Morogoro. Wilaya ya Kilosa inatarajia kuvuna mapato ya Sh1.17 bilioni kama gawio baada ya kuhifadhi misitu iliyowezasha uvunaji wa tani za ujazo 545,433 za hewa ya ukaa (kaboni) katika misitu ya vijiji vyake katika kipindi cha 2023 mpaka Februari 2024.
Ikumbukwe kuwa kwa mujibu wa Wizara ya Muungano na Mazingira, Tanzania inalenga kuingiza dola za Marekani bilioni 1 (takriban Sh2.4 trilioni) kila mwaka kutokana na biashara ya kaboni.
Katika hotuba ya wizara hiyo iliyosomwa bungeni Machi 2024 wizara ilisema, “Katika mwaka wa fedha hadi kufikia Machi, 2024 Jumla ya miradi 24 ya biashara ya kaboni ilisajiliwa na ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Kiasi cha dola za Marekani milioni 12.63 (Sh32 bilioni) zimelipwa kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini kama gawio la mauzo ya viwango vya kaboni”.
Kilosa ikiwa miongoni mwa maeneo yanayonufaika halmashauri na vijiji vimeanza kunufaika.
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka amewataka wakazi wa wilaya hiyo kujikita katika biashara ya hewa ukaa, kutambua kuwa ni moja miongoni mwa njia mkakati za ukombozi kwao kuanzia ngazi ya vijiji na halmashauri.
“Ninaimani sana na ninyi kwamba mtakwenda kufanya mageuzi ya kulinda na kutunza rasilimali tulizonazo ili tija iweze kuonekana, lazima tukiri kwamba bado tunachangamoto, mfano mzuri ni migogoro kati ya kijiji na kijiji, kamati za maliasili za kijiji fulani kuvamia kijiji fulani,” alisema.
Shaka aliongeza kuwa mafanikio hayo yalipatikana kwa kutunza mazingira katika misitu ya vijiji huku Kijiji cha Malolo, msiba na Mhenda vikifanya vizuri zaidi katika kipindi cha 2023 mpaka Februari 2024.
“Tuna uwezo wa kupunguza umaskini kupitia biashara hii ya hewa ukaa, lakini pia tuna uwezo wa kuifanya halmashauri hii kuwa ya mfano kupitia mapato haya ya biashara ya hewa ukaa kadri uwekezaji huu utakavyozidi kutanuka” ameeleza.
Hata hivyo, Shaka amepiga marufuku uvunaji na usafishaji mashamba holela huku akisitiza kuchukuliwa kwa hatua kali za kisheria kwa wote wataobainika kufanya hivyo bila ya kuwa na vibali halali.
“Vijiji kwa kushirikiana na halmashauri ya nendeni mkaboreshe sheria ndogo ndogo za usimamizi wa misitu ili kuweka adhabu kali zaidi kwa mtu yeyote atakayehusika na ukataji wa miti hovyo na uharibifu wa misitu,” alisema Shaka.
Biashara hii inayoratibiwa na Kituo cha Kitaifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) inahusisha hatua mbalimbali kusajili, zikiwemo utambuzi wa miradi inayostahili, tathmini ya athari zake kwa mazingira na uwezo wake wa kupunguza hewa ukaa, pamoja na uhakiki wa uzingatiaji wake wa viwango na kanuni za kimataifa.
Baada ya miradi hii kusajiliwa na kuanza kutekelezwa, haitachangia tu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kupunguza uzalishaji wa gesi joto, bali pia itatoa fursa za uwekezaji zenye faida.