Dodoma. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa amewaonya viongozi kutocheza na fedha za mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu na kuwa atakayebainika eneo lake lina kikundi hewa atawajibishwa.
Mikopo hiyo ilisitishwa Aprili 13, 2023 ili kutafuta utaratibu mwingine wa kuitoa baada ya uwepo wa kelele nyingi kuhusu namna ya ukopeshaji huo ikiwemo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (LAAC) ambao walisema fedha hizo zilikuwa zikiliwa na wajanja hata kukosa mwendelezo wake.
Mchengerwa ametoa onyo hilo leo Februari 7, 2025 wakati wa hafla ya utiaji saini mikataba ya utoaji mikopo hiyo kati ya halmashauri 10 na benki tatu jijini Dodoma.
“Kabla ya waziri hajawajibika, atawajibika mkuu wa mkoa, wilaya na wakurugenzi, nawaambia wazi kabisa, tumefika hapa kwa sababu kuna watumishi wasio waaminifu ambao walitafuna fedha hizi kwa kukopeshana wenyewe na hawakuwa na sifa ya kupokea mikopo hii,” amesema.
Amesema kanuni zimeboreshwa zinawapa nguvu maofisa maendeleo ya jamii na benki zinazotoa fedha hizo kufuatilia, kusimamia na kuvikagua vikundi kabla ya kutoa fedha hizo.
Amezitaka mamlaka za serikali za mitaa kuendelea kuchangia fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya mikopo hii kwa mujibu wa sheria ya fedha za serikali za mitaa.
“Katibu Mkuu, niletee orodha kama kuna halmashauri ambazo hazijachangia na zinadorora kuchangia na kama kuna halmashauri ambayo haijatekeleza ya maelekezo ya Rais,” amesema.
Amesema zaidi ya Sh234 bilioni zinakusudiwa kupelekwa kwa wananchi.
Naye Katibu Mkuu wa Tamisemi, Profesa Adolf Ndunguru amesema kusainiwa mikataba hiyo ni mwanzo wa mapinduzi ya kuhakikisha mikopo hiyo ya asilimia 10 inakuwa na tija tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Meya wa Jiji la Dodoma, Profesa Davis Mwamfupe amesema licha ya mfumo wa taarifa za wakopaji kuwa kidijitali ni vema mikopo hiyo kuangaliwa inafanya kazi gani kwa kuwa imewekwa kwa ajili ya kutoa huduma, kuzalisha na kuajiri ili matokeo chanya yaonekane.
Mkuu wa Ofisi ya NMB Makao Makuu ndogo Dodoma, Vicky Bishubo amesema hadi sasa benki hiyo imetoa mikopo yenye thamani ya Sh2 trilioni kwa vikundi vya wajasiriamali na makundi mbalimbali.
“NMB itahakikisha walengwa wa kundi hili wanapata mikopo waliosajiliwa na kutambulishwa kwetu na halmashauri, tutajiridhisha kama vikundi ni halali na zitatumika kwa malengo gani,” amesema.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Mwambapa amesema hadi sasa benki hiyo imetoa mikopo ya thamani ya Sh2.9 trilioni kwa makundi hayo na kwamba wataalam wamezunguka nchi nzima kutoa elimu kuhusu urejeshaji wake.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Biashara ya Uchumi (UCB), Samwel Wado amesema watahakikisha wanatoa mikopo kwa walengwa katika Wilaya ya Siha na kutoa elimu kuhusu matumizi yake na urejeshaji ili iwe na matokeo chanya.