Sare ya bao 1-1 imeifanya Simba kushindwa kurejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kufikisha pointi 44, moja nyuma ya vinara Yanga yenye 45.
Simba imepata sare hiyo dhidi ya Fountain Gate katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Manyara.
Kipindi cha kwanza cha mchezo huo kilikuwa na mashambulizi ya hapa na pale ambapo Simba ilionekana kuishambulia zaidi Fountain Gate lakini kipa wa timu hiyo, John Noble alifanya kazi nzuri ya kulinda lango lake.
Hata kipindi cha pili, Noble aliendelea kufanya vizuri akilinda lango lake hali iliyowanyima nyota wa Simba kufunga bao kupitia mashambulizi ya Elie Mpanzu na Leonel Ateba.
Baada ya kosakosa nyingi, Ateba akaifungia Simba dakika ya 58 akimalizia pasi ya Ladack Chasambi.
Hiyo ni baada ya Jean Charles Ahoua kuanzisha faulo ya haraka iliyotokana na Chasambi kuchezewa vibaya, ikiwa ni kabla ya Fountain Gate hawajajipanga vizuri.
Tukio hilo liliwafanya wachezaji wa Fountain Gate kumvaa mwamuzi, Abel William wa Arusha kisha kumfuata mwamuzi msaidizi namba mbili, Maria Mwakitalima kutoka Mbeya.
Kuingia kwa bao hilo, iliwafanya Simba kuzidisha mashambulizi lakini hayakuwa na madhara.
Dakika ya 65, Kocha wa Fountain Gate, Robert Matano alifanya mabadiliko ya wachezaji wanne kwa wakati mmoja akiwatoa Abdallah Kulandana, Salum Kihimbwa, Edgar William na Anack Mtambi wakaingia Kassim Haruna, Frank Antoni, Hashim Omary na Elie Mokono.
Mabadiliko hayo yaliifanya Fountain kuongeza mashambulizi kwa Simba huku ikishuhudiwa dakika ya 75 Ladack Chasambi akijifunga baada ya kuurudisha mpira vibaya kwa kipa wake, Moussa Camara na kujaa wavuni.
Kocha wa Simba, Fadlu Davids kila alipoangalia saa na kuona muda unakwenda akafanya mabadiliko ya wachezaji kwa nyakati tofauti akianza kumtoa Ahoua na kuingia Debora Mavambo, baadaye akawatoa Mohamed Hussein, Ladack Chasambi na Fabrice Ngoma, wakaingia Valentino Nouma, Joshua Mutale na Steven Mukwala.
Dakika ya 90+4, mwamuzi Abel William alimuonyesha kadi ya pili ya njano kipa John Noble iliyoambatana na nyekundu baada ya kuonekana akipoteza muda.
Kutolewa kwa Noble, ilibidi Hashim Omary achukue jukumu la kukaa golini kumalizia mchezo huo na kuiweka salama timu yake ikiambulia pointi moja.
Matokeo hayo yamekuwa mazuri kwa Fountain Gate ambayo duru la kwanza ilifungwa 4-0 na Simba.
Hata hivyo, sare hiyo imewafanya Simba kutibuliwa rekodi yao ambapo awali ilikuwa imeshinda mechi zote nane za ugenini msimu huu.
Mchezo wa mapema uliochezwa Uwanja wa Sokoine, Mbeya, wenyeji Tanzania Prisons waliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mashujaa.
Bao la dakika ya 88 lililofungwa na Meshack Abraham limeihakikishia Prisons kubaki na pointi tatu.
Abraham aliingia kutokea benchi akichukua nafasi Abdulkarim Segeja ambaye amebadili mchezo huo uliochezeshwa na mwamuzi Nasorro Mwinchui kutoka Tanga na kuibuka mchezaji bora wa mechi hiyo.
Mapema dakika ya tatu Prisons walitangulia kupata bao kupitia Beno Ngassa, huku Mashujaa wakisawazisha dakika ya 28 kwa penalti ikiwekwa wavuni na Seif Karihe.
Dakika ya 32, Kipa wa Prisons, Mussa Mbisa alishindwa kuendelea na mchezo baada ya kuumia na nafasi yake kuzibwa na Sebusebu Samson ambaye alionesha uimara kwa kuokoa hatari kadhaa.
Dodoma Jiji 0-1 Pamba Jiji
Licha ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji, lakini haikutosha kuifanya Pamba Jiji kujinasua kwenye mstari wa kushuka daraja ikiendelea kusalia palepale nafasi ya 14.
Pamba Jiji inayonolewa na Kocha Fred Felix Minziro, imepata ushindi huo kupitia bao la Mathew Momanyi dakika ya 23.
Huo ni ushindi wa tatu kwa Pamba Jiji msimu huu baada ya kucheza mechi 17, imetoka sare sita na kupoteza michezo nane.
Kwa upande wa Dodoma Jiji ambayo ilikuwa ikipambana kupata ushindi, ilijikuta ikiondoka nyumbani na kichapo hicho baada ya duru la kwanza matokeo kuwa 0-0 dhidi ya Pamba Jiji.
Dodoma Jiji imesalia na pointi 16 ikiwa nafasi ya tisa kwenye msimamo.
Fountain Gate: John Noble, Abdallah Kulandana/Kassim Haruna, Salum Kihimbwa/Frank Antoni, Edgar William/Hashim Omary, Jackson Shiga, Amos Kadikilo, Sadick Said, Daniel Jolam, Anack Mtambi/Elie Mokono, Shaaban Pandu na Mudrick Abdi
Simba: Moussa Camara, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein/Valentino Nouma, Che Malone Fondoh, Abdulrazack Hamza, Yusuph Kagoma, Ladack Chasambi/Joshua Mutale, Fabrice Ngoma/Steven Mukwala, Leonel Ateba, Jean Charles Ahoua/Debora Mavambo na Elie Mpanzu.