Vyama vyatakiwa kuweka mkakati wa nishati safi, mabadiliko ya tabianchi

Dar es Salaam. Wadau wa nishati nchini wamependekeza vyama vya siasa vieleze katika ilani zao za uchaguzi mkakati wa kuwezesha nishati safi na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Wametaka vyama hivyo viweke wazi nini vitafanya kuhakikisha nishati jadidifu inawafikia wananchi wa ngazi zote na namna watakavyopambana na mabadiliko ya tabianchi watakaposhika dola.

Pia, wametaka viweke mapendekezo ya namna nishati jadidifu itakavyoleta maendeleo katika sekta za uvuvi, maji, kilimo, mifugo, na afya yamewasilishwa na wadau hao.

Hayo yameelezwa jana Alhamisi, Februari 6, 2025 na Katibu Mradi wa Shirika la Can Tanzania, Fadhili Shahidi, wakati wa majadiliano na wadau wa nishati jadidifu jijini Dar es Salaam.

Amesema ripoti ya taasisi hiyo iliyotokana na utafiti, imebaini kuwa matumizi ya nishati jadidifu katika sekta hizo hupunguza gharama za maisha kwa asilimia 60 hadi 80.

“Ripoti hii imechunguza jinsi matumizi ya sera katika sekta hizi yanavyoweza kuhusisha matumizi ya nishati katika mipango yake, na kuwa sera inavyosema ndivyo itakavyotekelezwa ili kusaidia jamii na kuleta maendeleo chanya,” ameongeza.

Amesema kuwa ripoti hiyo, iliyofanywa kwa kushirikiana na mashirika na wadau wa nishati, imetoa mapendekezo kuhusu matumizi ya sera.

“Tumependekeza matumizi ya sera katika sekta tulizozitaja na kutoa elimu ili kuwawezesha wadau wa taasisi binafsi kuwafikia na kutoa misaada katika maeneo mbalimbali,” amesema.

Shahidi amesema kuwa kipindi hiki cha kuandaa Dira ya Taifa ya miaka 25, uchaguzi wa viongozi na mkakati wa National Energy Compact ni fursa muhimu ya kupanga maendeleo ya nchi kwa miaka ijayo.

Mdau wa nishati jadidifu, Brenda Kasmiri, amesema kuelekea uchaguzi mkuu, kuna vipengele vinavyopaswa kuingizwa kwenye sera za vyama vya siasa.

“Kuna baadhi ya sera zinapaswa kuingizwa kwenye ilani za vyama ili ziweze kutengewa fedha za utekelezaji,” amesema.

Ameeleza kuwa Wizara ya Nishati haina msimamizi wa nishati jadidifu katika ngazi za halmashauri.

“Wizara zote zinatumia nishati na baadhi yao hutumia jenereta, ambazo ni gharama kubwa. Ni vyema matumizi ya umeme wa upepo na jua yakatiliwa mkazo ili kupunguza gharama kwa serikali,” amesema.

Brenda amesisitiza kuwa ni muhimu nishati jadidifu ifike vijijini ili kuwasaidia wafugaji na wakulima.

“Uwepo wa nishati jadidifu vijijini utawasaidia wakulima kuwa na majokofu ya kutunza maziwa na mboga mboga kwa gharama nafuu,” amesema.

Aidha, mwakilishi kutoka Wizara ya Nishati, Emilian Nyanda amesema halmashauri nyingi hazina mipango mahususi ya kutekeleza ajenda za nishati jadidifu.

“Tutahakikisha fedha zinatengwa ili kutekeleza ajenda za nishati safi,” amesema.

Nyanda ameongeza kuwa matumizi ya umeme yameongezeka kutokana na shughuli za kijamii.

“Upatikanaji wa nishati ni lazima uwepo ili kukidhi mahitaji ya kijamii,” amesema.

Amehitimisha kwa kusema kuwa kupitia sera za vyama, utekelezaji wa nishati jadidifu utaweza kufanyika kwa ufanisi, na uwepo wa sera hizo kutachochea matumizi yake nchini.

Related Posts