Dodoma. Hatimaye Serikali imesikia kilio cha wafanyabiashara walioko katika Mfumo wa Stakabadhi za Ghala, kwa kuagiza kufanyika mapitio ya viwango na miongozo yote inayohusiana na biashara ya mazao kupitia mfumo huo.
Hatua hiyo imekuja muda mfupi baada ya Mwendesha Maghala ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Cropstan Investiment Ltd, Simon Nkana kulalamikia kushuka kwa uzito kwa mazao yanayohifadhiwa ghalani.
“Sasa katika haya mazao unavyotoa na kupokea kuna kiwango cha unyevu kinashuka ambacho huondoka na uzito wa zao husika. Wadau wenzetu wameshindwa kulitambua hili kuwa ikitokea unyaufu maana yake uzito unapungua na hivyo uzito unaoingia na zao si unavyotoka,” amesema.
Amesema suala hilo limewapa jina baya waendesha maghala na baadhi wameitwa kuwa ni wezi lakini anaamini kuwa kuna jambo la kisayansi na kuomba Shirika la Viwango Tanzania (TBS), kufanya utafiti na kuja na kiwango cha mazao baada ya kutunzwa ghalani.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo ametoa agizo hilo leo Ijumaa Februari 7, 2025 wakati akihitimisha msimu wa Biashara ya Bidhaa za Kilimo kupitia mfumo huo na kufungua msimu mpya wa 2025/26.
Amesema kumekuwa na malalamiko katika msimu uliopita wa mauzo ya mazao kupitia mfumo huo ya upungufu wa uzito hususani katika zao la korosho.
“Inawezekana wakati wa kusafisha, anaweza kuona kilo zimepungua na hiyo inatokana na ubora,”amesema.
Amesema ili kutatua changamoto hiyo TBS, Bodi ya ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB) na Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) zifanye mapitio ya viwango na miongozo yote inayohusiana na biashara ya mazao kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani.
“Tukubaliane kwa pamoja kipi kiwango cha ubora ili kuondoa mashaka kwa wakulima ili wawe na ujasiri, waweze kufuata viwango hivyo na kuondoa malalamiko yaliyopo na kuyapatia suluhisho la kudumu kabla ya mwisho msimu uja,” amesema.
Aidha, Dk Jafo amesema katika msimu wa 2024/2025, jumla ya bidhaa 14 zilikusanywa na kuuzwa kupitia mfumo wa stakabadhi za ghala.
Amesema kwa mara ya kwanza kumekuwa na ongezeko kubwa la uzalishaji na ukusanyaji wa mazao, ambapo tani 810.2 zilikusanywa, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia 80 ikilinganishwa na msimu wa 2023/2024, ambapo zilikusanywa tani 451.19.
Amesema ongezeko hilo halikuakisiwa tu katika kiwango cha mazao bali pia katika thamani ya mapato ya wakulima.
Dk Jafo amesema kutokana na wingi wa bidhaa pamoja na kuimarika kwa bei sokoni, wakulima walilipwa Sh2.9 trilioni, ikiwa ni ongezeko la asilimia 142 ikilinganishwa na Sh1.2 trilioni walizopata msimu uliotangulia.
“Mapato yatokanayo na ushuru yameongezeka kutoka Sh36 bilioni msimu wa 2023/2024 hadi kufikia Sh87 bilioni msimu huu unaokamilika. Hii ni ishara wazi kuwa mfumo wa stakabadhi za ghalani siyo tu unawanufaisha wakulima bali pia unachangia kwa kiasi kikubwa mapato ya Serikali za Mitaa,” amesema.
Mkulima wa mbaazi, Yohana Makasi amesema kuwa mfumo huo umewasaidia mfumo huo umewasaidia kuongeza bei ya mbaazi ambayo ilikuwa ni Sh200 kwa kilo hadi Sh2,000.
“Mfumo huu umetusaidia kuondoa hasara tuliyokuwa tukiipata kwa kuuza bei ambayo hailingani na gharama za uzalishaji,” amesema.