Farida Mangube, Morogoro
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Bw. Mussa Ali Mussa, amewataka watafiti kuchapisha tafiti zao kwa Kiswahili ili kuhakikisha matokeo ya utafiti yanafika kwa jamii inayolengwa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa utafiti wa magonjwa yanayo ambukizwa kutoka Kwa wanyama kwenda kwa binaadamu unaotekelezwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA), Mussa alisema kuwa tafiti nyingi zimekuwa zikifanywa kwa lugha za kigeni, hali inayowafanya wafugaji na jamii kwa ujumla kushindwa kunufaika na matokeo ya utafiti huo.
“Serikali inatumia pesa nyingi kufadhili tafiti hizi, lakini iwapo matokeo hayafiki kwa jamii kwa lugha inayoeleweka, basi jitihada hizi zinapotea bure,” alisema Mussa.
Katika hotuba yake, alisisitiza umuhimu wa kushirikisha watunga sera wakati wa kufanya tafiti ili kuhakikisha matokeo yake yanatumika kutengeneza miongozo na sheria zitakazosaidia jamii.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi huo kutoka SUA Prof. Esron Karimuribo, alisema kuwa mradi huu unatekelezwa katika Halmashauri tisa za Mkoa wa Morogoro kwa lengo la kudhibiti na kuzuia magonjwa yanayoathiri wanyama na binadamu, ambayo yanasababisha vifo na kupunguza pato la jamii.
“Magonjwa haya yanapoenea huathiri sio tu mifugo, bali pia binaadamu, hivyo kushusha uchumi wa wafugaji na jamii kwa ujumla,” alisema Prof. Karimuribo
Kwa upande wao baadhi ya Wafugaji Mkoa wa Morogoro wameelezwa kuwa ugonjwa wa kifua kikuu (TB) unaotokana na ng’ombe ni tatizo linaloenea kwa kasi, hasa kutokana na uhamaji wa mifugo.
Dkt. Kohei Makita ni Mratibu wa mradi wa utafiti wa magonjwa yanayoambukizwa na kutoka Kwa wanyama kwenda kwa binaadamu kutoka ( JICA) alisema kuwa tafiti kuhusu TB katika mifugo zilianza kufanyika Tanzania tangu mwaka 2008, lakini bado kuna changamoto kubwa ya uelewa kwa wafugaji.
“Wafugaji wengi hawaamini kuwa TB inaweza kutoka kwa ng’ombe na kumuambukiza binadamu, hali inayofanya usambazaji wa ugonjwa huu kuwa mkubwa,” alisema Dkt. Kohei
Bw. Kochocho Mgema mmoja wa wafugaji kutoka Morogoro alikiri kuwa wamekuwa wakikumbana na ugonjwa wa TB mara kwa mara, lakini wengi wao hawaelewi chanzo chake.
Kupitia mradi huu, wataalamu wanapendekeza mikakati madhubuti ya kudhibiti magonjwa yanayotoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wafugaji, udhibiti wa uhamaji wa mifugo, na uimarishaji wa huduma za afya ya mifugo.
Serikali, kwa kushirikiana na SUA na JICA, inatarajia kuwa mradi huu utasaidia si tu kutatua magonjwa ya mifugo, bali pia kuchochea ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Morogoro kupitia sekta ya mifugo.