Ahukumiwa miaka minne kwa mauaji ugomvi wa choo

Arusha. Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Bukoba imemhukumu adhabu ya kifungo cha miaka minne jela, Jacob Alphonce baada ya kumkuta na hatia ya kosa la mauaji bila kukusudia.

Mei 27,2024 Jacob alimuua Lucas Denis, katika eneo la Nyamiaga wilayani Ngara Mkoa wa Kagera.

Ilidaiwa na upande wa mashitaka kuwa siku ya tukio, mke wa Jacob, Salima Selemani alimtaka Lucas kubomoa choo chao na kukijenga upya katika eneo lingine kwa sababu eneo ambalo choo hicho kilikuwepo liliuzwa kwa mtu mwingine ambaye alitaka eneo lake liwe tupu.

Lucas alikubali  akakibomoa choo na kuanza kujenga mpya kwa mujibu wa maelekezo aliyopewa na mke wa mtuhumiwa na jioni Lucas alipofika nyumbani kwake na kumkuta marehemu akiendelea na ujenzi huo alimuuliza kwa nini anafanya hivyo.

Ilidaiwa kuwa marehemu alimweleza mshtakiwa kuwa mke wake ndiye amemuelekeza kufanya hivyo, jambo ambalo halikumfurahisha Lucas na kusababisha ugomvi baina yao.

Ilielezwa kuwa Jacob aliokota kipande cha mti na kumpiga Jacob sehemu mbalimbali za kichwa, marehemu alipoteza fahamu na kuanguka chini huku damu zikitoka mdomoni, puani na kichwani.

Ilidaiwa mke wa marehemu ambaye alikuwa katika eneo la tukio alichukua hatua ya kumsaidia mume wake, huku akipiga kelele kuomba msaada na kwa bahati mbaya mumewe alifariki siku hiyohiyo.

Jaji Gabriel Malata, alitoa hukumu hiyo katika kesi ya jinai namba 35149 ya mwaka 2024, Februari 6, 2025 ambayo nakala yake kuwekwa kwenye tovuti ya mahakama.

Jaji huyo amesema kosa la kuua bila kukusudia ambalo anashtakiwa chini yake linaweza kuadhibiwa kwa kifungo cha juu ambacho ni kunyongwa hadi kufa lakini mahakama ina hiari ya kuweka adhabu ndogo kulingana na mazingira ya kesi.

Ilidaiwa baada ya tukio hilo kuripotiwa kwa balozi wa nyumba 10 na baadaye Kituo cha Polisi Ngara.

Jacob alikamatwa na kufikishwa kituo cha Polisi ambapo akihojiwa alikiri kusababisha kifo cha marehemu na kufunguliwa kosa la mauaji bila kukusudia kinyume na kifungu cha 195 na 198 cha Kanuni ya Adhabu.

Februari 4, 2025 pande zote za kesi hiyo zilifikishwa mahakamani kwa ajili ya usikilizwaji wa wali ambapo upande wa Jamhuri uliwakilishwa na Wakili Matilda Assey huku mshitakiwa akiwakilishwa na Wakili Dastan Mutagahaywa.

Baada ya Jacob kusomewa shitaka hilo, alikiri kuwa alisababisha kifo cha Lucs bila kukusudia, Mahakama ilimtia hatiani Jacob kwa kosa la mauaji kinyume na kifungu cha 195 na 198 cha Kanuni ya Adhabu.

“Mahakama hii, baada ya kuchukua mazingira yote, inaona kuwa, mshitakiwa alimfanyia unyama marehemu aliyepewa mkataba na mke wa mshtakiwa wa kubomoa na kujenga choo kingine ni dhahiri kwamba mshitakiwa alitumia kipande cha mti kilichokusanywa kwa ajili ya kujenga choo kwa kumpiga marehemu,”

“Katika tukio hilo, mahakama hii inamhukumu mshtakiwa, Jacob Alphonce kutumikia kifungo cha miaka minne jela ,”amesema.

Related Posts