Dar es Salaam. Januari 23, 2024, Baraza la Mitinani la Tanzania (Necta) lilitangaza matokeo ya kidato cha nne yaliyoonyesha shule 110 zilifaulu kwa kupata umahiri wa daraja A.
Kati ya shule 5,563 zilizoorodheshwa, zaidi ya nusu (asilimia 55) zilikuwa na umahiri wa daraja D. Hata hivyo, idadi hiyo ni ndogo ikilinganishwa na asilimia 62 za shule zilizokuwa na wastani huo mwaka 2023.
Ndani ya matokeo hayo shule 11 zilikuwa na wastani wa daraja F ikiwa ni ongezeko, ikilinganishwa na tisa zilizokuwa na wastani huo mwaka 2023.
Kwa mujibu wa Necta, shule hizo 11 zilikuwa na GPA ya 4.6171 hadi 4.8753. Wanafunzi wengi katika shule hizo wana ufaulu wa daraja la nne au sifuri.
Katika shule hizo zilizokuwa na wanafunzi 632, takribani theluthi mbili walipata daraja sifuri, 199 walipata daraja la nne na 16 pekee walipata daraja la tatu. Hakuna aliyepata daraja la kwanza wala la pili.
Uchambuzi wa Mwananchi umebaini shule tatu kati ya 11 zilizofanya vibaya zaidi ni za Mkoa wa Dar es Salaam ambazo ni Kiwalani, Sunni Jamaat na Lua zilizopo wilayani Ilala.
Mkoa mwingine wenye shule zaidi ya moja kwenye orodha hiyo ni Ruvuma ambazo ni Ukata na Kizigila.
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini ushiriki wa wanafunzi kwenye ngoma, kukopa na kuweka fedha (Vicoba), simulizi za tamthilia shuleni na ukosefu wa uzio ni miongoni mwa mambo yaliyochochea wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kiwalani kufanya vibaya katika mtihani huo.
Mbali ya hayo, imebainika wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari Lua baadhi hawakuwa na ufaulu wa kuridhisha.
Katika shule hizo mbili, wazazi wanaelezwa hawakushirikiana na walimu kufuatilia maendeleo ya watoto shuleni.
Shule ya Sekondari Kiwalani kwa matokeo yaliyotangazwa na Necta, kati ya wanafunzi 194, waliopata daraja la nne ni 56, daraja la tatu (wawili) na sifuri (136).
Shule ipo katikati ya makazi ya watu ikiwa imezungushwa uzio wa mabati chakavu. Pia ina geti. Ni shule changa, wahitimu hao ni wa kwanza wa kidato cha nne.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Yombo, Kata ya Kiwalani, Muslim Dada amelieleza Mwananchi kuwa tatizo lililopo shuleni hapo ni wazazi kuwatelekeza wanafunzi kwa walimu.
“Unampa mwanafunzi madaftari na sare nzuri, swali unafuatilia maendeleo yake akiwa shuleni na nyumbani? Madaftari yake unayakagua? Kwa uchunguzi tulioufanya hapa Yombo ni vigumu wazazi kufuatilia maendeleo ya watoto wao, hili linachangia elimu kushuka,” amesema.
Amesema katika kata hiyo walimu hawana makosa na kama yapo ni machache yanayochangiwa na wazazi.
Amesema walimu wanapoitisha vikao vya wazazi ni wachache wanaohudhuria kutokana na mwamko mdogo wa elimu uliopo.
Mkazi wa Yombo aliyeomba kutotajwa jina amesema: “Wazazi wengi ni vijana ambao suala la malezi kwao ni changamoto. Jamii yetu hapa Kiwalani wengi ni watu wa Pwani wanapenda ngoma na shughuli, suala la kununua vijora kwao ni lazima na wanasasambua hadharani. Unakuta watoto nao wanashiriki ngoma hizo nao wamevaa sare, sasa huyo atasoma?” anahoji.
Anasema mzazi anayevua nguo hadharani na kucheza ngoma hawezi kumfundisha mtoto tabia njema.
Kuhusu watoto wa kiume, anasema wapo wanaoshinda kwenye runinga kuanzia asubuhi hadi mchana, wengine wakishiriki vitendo vya wizi huku wazazi wao wakiwakingia kifua.
Anasema wapo wanafunzi ambao kila filamu mpya inapotoka wanahakikisha wanaiangalia na wawapo shuleni badala ya kusoma hufanya kazi ya kuwasimulia wenzao, hivyo kuathiri uwezo wao darasani.
Anasema wapo baadhi ya wanafunzi wanaoshiriki michezo ya kuweka na kukopeshana fedha.
“Fedha wanazitumia kununua vijora (nguo), pia kwenye sherehe za kuzaliwa ambazo kwa baadhi wanakodi maeneo yakiwamo ya baa,” anasema.
Anaeleza wahitimu wa sasa walianzia kidato cha kwanza kwenye kituo cha Binti Musa (sehemu ya madrasa) kwa miezi sita na walikuwa wakisoma mchana kusubiri ratiba rasmi ya shule.
Anaeleza kwa miezi sita wanafunzi hao waliingia darasani mchana pekee, hivyo vipindi vingi muhimu walivikosa wakiwa kidato cha kwanza.
Zuwena Rashid, mkazi wa Yombo anasema shule hiyo haina uzio, jambo linalowafanya wanafunzi watoro kupata mwanya wa kuondoka na kutorudi wakati wa masomo.
“Ukiangalia sababu ya wanafunzi wengi kuanguka katika masomo imechangiwa na uzio. Pia mwaka huu tunataraji kupokea walimu wengi kwa sababu tunao wachache,” anasema.
