Wataalamu wafunguka ishu ya kadi Fountain gate vs Simba

KOCHA Fadlu Davids ameshindwa kuifikia rekodi ya Patrick Aussems ya kushinda mechi 11 mfululizo za Ligi Kuu baada ya jioni ya jana kulazimishwa sare ya 1-1 na Fountain Gate iliyomaliza pungufu baada ya kipa John Noble kutolewa kwa kadi nyekundu na mwamuzi Abel William kutoka Arusha.

Fadlu aliyetua Msimbazi msimu huu aliiongoza Simba kushinda mechi 10 mfululizo tangu timu hiyo ilipofungwa bao 1-0 na Yanga katika Dabi ya Kariakoo na sare hiyo imemtibulia kuifikia rekodi ya Aussems aliyoiweka msimu 2018-2019 alipoiongoza kushinda mechi 11 mfululizo.

Sare hiyo ni ya kwanza kwa Simba katika mechi za ugenini kwani ilishacheza mechi nane mfululizo bila kupoteza wala kutoka sare yoyote zaidi ya kushinda zote, lakini ni ya pili kwa msimu huu ikiwaacha nafasi ya pili nyuma ya Yanga inayoongoza kwa pointi 45, wakati Wekundu wakiwa na 44. Kila timu imecheza mechi 17 hadi sasa.

Simba imepata sare hiyo kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Babati, Manyara licha ya wenyeji kumpoteza kipa aliyekuwa kikwazo kwa mashambulizi mechi ya Simba pale alipolimwa kadi ya pili ya njano iliyosindikizwa na nyekundu kwa kupoteza muda baada ya awali kuonyeshwa njano ya kwanza kipindi cha kwanza kwa kosa hilo hilo.

Kabla ya kutolewa katika kipindi cha pili, Noble aliendelea kufanya vizuri akilinda lango lake hali iliyowanyima nyota wa Simba kufunga bao kupitia mashambulizi ya Elie Mpanzu na Leonel Ateba na wengineo.

Baada ya kosakosa nyingi, Ateba akaifungia Simba katika dakika ya 58 akimalizia pasi ya Ladack Chasambi, likiwa ni bao lake la nane katika Ligi Kuu msimu huu akimfikia Elvis Rupia wa Singida Big Stars katika nafasi ya pili ya chati ya vinara wa mabao, wakizidiwa na Clement Mzize wa Yanga pekee aliye na mabao tisa.

Ateba alifunga bao hilo baada ya Jean Charles Ahoua kuanzisha kwa haraka mpira wa frii-kiki ya nje kidogo ya boksi iliyotokana na Chasambi kuchezewa vibaya.

Tukio hilo liliwafanya wachezaji wa Fountain Gate kumvaa mwamuzi, Abel William wa Arusha kisha kumfuata mwamuzi msaidizi namba mbili, Maria Mwakitalima kutoka Mbeya.

Kuingia kwa bao hilo, kuliwafanya Simba kuzidisha mashambulizi lakini hayakuwa na madhara.

Dakika ya 65, kocha wa Fountain Gate, Robert Matano alifanya mabadiliko ya wachezaji wanne kwa wakati mmoja akiwatoa Abdallah Kulandana, Salum Kihimbwa, Edgar William na Anack Mtambi wakaingia Kassim Haruna, Frank Antoni, Hashim Omary na Elie Mokono. 

Mabadiliko hayo yaliifanya Fountain kuongeza mashambulizi kwa Simba huku ikishuhudiwa dakika ya 75 Ladack Chasambi akijifunga baada ya kuurudisha mpira vibaya kwa kipa wake, Moussa Camara na kujaa wavuni.

Kocha wa Simba, Fadlu Davids kila alipoangalia saa na kuona muda unakwenda akafanya mabadiliko ya wachezaji kwa nyakati tofauti akianza kumtoa Ahoua na kuingia Debora Mavambo, baadaye akawatoa Mohamed Hussein, Ladack Chasambi na Fabrice Ngoma, wakaingia Valentino Nouma, Joshua Mutale na Steven Mukwala.

Dakika ya 90+4, mwamuzi Abel William alimuonyesha kadi ya pili ya njano kipa John Noble iliyoambatana na nyekundu baada ya kuonekana akipoteza muda, huku staili ya mwamuzi huyo kunyanyua juu kwa pamoja kadi zote mbili — moja kila mkono, ikiacha gumzo.

Kutolewa kwa Noble, ilibidi mchezaji wa ndani Hashim Omary achukue jukumu la kusimama golini ambapo alidaka hatari moja kubwa ya shuti na kuiwezesha timu hiyo kupata pointi moja katika mchezo huo ambao dakika tisa ziliongezwa zilipomalizika 90 na baada ya mpira kusimama katika tukio la kadi nyekundu mpira ukachezwa kwa jumla ya dakika 14 za nyongeza za majeruhi.

Matokeo hayo yamekuwa mazuri kwa Fountain Gate ambayo duru la kwanza ilifungwa 4-0 na Simba.

Hata hivyo, sare hiyo imewafanya Simba kutibuliwa rekodi yao ambapo awali ilikuwa imeshinda mechi zote nane za ugenini msimu huu.

Refa wa zamani, Osmani Kazi ametoa ufafanuzi kuhusu kitendo cha mwamuzi Abel William kuinua juu kadi mbili kwa wakati mmoja, akisema ni tulio ambalo halina makosa yoyote.

“Hamna shida yoyote kufanya vile,” alisema Kazi na kuongeza: “Ingawa inakuwa vizuri mwamuzi akitanguliza kadi ya pili ya njano na kisha kutoa nyekundu.”

FOUNTAIN GATE: John Noble, Abdallah Kulandana/Kassim Haruna, Salum Kihimbwa/Frank Antoni, Edgar William/Hashim Omary, Jackson Shiga, Amos Kadikilo, Sadick Said, Daniel Jolam, Anack Mtambi/Elie Mokono, Shaaban Pandu na Mudrick Abdi

SIMBA: Moussa Camara, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein/Valentino Nouma, Che Malone Fondoh, Abdulrazack Hamza, Yusuph Kagoma, Ladack Chasambi/Joshua Mutale, Fabrice Ngoma/Steven Mukwala, Leonel Ateba, Jean Charles Ahoua/Debora Mavambo na Elie Mpanzu.

Related Posts