Manyara kuanza kusafisha figo kwa wagonjwa

Babati. Wagonjwa wa figo katika Mkoa wa Manyara wataanza kunufaika na huduma ya kusafisha figo baada ya kupatikana mashine sita zenye uwezo wa kusafisha damu za wagonjwa 12 kwa siku, kwenye hospitali ya rufaa ya mkoa huo.

Huduma hiyo itawaondolea wagonjwa hao adha ya kusafiri umbali mrefu hadi hospitali ya rufaa ya Kilutheri ya Haydom na ya Kanda ya KCMC iliyopo mjini Moshi na Mount Meru ya jijini Arusha.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga ameyasema hayo leo Februari 7, 2025 mjini Babati wakati akizindua bodi ya ushauri ya hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Manyara.

Sendiga amesema huduma hiyo itaanza kutolewa baada ya wiki moja kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara.

“Mashine hizo zina uwezo wa kusafisha damu kwa wagonjwa 12 kwa siku na zitasaidia kupunguza adha ya kwenda mbali, gharama na muda,” amesema Sendiga.

Amewataka wajumbe wa bodi ya hospitali hiyo kushauri, kusimamia huduma bora na matumizi sahihi ya rasilimali za hospitali hiyo ipasavyo.

“Mwenyekiti na wajumbe wa bodi mnapaswa kuwa waadilifu, wawazi na kuzingatia masilahi bora kwa jamii kwa lengo la kuhakikisha huduma bora inatolewa kwa wahusika,” amesema Sendiga.

Mkazi wa Mtaa wa Nangara uliopo mjini Babati, Ezekiel Mao amesema ni hatua kubwa kwa huduma ya kusafisha figo kupatikana wilayani humo hivi sasa kwenye hospitali ya rufaa ya mkoa huo.

Mmoja wa wajumbe wa bodi hiyo, Vrajilal Jituson ambaye ni mbunge mstaafu wa Babati Vijijini, amepongeza hatua hiyo akisema itasogeza karibu huduma kwa wahitaji.

Jituson amesema kwa sasa Mkoa wa Manyara unazidi kupiga hatua ya maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo kwenye huduma za afya, elimu, maji na nyingine.

“Kwa sasa maendeleo yanazidi kuonekana Manyara kupitia Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kule Mwada kuna shule mpya ya wavulana ya kidato cha sita imejengwa, tunasubiri uwanja wa ndege,” amesema.

Related Posts