Kumeanza kuchangamka! Nabi amng’oa Fadlu Simba

KABLA ya tukio la Simba kuangusha pointi moja mbele ya Fountain Gate juzi jioni, mjadala ulikuwa kitendo cha kocha wa Yanga, Saed Ramovic kuikacha timu hiyo ndani ya muda mfupi na kuibukia CR Belouizdad ya Morocco.

Lakini sasa kuna jipya. Mwanaspoti linajua kuna timu nyingine ya nchi hiyo ambayo ipo siriazi ikipania kumng’oa kocha wa Simba, Fadlu Davids tena kwa ahadi ya mkwanja mrefu wa mshahara na posho ndefu.

Mwanaspoti linajua kwamba kuna kitu kinaendelea kati ya Fadlu na FAR Rabat na wamewasiliana kwa simu mara kadhaa wakitaka huduma yake.

Inaelezwa endapo Fadlu atakubali ofa hiyo anaweza kuwa analipwa Sh114 milioni kwa mwezi ambacho ni kiasi maradufu ya kile anacholipwa Msimbazi. Kocha Mtunisia, Mouin Chaabani wa RS Berkane ndiye anayeongoza kwa kupokea mshahara mkubwa zaidi Morocco akipokea zaidi ya Sh120 milioni kwa mwezi.

NB 01

Rabat inataka kocha mpya baada ya kumtimua aliyekuwa kocha wao Mfaransa Hubert Velud ambaye ameiongoza timu hiyo kwenye mechi 19 za msimu huu na Mwanaspoti linajua kwamba kocha wa zamani wa Yanga, Nabi Mohammed ni miongoni mwa watu waliopigiwa simu kuulizwa kuhusiana na Fadlu na akawaambia ni bonge la kocha anayeendana na mahitaji yao ya muda mrefu.

Velud tangu aanze kuifundisha timu hiyo imepoteza nguvu kubwa tofauti na ilivyokuwa chini ya Nabi ambaye kwasasa yupo Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini. FAR inashika nafasi ya tatu kwenye ligi msimamo ukiongozwa na RS Berkane huku nafasi ya pili ikishikiliwa na Renaisance Zemamra.

Mwanaspoti linajua mabosi wa juu wa FAR tayari wameshampigia simu Fadlu ikimpa ofa kubwa ambayo itahitaji uamuzi mgumu kwa kocha huyo raia wa Afrika Kusini kuikataa ili abaki Simba ambayo tayari ufundi wake umewanogea kwani wanacheza soka la kisasa na namba zinaonekana kwenye majedwali.

FAR ambako anachezea Henock Inonga, inamtaka Fadlu kama chaguo lao namba moja kutokana na kocha huyo kulijua vizuri soka la Morocco baada ya awali kutumika nchini humo akiwa kocha msaidizi pale Raja Athletic ambao ndio mabingwa watetezi.

Fadlu mwenye miaka 43, baada ya kuwapa ubingwa huo Raja alitimka akichukuliwa na Simba ambayo ameiongoza kufuzu robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kumaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara wakiwa vinara, akiibadilisha pakubwa timu hiyo ya Msimbazi.

NB 02

Hata hivyo, juzi Fadlu alishushwa hadi nafasi ya pili baada ya Simba kupata sare ya kushtua ya bao 1-1 ugenini dhidi ya Fountain Gate nafasi ya kwanza sasa ikishikwa na mabingwa watetezi Yanga wakiwa na pointi 45.

Taarifa zinasema Fadlu bado yuko njia panda kukubaliana na ofa hiyo au kuikataa ambapo akili yake inataka kumalizia msimu akiwa na wekundu hao ingawa FAR wanamuwekea presha kubwa kocha huyo anayeelezwa kuwa na hofu ya Mungu na asiye na tamaa ya fedha.

Akimzungumzia Fadlu juu ya ofa hiyo Nabi ambaye amewahi kung’ara na Yanga na kukutana na Msauzi huyo kwenye ligi ya Morocco, akimsifu ni kocha wa kisasa anayejua kuendeleza viwango vya wachezaji wake.

“Namfahamu Fadlu, nilikutana naye tukiwa wapinzani kule Morocco akiwa na Raja na mimi FAR Rabat, ni kocha mzuri anayefundisha kisasa, analijua soka la Morocco na ushindani na changamoto zake, FAR itakuwa imepata kocha mzuri lakini sijajua kama atakubaliana kuachana na Simba,” alisema Nabi ambaye amejenga jina Bongo.

“Unajua huwezi kulinganisha kabisa maslahi ambayo unaweza kuyapata Tanzania na kule Morocco lakini pia hata mazingira ya kazi, kule wameendelea sana kwa miundombinu.”

Moja ya presha ambayo FAR imeiweka kwa Fadlu ni kwamba ipo tayari kulipa gharama zozote za kuvunjia mkataba wake na Simba endapo itahitajika

NB 03

KWANINI WAARABU WANAVAMIA BONGO?

