Wakurugenzi wastaafu MCL wanavyomkumbuka Mtukufu Aga Khan

Dar es Salaam. Watendaji wakuu wastaafu wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) wamemwelezea aliyekuwa kiongozi mkuu wa madhehebu ya Ismailia duniani, Mtukufu Aga Khan kama kiongozi aliyetumia maisha yake yote kusaidia jamii katika nchi zote alizowekeza.

MCL, inayochapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na MwanaSpoti ni moja ya kampuni tanzu za Nation Media Group (NMG), kampuni iliyoasisiwa na Mtukufu Aga Khan kupitia Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN), unaosimamia kampuni nyingine nyingi.

Mtukufu Aga Khan, Imamu 49 wa madhehebu ya Shia Ismailia, alifariki dunia Februari 4, 2025, akiwa na umri wa miaka 88.

Mwanaye, Mwana Mfalme Rahim Al-Hussaini ameteuliwa kuwa Imamu wa 50 akichukua nafasi ya kiongozi huyo.

Watendaji hao wakuu wamesema Aga Khan IV alikuwa mwenye maono ya muda mrefu, aliyeamini katika maendeleo ya jamii na aliyetoa nafasi kwa wataalamu.

Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Bakari Machumu amesema alianza kumfahamu Mtukufu Aga Khan kwa kufuatilia alivyoanzisha kampuni ya magazeti ya Nation na Taifa Leo nchini Kenya, akiwa na umri wa miaka 24.

Machumu amesema huo ulikuwa uthubutu wa hali ya juu na maono mapana ya kuisaidia jamii, kupitia utoaji wa taarifa za kuchochea maendeleo na uwajibikaji kupitia utawala bora.

“Alikuwa mtu aliyelenga kuisaidia jamii ambayo vyombo vyake vya habari vilikuwa vinafanyia kazi. Kwa hiyo, ukiangalia AKDN msingi mkubwa ulikuwa service to humanity (huduma kwa ubinadamu).

“Kwa hiyo unaweza kumwelezea Mtukufu Aga Khan kama mtu aliyekuwa na msimamo, aliamini kitu ukikifanya vizuri kitakulipa,” amesema Machumu ambaye pia alifanya kazi kama mhariri wa gazeti la The Citizen na hatimaye mkurugenzi mtendaji kwa jumla ya miaka 20.

Amesema Mtukufu Aga Khan alijitolea maisha yake kuhudumia binadamu wengine, kwa hiyo ni kinara mwenye mchango mkubwa kwa dunia, aliyeondoka baada ya kutimiza kazi aliyokuja kuifanya.

Amesema alikuwa mtu mwenye maono ya muda mrefu, akieleza mipango yote ya NMG au MCL ni miaka 50 kwenda mbele, kwa hiyo alikuwa akiangalia miaka 50 mbele.

Amesema NMG imefikisha zaidi ya miaka 60 wakati MCL imefikisha miaka 22 na itafikisha 50 na zaidi.

“Taarifa za kifo chake zimenisikitisha kama binadamu mwingine yeyote. Ninawaombea waumini wa Ismailia, familia ya AKDN, wawe na subira na kumwombea heri, kikubwa ni kuyaishi yale ambayo ametujengea,” amesema.

Aliyekuwa Mhariri Mtendaji Mkuu wa MCL, Theophil Makunga amesema Mtukufu Aga Khan IV alipenda demokrasia na alikuwa akiwapa nafasi wataalamu kuendesha kampuni zake bila kuwaingilia.

Ametoa mfano kwenye vyombo vyake vya habari, kuwa aliruhusu wahariri kufanya kazi kwa uhuru, ndiyo maana kwenye sera ya habari ya NMG/MCL kuna kipengele kinachoeleza mhariri ndiyo mtu wa mwisho wa kuamua habari ichapishwe kwenye chombo cha habari.

“Kwa hali hiyo, alikuwa anataka professionals (wataalamu) waendeshe kampuni zake, kweli tulikuwa tunaziendesha professionally (kitaalamu),” amesema Makunga ambaye ni mhariri mwaasisi wa gazeti la Mwananchi.

Ameeleza kusikitishwa na taarifa za kifo cha kiongozi huyo kwa kuwa alimfahamu kama mtu aliyeamini watu wake na aliwapa nafasi ya kufanya kazi bila kuwaingilia na kuwa ndiyo maana kampuni zake zinafanya vizuri.

“Nilipopata taarifa kwamba amefariki, nilishtuka. Imenisikitisha lakini kwa sababu wote tunaelekea huko, tunamshukuru Mungu kwa kutupatia yeye,” amesema.

Alisikiliza kuliko kuongea

Francis Nanai, mkurugenzi mtendaji mwingine wa zamani MCL, amesema kiongozi huyo alikuwa ni mtu anayesikiliza zaidi kuliko kuongea, jambo lililompa nafasi ya kuelewa shida za watu na changamoto wanazopitia.

Amesema alikutana na Mtukufu Aga Khan IV mara mbili na anamtambua kama kiongozi mahiri, mwenye uwezo wa kutambua na kuchambua mambo.

Nanai amesema Aga Khan IV alikuwa anafanya uamuzi kwa jambo alilolifanyia uchambuzi mzuri.

