyo, amewataka wakazi wa maeneo hayo kutuza mazingira na kuacha kuchoma taka ovyo kwani kunasabibisha kutoboka kwa ozon layer na kushuka kwa mionzi mikali na kupata maradhi ya ngozi.

Pia, amewataka wananchi kuacha tabia ya kukata miti  na inapobidi kufanya hivyo wapande miti mingine ili kuepukana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Halmashauri hii itaendelea kusimamia masuala hayo ili jamii isiendelee kuathirika zaidi kutokana na hali hiyo, pia wananchi wa eneo hilo wanapaswa kutulia huku Serikali ikitafuta njia mbadala ya kutatua changamoto hiyo,” amesema Saleh.

Amefafanua kuwa mabadiliko ya tabianchi yanachangia ongezeko la joto, mabadiliko ya mifumo ya mvua, ongezeko la majanga ya asili kama mafuriko, ukame, na vimbunga na kuacha athari kubwa kwa mazingira, jamii, na uchumi.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Zanzibar ina maeneo 148 ambayo yameathiriwa na mabadiliko ya tabianchi.

Related Posts