Muda mfupi baada ya Yanga kuwasili katika Uwanja wa Mkapa, wamelazimika kugomea kuingia kwenye chumba cha kubadilishia nguo.
Maofisa wa Yanga waliotangulia kukagua chumba hicho walionekana kutoridhishwa na mandhari waliyoyakuta ambapo walionekana kulalamika kuna hewa nzito na kuumia macho wakidai kutokwa machozi.
Kutokana na ishu hiyo, wahusika wakuu wa mchezo huo akiwemo Mratibu Mkuu, Herieth Gilla, walifika kujadiliana jambo na maofisa wa Yanga, mwisho wa siku wakapatiwa eneo lingine la kukaa ambalo ni kwenye korido pembeni.
Hayo yamejiri wakati Yanga ikiwa ni mwenyeji wa mchezo wa Kariakoo Dabi dhidi ya Simba unaotarajiwa kuchezwa kuanza saa 11:00 jioni.
Kariakoo Dabi mara nyingi imekuwa na matukio mengi ya kabla na baada ya mchezo kitu ambacho kinazidi kuufanya mchezo huo kuwa wa kipekee kulinganisha na michezo mingine.