12 kutoa ushahidi kesi ya kusafirisha binadamu kimagendo

Dar es Salaam.  Serikali imesema kuwa inatarajia kuwa na mashahidi 12, watakaotoa ushahidi katika kesi ya kusafirisha binadamu kimagendo, inayomkabili raia ya Ufaransa, Michael Mroivili.

Mbali na mashahidi hao, pia Serikali itakuwa na vielelezo 18. Mroivili anakabiliwa shtaka moja katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Wakili wa Serikali, Raphael Mpuya, ameieleza Mahakama hivyo, leo Ijumaa Februari 7, 2025 wakati akimsomea hoja za awali (PH) mshtakiwa huyo.

Wakili Mpuya amemsomea PH, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Gwantwa Mwankuga, baada ya upelelezi wa kesi hiyo kukamilika.

Akimsomea hoja hizo alidai, Mpuya alidai mshitakiwa akiwa ni raia wa Ufaransa mwenye asili yake Comoro  alizaliwa katika visiwa vya Comoro.

Wakili Mpuya, alidai mshtakiwa alikuja  Tanzania kwa mara ya kwanza mwaka 2008 kwa lengo la matibabu ya macho, hivyo siku nyingine akiwa Tanzania alikuwa na madhumuni mengine ya kupanga na raia wenzake ndipo alipokea kiasi cha fedha ili kuandaa safari.

Aliendelea kudai kuwa  Januari 3, 2025  katika Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) uliopo Wilaya ya Ilala, mshtakiwa akiwa raia wa Ufaransa alifanya mchakato wa  kusafirisha raia wawili kutoka Tanzania na kwenda nchi ya Ufaransa na Italia.

Aliwataja raia hao kuwa ni Said  Omar na Aliane Abdouluihabi wote wakiwa ni raia wa Comoro ambao Desemba, 2024, mshitakiwa Mroivili alikata tiketi kwa Wakala wa ndege za Ethiopia kutoka Dar es Salaam hadi Adds Ababa.

Pia, alidai Januari 2025, Mroivili aliwakatia tiketi ya  kutoka Addis Ababa hadi Roma nchini Italia.

Mshtakiwa hiyo pia anadaiwa kukodi gari ya kuwachua kuwa hotelini iliyoko Kariakoo, Omar na Abdouloihabi hadi  uwanja wa Ndege kwa safari huku akifanya mpango kwa kuwaelekeza namna ya kukwepa vizuizi vya Uhamiaji.

Watu hao wakiwa wanasubiri  kwa muda sehemu ya kukaa abiria kwa safari maofisa Uhamiaji waliwashtukia na kuwakamata kwa kukwepa ukaguzi na wakiwa wanakamatwa tayari mshitakiwa Mroivili alikuwa ameshaondoka  uwanjani hapo.

Inadaiwa mshitakiwa huyo, alikamatiwa uwanja wa Ndege wa Aman Abed Karume, Zanzibar akiwa katika taratibu za kurudi nchini Ufaransa.

Baada ya kumsomea hoja hizo, mshitakiwa alikiri taarifa zake binafsi, kukamatwa, kuhojiwa na maofisa wa Uhamiaji na kufikishwa mahakamani, huku akikana kutenda kosa hilo.

Hakimu Gwantwa aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 12, 2025 kwa usikilizwaji na mshitakiwa yuko nje kwa dhamana.

Related Posts