Tehama yawezesha kufungua kesi bila kufika mahakamani

Morogoro. Matumizi ya Tehema katika mahakama nchini yamerahisisha ufunguaji wa kesi ambapo mlalamikaji anaweza kufungua kesi bila kulazimika kufika mahakamani wala kuonana na karani.

Pia, Tehema imewezesha kupunguza vitendo vya rushwa na malalamiko ya ucheweshaji wa kesi.

Hayo yamesemwa leo Februari 6, 2025 mkoani Morogoro na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Profesa Elisante Ole Gabriel wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi wa mahakama ambayo hutolewa kila baada ya miezi mitatu.

“Sasa hivi mwananchi anaweza kufungua shauri akiwa popote halazimiki kufika mahakamani wala kuonana na karani ama mtumishi wa mahakama, mwananchi anaweza kupata nalala ya hukumu au mwenendo wa shauri kidigotali, kwa msingi huo hakutakiwa na mazingira ya rushwa wala Ile njoo kesho njoo kesho kutwa,” amesema Profesa Gabriel.

Amesema Tehama imekuwa na mchango mkubwa katika kupunguza mlundikano wa kesi, kutoka asilimia tano hadi asilimia nne na kiwango cha umalizaji wa kesi kimeongezeka kutoka asilimia 100 hadi asilimia 101.

“Hizi mahakama zinazotembea zimeweza kuwasaidia wananchi wenye kipato kidogo ambao wanashindwa kusafiri umbali mrefu kutafuta haki, lakini pia mahakama hizi zimesaidia kuokoa muda,” amesema Profesa Gabriel.

Amesema mashauri yanayoongoza kufunguliwa kwenye mahakama mbalimbali hapa nchini ni yale yanayohusu migogoro ya ardhi, biashara na mirathi, hata hivyo Ili kumaliza haraka mashauri hiyo mahakama imeweka divisheni maalumu ya mashauri ya ardhi na biashara.

Akizungumzia miradi inayotekelezwa na mahakama Profesa Gabriel amesema hadi kufikia Desemba 2024 miradi inayoendelea kuboreshwa ni pamoja na ujenzi wa majengo ya vituo Jumuishi vya utoaji haki vipatavyo tisa katika mikoa ya Katavi, Simiyu, Songwe, Ruvuma, Geita, Lindi, Njombe, Singida na Pemba pamoja na ujenzi wa mahakama za mwanzo katika mikoa mbalimbali hapa nchini.

“Mradi mwingine ni ujenzi wa nyumba 48  za majaji na kwamba ujenzi huo umefikia asilimia 98,” amesema Profesa Gabriel.

Janet Sheiza akizungumzia utendaji wa mahakama amesema miaka ya zamani mahakama ilikuwa na changamoto nyingi ikiwemo uchakavu wa majengo, uchache wa makarani na hata vitendea kazi zikiwemo kompyuta, lakini kwa sasa mahakama zimeboreshwa.

“Sasa hivi shughuli za mahakama zinafanywa kidijitali hii imeweza kurahisha mashauri kumalizika kwa haraka lakini pia kupunguza mazingira ya rushwa,” amesema Janeth

Naye msaidizi wa mawakili wa kujitegemea, Ivan Msimbe amesema maboresho mazuri yaliyofanywa na mahakama ni pamoja na kuimarisha Tehama ambapo wao kama mawakili wanaweza kumuwakilisha mteja mahakamani kwa njia ya mtandao.

“Hata mashauri ya kuwasilisha mahakamani tumeweza kuwasilisha kidijitali, hii imetupunguzia usumbufu kwetu na wateja wetu,” amesema Msimbe.

Related Posts