Simba na Yanga zinatamba kwenye mashindano ya klabu Afrika katika kipindi cha miaka sita ya hivi karibuni jambo lililozifanya ziwe gumzo Afrika.

Hata hivyo, wakati Yanga na Simba zikionekana kuleta ubishi katika mashindano ya kimataifa, bado zinasumbuliwa na nguvu ya fedha ambayo timu nyingi kutoka Kaskazini mwa Afrika zimekuwa nayo kulinganisha na vigogo hivyo viwili vya Tanzania.

Katika kipindi hicho cha miaka sita, timu za Kaskazini zimeonyesha jeuri ya fedha kwa kung’oa baadhi ya wachezaji muhimu na makocha wa timu hizo kutokana na ushawishi wa kifedha ambao zimekuwa zikiwapa.

“Wachezaji pia hukubali kupokea ofa hizo kubwa kwa haraka kwavile wanaona ni ngumu kwao kucheza Ulaya ambako ndiko zilipo ndoto za wengi, lakini hata ushawishi wa mawakala wao ni mkubwa sana kwavile na wao wana uhakika wa kupata cha juu kwa haraka na wanajua ndani ya muda mfupi mchezaji atauzwa tena hatadumu Uarabuni,” anasema Philip Nkini, Mchambuzi wa Mwanaspoti. 

Tathmini inaonyesha makocha au wachezaji hao wamejikuta wakiziacha kwenye mataa Simba na Yanga na kufuata mishahara minono Uarabuni ambako hatahivyo, wengi wao wamekuwa hawadumu zaidi ya msimu mmoja kutokana na mazingira, uhitaji na ushindani.

Timu za Afrika Kaskazini zina bajeti kubwa tofauti na Tanzania au Afrika Mashariki ambako bado klabu kubwa ikiwemo Simba, Yanga bado zinategemea kipato kutoka kwa wadhamini ambao ni wachache na mapato ya milangoni sambamba na ada za wanachama wao.

Pia kupanda kwa soka la Tanzania limekuwa kivutio kingine cha timu hizo za Waarabu kukimbilia huku kuchukua makocha na wachezaji, kwani wameona nguvu zao viwanjani katika mechi dhidi ya vigogo wa Tanzania katika michuano ya CAF.

Hapa chini ni orodha ya wachezaji na makocha waliowahi kuzitumikia Yanga na Simba na kisha kufuata malisho ya kijani zaidi huko Uarabuni.

Februari 23, 2021, Luis Miquissone alifunga bao la kideoni katika mechi ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly na  kuiwezesha Simba kupata ushindi wa bao 1-0.

Bao hilo liliifanya Al Ahly ivutike kumsajili Miquissone ambapo ilitoa dau la Dola 900,000 (Sh2.3 bilioni), dau ambalo Simba haikulikataa.

Dirisha kubwa la usajili kwa mwaka 2023 halikuacha furaha kwa mashabiki wa Simba kwani baada ya Miquissone kusajiliwa na Al Ahly, nyota mwingine wa timu hiyo, Clatous Chama naye aliondoka kwa kujiunga na RS Berkane ya Morocco.

Kiasi cha fedha kinachotajwa kufikia Sh 1.5 bilioni kilitumiwa na RS Berkane kuishawishi Simba iwauzie mchezaji huyo jambo ambalo lilitimia.

Noti za FAR Rabat ya Morocco ziliacha majonzi Simba baada ya timu hiyo kumbeba ghafla kocha wake mkuu, Sven Vandenbroeck ambaye alikuwa ametoka kuiongoza Simba kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2020/2021.

Japo kiwango cha mshahara ambacho alikipata AS FAR hakikutajwa, inasemekana kuwa Vandenbroeck alipata mshahara mkubwa zaidi ambao ulimshawishi kwenda Morocco.

Baada ya kuiongoza Yanga kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara mbili mfululizo, Juni, 2023 kocha Nasreddine Nabi alifuata malisho bora zaidi Morocco ambako alienda kujiunga na AS FAR ambayo ilimpa maslahi bora zaidi.

Akiwa Morocco, Nabi aliiongoza AS FAR kumaliza katika nafasi ya pili.

Mwaka huohuo, Yanga ilipata pigo jingine kufuatia kuondoka kwa mshambuliaji wake aliyekuwa moto wa kuotea mbali kwa kufumania nyavu, Fiston Mayele.

Mayele aliondoka baada ya Yanga kumuuza kwa Pyramids FC kwa dau la Sh2 bilioni.

Baada ya kuitumikia Yanga kwa siku 82 tu, kocha Sead Ramovic amekumbwa na upepo wa noti za Waarabu baada ya kujiunga na CR Belouzdad inayoshiriki Ligi Kuu ya Algeria.

Mshahara wa Dola 40,000 kwa mwezi, umeonekana kumshawishi Ramovic aiache Yanga kwenye mataa na kwenda Algeria.

Related Posts