​​​​​​​Ramaphosa atema nyongo Trump kusitisha ufadhili

Mwanza. Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amesema kuwa taifa hilo haliko tayari kupelekeshwa na taifa lolote, kauli ambayo imedaiwa kuwa ameitoa ili kumjibu Rais wa Marekani, Donald Trump.

Shirika la Reuters limeripoti kuwa, Ramaphosa alitoa kauli hiyo jana Alhamisi Februari 6, 2025, wakati wa hotuba yake ya mwaka kwa umma, zikiwa zimepita siku nne tangu Rais Trump atishie kusitisha misaada yote inayotolewa na Marekani kwa Afrika Kusini.

Kupitia hotuba yake, bila kumtaja Trump, Rais huyo (Ramaphosa) ameonekana kujibu tuhuma za Trump dhidi ya Serikali ya Afrika Kusini, kuwa kuna vitendo vinavyokiuka haki za binadamu.

“Sasahivi tunashuhudia kuibuka kwa harakati za utaifa na ulinzi wa nchi,” amesema Ramaphosa alipokuwa akihutubia Bunge la nchi hiyo jijini Cape Town.

“Hiyo ndiyo dunia ambayo tuliomo sasahivi, kuendeleza uchumi ndicho kipaumbele chetu,”

“Ila nisisitize, hatutotetereshwa, wala hatutotolewa kwenye reli. Sisi ni wastahimilivu, na hatutoruhusu kupelekeshwa. Tutasimama pamoja kama nchi na tutazungumza kwa kauli moja ya kulinda maslahi ya taifa letu, uhuru wetu na Demokrasia iliyotajwa kwenye Katiba yetu,” amesema Ramaphosa.

Baada ya kutamka hivyo kwenye hotuba yake, ukumbi mzima wa Bunge ulimpigia Rais Ramaphosa makofi ikiwa ni ishara ya kuonyesha kuridhishwa na kupenda namna Rais huyo anavyoshughulikia msukumo kutoka mataifa ya nje.

Ramaphosa na Serikali yake, walijikuta wakitumia muda mwingi wiki hii kutetea maslahi ya taifa hilo baada ya Rais Trump kuchapisha kwenye akaunti ya Mtandao wake wa ‘Truth Social’ kuwa atasitisha ufadhiri na misaada yote kwa Afrika Kusini kwa alichodai:

 “Kuna utwaaji wa ardhi na kuwashughulikia baadhi ya watu kwa namna ambayo siyo ya kupendeza kabisa,” ameandika Trump bila kutaja watu wanaotendewa vibaya na Serikali hiyo.

Trump ameenda mbali na kuandika kuwa uongozi wa Afrika Kusini umekuwa ukijihusisha na vitendo vya uvunjifu wa Haki za Binadamu jambo ambalo alidai kuwa halitiliwi maanani na vyombo vya habari nchini humo.

 “Serikali ya Afrika Kusini inafanya vitu vya ajabu na mambo yasiyokubalika,” amesema Trump bila kuainisha ni mambo gani yanayofanywa na Afrika Kusini.

Kauli hiyo ya Trump, ilihusishwa na uamuzi wa Afrika Kusini kupitisha sheria inayozipa nguvu mamlaka za nchi hiyo kutwaa ardhi kutoka katika umiliki wa Taasisi binafsi. Hata hivyo, Serikali ya Ramaphosa imekuwa ikikanusha upotoshaji badala yake ilisema sheria hiyo ililenga kuyarejesha maeneo ambayo hayajatumika chini ya usimamizi wa Serikali.

Msemaji wa Ikulu ya Rais, Ramaphosa amesema kauli ya Trump imechochewa na maneno ya upotoshaji yanayosambazwa na msaidizi wake, Bilionea, Elon Musk ambaye ni mzaliwa na Afrika Kusini.

Musk, ambaye aliondoka Afrika Kusini miaka ya 1980, amekuwa mkosoaji mkubwa wa Serikali ya Afrika Kusini kwa kile ambacho anadai inawakandamiza raia wenye asili ya watu weupe (whites).

Pia Musk amesema sheria hiyo inalenga kupora ardhi inayomilikiwa na tabaka ya watu wachache (Whites) wanaoishi na kumiliki sehemu kubwa ya ardhi nchini humo.

Madai hayo ya Trump yamekuja siku chache tangu atangaze kusitisha ufadhiri na misaada iliyokuwa ikitolewa na Marekani kupitisha Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) kwa siku 90 ili kuruhusu tathmini ifanyike juu ya uendeshwaji na ufanisi wake.

Kusitishwa kwa ufadhiri huo kunatajwa kuwa huenda kukasababisha athari ikiwemo kuikosesha Afrika Kusini fedha ambapo taifa hilo linapokea kila mwaka kutoka Marekani kupitia Programu za kuimarisha Afua za VVU/ Ukimwi.

Kutokana na uamuzi huo, Ramaphosa kupitia hotuba yake amesema taifa hilo litapitia changamoto baada ya kusitishwaufadhiri huo, huku akisisitiza kuwa wanapambana kuimarisha huduma za afua za VVU/Ukimwi nchini humo.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.

Related Posts