Dodoma. Jeshi la Polisi limewaokoa watoto 122 waliokuwa wakitumikishwa katika biashara ya ukahaba kwenye madanguro, kuomba mitaani, na kwenye makazi ya watu.
Watoto hao wameokolewa katika kipindi cha Julai, 2023 hadi Aprili, 2024.
Hayo yamesemwa bungeni leo Mei 15, 2024 na Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Yusuf Masauni alipowasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/25. Wizara imeomba Bunge liidhinishe Sh1.7 trilioni.
Masauni amesema wizara imeendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria ya kuzuia usafirishaji haramu wa binadamu.
Amesema katika kipindi cha Julai, 2023 hadi Aprili, 2024, waathirika 184 waliokuwa wakitumikishwa wameokolewa.
“Jumla ya waathirika 184 waliokuwa wakitumikishwa kuomba mitaani, kufanya kazi majumbani, kwenye mashamba, kuchunga mifugo na kwenye madanguro wameokolewa na kupewa huduma za kibinadamu,” amesema.
“Kati ya hao, waathirika 122 walikuwa ni watoto na 62 walikuwa ni watu wazima. Wahalifu wanne waliokuwa wakijihusisha na usafirishaji haramu wa binadamu walihukumiwa kifungo gerezani na watuhumiwa 11 kesi zao ziko katika hatua mbalimbali za usikilizwaji,” amesema.
Mwaka 2023 mkoani Dar es Salaam yalivunjwa madanguro 700 ikiwa ni hatua ya kupambana na mmomonyoko wa maadili na maambukizi ya magonjwa ya zinaa na Virusi vya Ukimwi.
Madanguro hayo yalivunjwa wakati wa operesheni maalumu iliyofanywa na timu ya mkoa kati ya Oktoba na Novemba 2023.
Ilielezwa madanguro 550 yalivunjwa wilayani Kinondoni na mengine Ubungo kwenye kata za Manzese na Mbezi Luis.