Simanjiro. Mkazi wa Kijiji cha Okutu Wilayani Simanjiro mkoani Manyara, Melkzedek Moikani (33) amehukumiwa kwenda jela miezi sita kwa kosa la kufanya fujo na kufunga ofisi ya kijiji kwa kufuli.
Imeelezwa kuwa kitendo hicho kilizua hofu kwa wananchi waliofuata huduma katika ofisi hiyo, lakini pia kilikwamisha shughuli za maendeleo.
Hukumu hiyo imetolewa leo Jumatano Mei 15, 2024 na Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro, Evarest Mushi.
Moikani aliyekuwa mshtakiwa namba mbili katika kesi hiyo na wenzake watatu, wanadaiwa kutenda kosa hilo Januari 28, 2024 Saa 9 alasiri.
Awali, akitoa ushahidi mahakamani hapo, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Okutu, Neema Gelpeter ambaye ni mlalamikaji kwenye kesi hiyo ya jinai namba 19/2024, alidai kuwa siku ya tukio, Moikani akiwa na wenzake watatu, Said Mdachi (65), Tumburu Jembe (40) na Seuri Moikani, walifanya fujo ofisini hapo na baadaye Moikani akaamua kufunga mlango wa ofisi hiyo kwa kufuli.
“Mheshimiwa hakimu hali hii ilisababisha usumbufu mkubwa kwa sababu kazi za ofisi zilizokuwa zikiendelea, zilisimama,” amedai Gelpeter.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mushi amesema anamuhukumu Moikani kifungo cha miezi sita jela bila faini baadaya kudhibitika kuwa alitenda kosa hilo pasi na shaka.
Amesema anamuhukumu mshtakiwa kifungo hicho kwa kosa la kufanya fujo na ufunga ofisi ya kijiji kinyume na kifungu cha sheria namba 89/12 ya kanuni ya adhabu sura ya 16.
Amesema siku ya tukio, mshtakiwa alifunga mlango wa ofisi ya mwenyekiti wa kijiji hicho kwa kutumia kufuli aina ya Solex lenye rangi ya fedha.
Pia, amesema mshtakiwa siku hiyo alifunga mlango wa ofisi ya ofisa mtendaji wa kijiji cha Okutu kwa kutumia kufuli lenye rangi ya shaba hali iliyosababisha hofu kwa viongozi hao ambao pia walishindwa kutekeleza majukumu yao.
“Kulingana na ushahidi uliotolewa mahakamani hapa upande wa mashitaka umethibitisha bila kutia shaka kuwa mshtakiwa namba mbili Melkzedek Moikani amekutwa na hatia, hivyo anahukumiwa kwenda jela kifungo cha miezi sita bila faini,” amesema Hakimu Mushi.
Amesema mshtakiwa namba moja, tatu na nne, upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha mashitaka yao hivyo mahakama inawaachia huru.