Amesema kuna walimu 13 lakini wanafunzi ni takribani 2,000, hivyo uwezo wa walimu kutoa ujuzi kwa weledi ni mdogo kutokana na kuhudumia wanafunzi wengi.
Imamu wa msikiti jirani na sekondari ya Kiwalani aliyejitambulisha kwa jina moja la Abdallah anasema kuna changamoto la miundombinu ambayo si rafiki shuleni hapo.
“Watoto ni watukutu, imekuwa ni vigumu walimu kuwadhibiti wanafunzi wawepo eneo la shule muda wote, zipo mbao na mabati ambayo yamefungwa na walimu kama uzio kuzuia wanafunzi kutoroka lakini hayasaidii,” anasema.
Anasema wahitimu wa kidato cha nne walianza masomo wakiwa chaguo la pili, hivyo uwezo wao darasani ulikuwa mdogo.
“Walimu walikuwa na kazi kubwa ya kuwatengeneza kutokana na utukutu wao, tulitarajia matokeo yangekuwa mabaya. Siyo tu walimu walipata shida kwa wanafunzi wale, hata sisi majirani tulipata shida,” amesema.
Anasema pia idadi ya walimu ni ndogo, wengi wakiwa wa kujitolea.
Kiongozi huyo wa dini anasema wazazi walivutana kuhusu mchango wa chakula shuleni, hivyo vikao vingi vilijadili suala hilo badala ya maendeleo ya wanafunzi.
Ofisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Mussa Ally amesema baada ya matokeo ya kidato cha nne, waliitisha kikao cha kila darasa katika Shule ya Sekondari Kiwalani.
“Pia tunakwenda kuongeza idadi ya walimu, kwa sasa wapo 29 na wengine 12 wa kujitolea, tutaongeza wengine sita,” amesema.
Amesema wamejikita kuiboresha shule hiyo kwa awamu.
“Tumetenga Sh500 milioni kwa ajili ya ujenzi wa jengo jipya la ghorofa shuleni hapo, ambalo litabeba miundombinu yote iliyopungua. Tayari tumebadili ofisa elimu kata na kumpeleka mwingine atakayeshirikiana na walimu na wazazi kuboresha taaluma ya wanafunzi,” amesema.
Shule ya Sekondari Lua iliyopo Gongo la Mboto katika matokeo ya Necta ya kidato cha nne, kati ya wanafunzi 12 waliohitimu, wanane walipata daraja sifuri, wanne daraja la nne.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Ulongoni A, Kata ya Gongo la Mboto, Abdurahim Munisi amesema mtaa huo wenye shule za sekondari Ulongoni A na Lu,a baadhi ya wanafunzi hujihusisha na vitendo vya ngono na uvutaji wa bangi.
“Walimu wanafanya jitihada kubwa lakini watoto ni changamoto. Sekondari ya Lua wanafunzi walikuwa wachache lakini walichaguliwa kujiunga wakiwa na ufaulu mdogo,” amesema.
Petro Silvanus, mkuu wa shule msaidizi anasema ufaulu umeshuka zaidi.
“Mwaka jana tulifaulisha vizuri, mwaka huu baada ya matokeo kuonekana mabaya tuliweka mkakati wa kuwabakisha wanafunzi shuleni wasome kwa kuwapa maswali kabla ya kwenda nyumbani na kila mwezi tunakuwa na mitihani na majadiliano,” amesema.
Anakiri kwamba baadhi ya waliohitimu walipochaguliwa kujiunga na sekondari ufaulu wao wa darasa la saba ulikuwa chini.
Anasema shule hiyo ina wanafunzi wachache kwani inamilikiwa na mtu binafsi. Anasema kwa sasa kidato cha nne kuna wanafunzi wanne, kidato cha tatu wapo sita, cha pili wawili na bado hawajapata wa kidato cha kwanza.
Silvanus anasema kutokana na uwezo mdogo wa wanafunzi walimu hutumia nguvu nyingi zaidi kumsaidia mwanafunzi kufaulu, lakini kama mzazi hamsaidii mwanaye ni kazi bure.
“Tunamuita mzazi anakuja, umamuuliza kuhusu usomaji wa mwanaye anakwambia hajawahi kumuona akishika daftari kujisomea, kazi ni kuangalia runinga, mzazi mwenyewe hajipi jukumu la kumfuatilia mtoto.
“Ukiangalia wakazi wengi wa Dar es Salaam hawatengenezi mazingira mazuri kwa ajili ya mwanafunzi kujisomea, sebuleni wanaangalia runinga, mtoto anasoma papo hapo kama anaingia chumbani ni kulala tu,” amesema.
Shule nyingine zilizokuwa na wastani wa daraja F ni Kibogwa iliyopo Morogoro ambayo wanafunzi 20 kati ya 23 walipata daraja sifuri na wengine wakipata daraja la nne.
Shule ya Viziwi Njombe wanafunzi 20 kati ya 24 walipata daraja sifuri, Mtumachi ya Mtwara wanafunzi 38 kati ya 56 walipata sifuri, wakati shule za Ukata na Litumbandyosi za Ruvuma wanafunzi 15 kati ya 22 na wengine 27 kati ya 41 walipata sifuri katika shule hizi, mtawalia.
Shule nyingine ni Ndalichako ya mkoani Kigoma ambayo zaidi ya nusu ya wanafunzi 68 walipata sifuri.
Litumbandyosi na Viziwi Njombe pia zilikuwa miongoni mwa shule tisa zilizopata wastani wa daraja F mwaka 2023.