Rungu la Fifa laigusa Taifa Stars

Unaweza kusema rungu la FIFA limeigusa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ baada ya kutangazwa uamuzi wa kuifungia Congo Brazzaville kutokana na kosa la serikali kuingilia uendeshaji wa Shirikisho la mpira wa miguu nchini humo (Fecofoot).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) jana Februari 6, 2025 imeeleza kuwa kusimamishwa huko kwa Congo ni kwa sababu ya serikali kuingilia michezo jambo ambalo ni kinyume na katiba ya FIFA.

“Tunakutaarifu kwamba, kwa kuzingatia uamuzi uliochukuliwa na Ofisi ya Baraza la FIFA Februari 6, 2025, FECOFOOT imesimamishwa hadi itakavyoamriwa vingine, kwa mujibu wa kifungu cha 16 cha katiba ya FIFA,”

“Hivyo kuanzia Februari 6, 2025, FECOFOOT itapoteza haki zake zote za uanachama, kama ilivyofafanuliwa katika kifungu cha 13 cha katiba ya FIFA, mara moja na hadi itakavyoamriwa vingine.

“Vile vile, timu zinazowakilisha FECOFOOT na klabu wakilishi hazitashiriki tena katika mashindano ya kimataifa hadi kusimamishwa huko kutakapoondolewa,” imebainisha taarifa hiyo ya Fifa.

Kifungo hicho kimekuja mwezi mmoja kabla ya mchezo baina ya Taifa Stars dhidi ya Congo uliopangwa kupigwa Machi 17, 2025 ambapo FIFA ni kama imelainisha mambo kwa Stars ambayo inaweza kujikuta mambo yapo vizuri.

Taifa Stars imeonyesha muelekeo mzuri katika mechi za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026 ambapo kwa sasa inashika nafasi ya tatu katika kundi E ikiwa na pointi sita ilizokusanya katika mechi tatu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya FIFA, Congo pia haitopata fursa ya kushiriki shughuli tofauti za kiutawala za FIFA hadi pale itakapoondolewa kusimamishwa huko.

“Hii pia inamaanisha kuwa FECOFOOT, wanachama na maofisa wake hawatafaidika tena na programu za maendeleo, kozi na mafunzo yanayotolewa na FIFA au CAF.

“Zaidi ya hayo, tunakukumbusha kuwa wewe na washirika wako hamruhusiwi kudumisha uhusiano wowote wa michezo na FECOFOOT na/au timu zake kwa muda wa kusimamishwa kwa shirikisho.

“Tafadhali kumbuka kuwa ofisi ya baraza la FIFA au baraza lenyewe linaweza kuondoa kusimamishwa wakati wowote kabla ya kongamano lijalo la FIFA. Kisha tutakujulisha ipasavyo,” ilifafanua barua hiyo ya FIFA.

Ikiwa Fifa itaendeleza uamuzi huo wa kuisimamisha Congo hadi Machi 17, 2025, maana yake Taifa Stars haitacheza mechi yake ya nyumbani dhidi ya Congo jambo ambalo litaipa muda wa kutosha wa kufanya maandalizi ya mchezo dhidi ya Morocco, siku saba baadaye.

Related Posts