Kafulila: Uchumi hauwezi kujengwa kwa kodi na mikopo pekee

Dar es Salaam. Licha ya Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kutumia kodi na mikopo, ushiriki wa sekta binafsi umetajwa kuwa michango mkubwa katika maendeleo hayo.

Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, sekta binafsi imechangia asilimia 23.9 ya mtaji katika pato la ndani la Tanzania kwa mwaka 2023, kupitia ajira, ubunifu na kodi.

Akizungumza katika kipindi cha Dakika 45 cha televisheni ya ITV mwanzo wa wiki hii, Mkurugenzi wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta Binafsi na Sekta ya umma (PPP), David Kafulila amesema Serikali haiwezi kukidhi mahitaji yote ya wananchi bila kutumia michango wa sekta binafsi.

“Mahitaji ya binadamu ni makubwa kuliko uwezo wa Serikali kutumia kodi na mikopo kuyafikia. Ili kufikia matarajio ya wananchi, utaratibu wa kutafuta njia mbadala, ni kitu kilichofikiriwa sana.

“Tunahitaji kuingiza sekta binafsi ambazo zitatekeleza kile ambacho Serikali imeshindwa kutekeleza, na hiyo ndio dhana ya PPP,” amesema.

Ametoa mfano wa Kampuni ya Azam Marine ya Bakhresa iliyotoa vivuko katika eneo la Kivukoni kwa ajili ya kusafirisha abiria kwenda na kurudi Kigamboni.

“Bakhresa wanaleta vivuko badala ya Temesa (Wakala wa Ufundi na Umeme), tuna bandari Serikali imeingia ubia na DP World. Kwa hiyo, kwa hiyo tunaingia ubia kwa ajili ya kupata mitaji na ufanisi, kwa sababu uzoefu umeonyesha sekta binafsi zina uwezo kuliko Serikali,” amesema.

Amegusia pia suala la usafiri jijini Dar es Salaam, akisema bado Serikali iko kwenye hatua za kisheria kutoa zabuni kwa kampuni mojawapo ya Dubai kuleta mabasi ya mwendo wa haraka jijini humo.

“Awali kulikuwa na kampuni ya Dubai ambayo ilitaka ilete mabasi, ni suala ambalo liko kwenye hatua za kisheria kwa sasa ni nje ya mamlaka ya PPP, kama itakubalika ndio tutajua twende hatua gani,” amesema.

Mbali na miradi hiyo, Kafulila ametaja mradi wa jengo la biashara lililopo Kariakoo Dar es Salaam linalotarajiwa kuwa kituo kikubwa cha biashara.

Amezungumzia pia mkutano wa nishati uliotanisha baadhi ya wakuu wa nchi za Afrika jijini Dar es Salaam wiki iliyopita, akisema umuhimu wa sekta binafsi pia ulibainishwa.

“Tuna ajenda ya watu milioni 300 wafikiwe na umeme, gharama ote ni takribani Dola 13 bilioni lakini Dola 5 bilioni zitatokana na sekta binafsi.

“Maana yake hiyo ni kazi ya kutengeneza miundombinu ya umeme kwa ubia kama sehemu ya utekelezaji wa Azimio la Mkutano wa Nishati.

Katika jukumu hilo, amesema Serikali italazimika kushirikisha sekta binafsi ili kuwafikia wananchi ambao hawajaunganishwa na umeme hasa wa vijijini.

Ameendelea kusema kuwa Serikali imeshatekeleza jukumu lake la uzalishaji wa umeme kupitia miradi mbalimbali ukiwemo wa Bwawa la Umeme la Julius Nyerere na sasa jukumu la kusafirisha na kusambaza litakuwa shirikishi.

“Mpaka sasa hivi tuna umeme wa kutosha, hata kama hautoshi kwa muda mrefu, sasa mkakati ni kuongeza uzalishaji na kuusambaza huo umeme.

“Maeneo yote haya yanahitaji uwekezaji wa Serikali na sekta binafsi ili kuyafikia na kwa ufanisi kwa sababu kodi peke yake haiwezi kufikia,” amesema.

Katika kilimo, amesema Serikali pia imeongeza uwekezaji kwa kuoongeza bajeti ya Wizara ya Kilimo.

“Utakumbuka kwamba wakati mheshimiwa Rais (Samia Suluhu Hassan) anaingia madarakani, bajeti ya kilimo ilikuwa inatengwa Sh250 bilioni, leo imefika zaidi ya Sh1 trilioni. Ni kweli umasikini bado upo, lakini kuna juhudi zinafanywa.

“Vituo vya afya vilivyojengwa inawezekana havina dawa, lakini kwamba havina maana yoyote? Hapo tutabishana,” amesema.

Related Posts