“Alikuwa mwanadiplomasia mwenye uwezo mkubwa wa kutambua uongozi ulio madarakani na vyombo vyake vyote na kuona namna ya kuishi navyo. Ndiyo maana sikumbuki lini amewahi kuwa na mgogoro katika nchi ambazo kuna biashara zake, iwe ni Kenya au Tanzania.

“Tunafahamu kuwa Jubilee Insurance ni ya kwake, Aga Khan Hospital ni ya kwake, Aga Khan University ni ya kwake, Mwananchi Communications Ltd ni ya kwake. Zote ukiangalia utendaji wake wa kazi ni mzuri na hakuna mgogoro wowote ambao tunausikia,” amesema.

Amebainisha kuwa alikuwa baba mlezi, kiongozi wa dini, mfanyabiashara mahiri na kuna vitu vingi vya kuiga kutoka kwake, ikiwemo kuwa na upendo na mshauri mzuri.

“Nakumbuka tuliwahi kukutana kwenye nyumba yake Oysterbay, akawa anatwambia katika uandishi ndiyo unaweza kuamua kuwa very objective (kuandika kwa usahihi) au kuwa mkweli sana, lakini lazima uangalie context (muktadha) ya hicho unachoandika, unaandika ili iweje? Je, ukweli wote huwa unatoka?

“Kwa hiyo, akasema katika uandishi, pamoja na kuwa unatakiwa uwe mkweli, uweke mizania. Ni muhimu pia kuangalia context (muktadha) ya hicho unachokiandikia. Mimi nilimwelewa sana ingawa si mwandishi wa habari,” amesema.

Nanai amesema ulimwengu umepoteza kiongozi mahiri, mashuhuri, baba, babu, hivyo Watanzania na ulimwengu kwa ujumla wamwombee kwa Mungu, ampokee kwake mbinguni kwani urithi aliouacha hautafutika.

Kwa upande wake, Tido Mhando, aliyewahi pia kuwa mkurugenzi mtendaji wa MCL, amekumbuka alipokutana na Mtukufu Aga Khan na kupeana mkono, akibainisha katika mila za Kihindu, kupeana naye mkono huleta baraka.

Anaeleza anajiona mwenye baraka maradufu baada ya kupata heshima hiyo mara kadhaa.

Wakati wa utumishi wake kama mkurugenzi, Tido alihudhuria tathmini ya utendaji wa biashara ya kila mwaka katika makazi ya Mtukufu Aga Khan, Ufaransa chini ya NMG.

Amesema alishangazwa na namna mtu mwenye masilahi ya kibiashara duniani, alivyochukua muda kuelewa utendaji wa MCL.

Amesema licha ya kupokea taarifa, Aga Khan alionyesha kufahamu kwa kina shughuli za kampuni hiyo na hali ya kisiasa nchini Tanzania.

Tido amesema kiongozi huyo alishangaa ulipoletwa mjadala kuwa Mwananchi ilikuwa imefungiwa, kiongozi huyo alitoa ushauri muhimu ambao ulisaidia kampuni baada ya kurejea kwake.

“Nilifurahishwa sana Mtukufu alivyokuwa anatoa haki kwa taasisi zake, bila kujali ukubwa wao au eneo. Alikuwa akikaribisha, yuko wazi kwa mazungumzo na alikuwa na nia ya kuunga mkono uandishi bora wa habari ambao aliamini ni muhimu kwa ajili ya kujenga vyombo vya habari vyenye mamlaka na kuaminika,” amesema.

Amesema ana matumaini kwamba mrithi wake ataendelea kushikilia maadili ya uandishi wa habari bora.

Mwenyekiti mstaafu wa Bodi ya MCL, Leonard Mususa amesema tasnia ya habari imekuwa na changamoto katika uendeshaji, lakini Mtukufu Aga Khan alitoa msaada mkubwa wa kifedha, mtaji wa watu na kudumisha uvumilivu kabla ya kupata faida.

“Alibeba jukumu muhimu katika kutoa wataalamu ama kwa kuwachunguza au kuwaangalia yeye mwenyewe. Ukiangalia muundo wa Bodi ya NMG, utaona watu wa kaliba ya juu sana,” amesema.

Mususa amesema kuna watu kutoka Washington Post, New York Times na Financial Times.

“Hakuwa mtu aliyetafuta mapato ya haraka ya kifedha (gawio). Katika kutekeleza mkakati wa mabadiliko ya kidijitali, lengo lake halijawa na faida. Huu ndiyo mkakati unaotekelezwa sasa baada ya kufanyiwa kazi kwa kina mwaka 2022 na ushauri wa Financial Times,” amesema.

Amesema timu inapaswa kuhakikisha mabadiliko hayo yanafanikiwa, akidokeza kuwa licha ya changamoto zilizopo katika mkakati wa vyombo vya habari, NMG Group na MCL zinaendelea vizuri.

“Kuheshimu urithi wake ni kuhakikisha msaada unatolewa katika mabadiliko ya kidijitali. Tunapaswa kuhakikisha mchakato wa mageuzi unafanikiwa,” amesema.

Related Posts