Trump aja na mpya, aahidi kubadili Gaza kuwa bustani ya Paradiso

Kauli ya Rais Donald Trump wa Marekani ya kuchukua eneo la Gaza na kuibadilisha kutoka magofu kuwa bustani ya Paradiso imetajwa kuzua hofu ya kuongeza joto la mgogoro kati ya Palestina na Israel.

Kauli za Trump kuhusu suala hilo, ikiwemo kupeleka wanajeshi ikiwa italazimu, zimezua mjadala miongoni mwa wabunge na wachambuzi, wakihofia kwamba zinaweza kuitumbukiza nchi katika jukumu gumu la kuwa mamlaka inayokalia eneo hilo kwa mabavu, katikati ya mzozo mgumu kutatuliwa.

Trump aliyasema hayo Februari 4, 2025 katika Ikulu ya White House alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari akiwa na Waziri Mkuu wa Israel.

Trump alivyouelezea, mpango huo ungehusisha ujenzi mkubwa wa miundombinu na fursa za ajira.

“Sitaki kuonekana mjuaji, lakini Riviera ya Mashariki ya Kati… hili linaweza kuwa jambo la ajabu sana,” alisema Trump akisindikizwa na Benjamin Netanyahu.

Licha ya kwamba mapendekezo ya Trump yanaweza yasitekelezwe lakini yana athari kubwa kwa mujibu wa BBC.

Hiyo ni kutokana na Trump kuwa mtu mwenye ushawishi mkubwa duniani.

“Pendekezo lake linaweza kuathiri makubaliano ya kusitisha vita nchini Gaza ambayo yalikuwa yameanza.

“Kutokuwa na mkakati wa mustakabali wa uhuru wa Gaza tayari umeingiza kiwewe ndani ya makubaliano ya kusitisha vita vya Gaza,” imeeleza BBC.

Kauli hiyo imetajwa kuimarisha mikakati kwa upande unaoamini ardhi yote kati ya Bahari ya Mediterranean na Mto Jordan, ni mali waliobinafsishwa na Mungu.

Viongozi walio na msimamo kama huu ni miongoni mwa wajumbe wa Serikali ya Netanyahu na wanaompa mamlaka zaidi na wanafurahia hilo.

Wanapendelea vita vya Gaza virejee vikilenga kuwaondoa Wapalestina na kutoa fursa kudhibiti walowezi.

Waziri wa Fedha, Bezalel Smotrich amesema wazo la Rais Trump limeeleza wazi mustakabali wa Gaza baada ya mashambulizi ya Oktoba 7, 2024.

“Aliyejaribu kuvamia Israel inamaana atajikuta amepoteza ardhi yake milele. Hili linatupa fursa ya kuzika wazo la kuipa uhuru Palestina,” imenukuliwa na BBC.

Upande wa upinzani ambao wako katika Serikali ya Israel hawajaoneka kutoa msimamo wakiogopa kukemewa japo kwa kusita wamekaribisha wazo hilo la Trump.

Hamas na baadhi ya vikundi vilivyo na silaha vya Palestina wanatarajiwa kujibu kauli ya Trump kwa mpigo na labda kuishambulia Israel.

Kwa upande wa Palestina, mzozo kati yao na Israel unajikita katika mzizi ya kumbukumbu ya wanachokiita al- Nakba, kama janga.

Huo ulikuwa uhamisho wa Palestina huku Walowezi wakishinda vita vya kupigania uhuru mwaka 1948.

Zaidi ya Wapalestina 700,000 walitoroka au walilazimishwa kutoka makazi yao na Walowezi.

Wengi wao ambao waliruhusiwa kurejea walilazimika kufuata sheria za Israel zilizoidhinishwa ambazo wanazitumia kuwapokonya mali yao.

Sasa uoga unaowaingia raia wa Palestina ni kuwa jambo kama hilo huenda likatokea tena.

Palestina wanaamini Israel ina njama ya kutumia vita hivi na Hamas kuharibu Gaza na kufuta kizazi cha Palestina.

Ni kati ya wanachodai kuwa Israel inatekeleza mauaji ya kimbari na sasa wanaeza anza kuamini kuwa Donald Trump anagongelea msumari njama hizo za Israel.

Related Posts