Dodoma. Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa amewataka wananchi kuhakikisha wanazifahamu na kuzitumia anuani zao za makazi, akisisitiza kwamba zinasaidia katika kupata huduma muhimu kama afya na elimu kwa urahisi.
Silaa ameitoa kauli hiyo leo Alhamisi Februari 6, 2025 wakati akifungua maadhimisho ya wiki ya anuani za makazi jijini Dodoma.
Silaa amesema kuwa asilimia 95 ya nchi imeingizwa kwenye mfumo wa postkodi, na kuwa utekelezaji wa mpango wa kutambua anuani za makazi ulifanyika kwa mafanikio, ambapo zaidi ya taarifa milioni 12.3 zilikusanywa na kuhifadhiwa kwenye mfumo wa kidijitali wa anuani za makazi, NaPA, hadi Mei 31, 2022.
Amesisitiza kwamba wananchi wanapaswa kutumia anuani hizi kujitambulisha na kumaliza changamoto za utambuzi wa maeneo na kwa yeyote atakayekutana na changamoto anapaswa kufika kwa viongozi wa mitaa, vijiji, au shehia.
Waziri Silaa ameelezea umuhimu wa anwani za makazi kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii, akifafanua kuwa mfumo huu unarahisisha utoaji wa huduma za kijamii na za biashara.
Amesema kuwa anuani hizi zimeanza kutumika na taasisi na wananchi wengine, na manufaa yake yanaonekana kwenye utoaji wa huduma za kijamii.
“Mfumo wa anuani za makazi utaendelea kuboreshwa na kuhifadhiwa ili kuhakikisha huduma zote zinapatikana kwa urahisi,” amesema.
Kwa upande mwingine, Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Festo Dugange, amesema wizara yake imeshaanza kutumia mfumo wa anuani za makazi kwa mitaa yote nchini, na hivyo kuboresha utambuzi wa maeneo.
Amesema kuwa anuani za makazi zimesaidia kutoa huduma katika sekta za afya na elimu kwa kufika kwa urahisi kwa walengwa.
Kwa upande wake mkazi wa Kilimani, Dodoma, Jenipha Japhet ambaye ni mmoja wa washiriki wa maonyesho, amesema alijua kidogo kuhusu anwani za makazi, lakini kupitia maonyesho haya, amejua umuhimu wa kutumia mfumo huu katika jamii.