Rombo. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amewataka vijana nchini waliobahatika kuwa na wazazi walio hai kujenga utamaduni wa kuwatunza, kuwalea na kuwaonyesha upendo.
Amesema mzazi (mama) ni mtu muhimu kwa kuwa ndiye wakili wa Mwenyezi Mungu hapa duniani.
Hayo ameyasema leo, Februari 6, 2025 wakati wa ibada ya misa ya mazishi ya mama mzazi wa Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, mama Sekunda Massawe (82) iliyofanyika Kanisa la Mtakatifu Pius wa X, Parokia ya Tarakea, wilaya ya Rombo, Mkoani Kilimanjaro.
Mama Sekunda, ambaye alifariki Januari 30, mwaka huu akisumbuliwa na ugonjwa wa saratani, amezikwa katika makaburi ya familia yaliyopo katika Kijiji cha Mbomai Juu, Kata ya Tarakea Motamburu, wilayani hapa.
Hata hivyo, Viongozi mbalimbali wa Serikali na chama, wakiwemo mawaziri, wabunge wa Mkoa wa Kilimanjaro na baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya wameshiriki maziko hayo.
Ibada hiyo ya mazishi imeongozwa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi, Askofu Ludovick Minde akiongozana na mapadre zaidi ya 40 wa Jimbo hilo.
Akizungumza wakati akitoa salamu za Serikali, Dk Mpango amesema vijana wanao wajibu mkubwa wa kuwalea na kuwatunza wazazi wao wangali hai hapa duniani.
“Nitumie nafasi hii kuwasihi Watanzania wote, Wanarombo wote ambao mmebahatika kuwa na wazazi waliohai muwatunze kwa upendo na kwa bidii zote kwa maana mama ndio wakili wa Mwenyezi Mungu hapa duniani.
“Sisi kwa upande wa Serikali tunamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa maisha ya mama huyu ambaye alituzalia Profesa Mkenda, Waziri wetu wa Elimu ambaye amekuwa kiongozi na mtendaji mahiri sana katika utumishi wa umma tangu alipokuwa akifundisha Chuo Kikuu Dar es salaam na katika nafasi mbalimbali alizoshika serikalini,” ,” amasema Dk Mpango.
Amesema kifo cha mama Mkenda ni pigo kwa familia lakini akiishukuru familia hiyo kwa kuwalea watoto katika malezi bora na kwamba mama huyo amewaachia matunda bora.
“Tunaendelea kufaidi matunda ya mama, tunaomba sasa wazazi wote tujifunze kutoka kwa mama huyu ambaye sasa amerudi kwa muumba wake,” amesema Dk Mpango.
Pamoja na mambo mengine amewataka wazazi kuwasomesha watoto wao kwa kuwa ndio hazina ya baadaye pindi watakapozeeka.
“Wazazi tufanye jitihada za kusomesha watoto, kuwafundisha maadili mema kushika dini yao kiadilifu, na kufanya kazi kwa bidii kwa faida yetu wote,” amasema Dk Mpango.
Akitoa mahubiri katika mazishi hayo, Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi, Askofu Ludovick Minde ameitaka jamii kuendelea kutenda matendo mema na kuacha historia nzuri katika jamii.
“Watoto wa marehemu pamoja na wajukuu endeleeni kumuenzi mama yenu na kuishi yale mazuri aliyoyaacha na kuyaishi mafundisho aliyowafundisha, ili kuendelea kumuenzi,” amesema Askofu Minde.
Akisoma historia ya marehemu mtoto wa marehemu, Ulirk Mkenda amesema kifo cha mama yao ni pigo kwa familia kwa kuwa alikuwa ni kiungo muhimu cha familia.
“Mama yetu alikuwa mtu wa watu, mwenye imani ya kumcha Mungu, mwenye upendo na kila mtu, hakika tumempoteza mtu muhimu na tegemo katika familia,” amesema Mkenda.
Amesema watamkumbuka mama Sekunda kwa ukarimu wake mzuri aliokuwa nao, uchapakazi wake.
Naye, Profesa Adolf Mkenda ameishukuru Serikali na wadau wengine waliojitokeza kushiriki katika maziko ya mama yake.
“Nashukuru kanisa mmetulea na kwa kweli mmemlea mama, alikuwa mtu wa dini na ametulea vyema, nitoa shukran sana kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa maneno ya faraja kutoka kwake na Dk mpango kwa kutukimbilia na kutufarij,” amesema Profesa Mkenda.