Dar es Salaam. Wakazi wa Kinyerezi, Tabata na Ukonga imeelezwa wataondokana na adha ya kukosa maji iliyokuwa ikiwakabili baada ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) kutangaza kuanza kusambaza maji safi kuanzia Februari 20, 2025.
Hatua hiyo imekuja baada ya kukamilika kwa mradi wa Maji wa Bangulo unaogharimu kiasi cha Sh36.8 bilioni ambao utahudumia wakazi zaidi ya 450,000 huku ukijumuisha ujenzi wa tenki kubwa la kuhifadhi maji lita milioni tisa na ulazaji wa mtandao wa bomba wenye kilomita 108.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Mkama Bwire leo Ijumaa Februari 7, 2025 kwenye ziara ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na waandishi wa habari iliyotembelea maeneo mbalimbali hususan ujenzi wa Bwawa la Kidunda lililopo mkoani Morogoro.
“Katika huu mradi wa kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji kilichokuwa kimebaki ni kuunganishwa kwa mitambo yetu ya umeme ianze kazi na ndani ya siku mbili hizi tutaanza kuwasha mitambo yetu kuanza majaribio,” amesema.
Bwire amewataka wananchi kwa kipindi hiki kuwa na subira hadi ifikapo tarehe hiyo tayari kuanza kuyaachia maji hayo.
Kauli ya Dawasa inatoka kipindi ambacho baadhi ya maeneo mathalani ya Tabata yakiwa hayana maji kwa siku tatu na kwingine siku zaidi ya siku tano.

Joseph John, Mkazi wa Mawenzi anasema:”Sisi hatuna maji siku ya tatu, tunachokitaka ni maji si maneno maneno. Hivyo wapambane maji yatoke.”
Mkazi wa Kwa Mkua, Mariam Abdallah amesema wana zaidi ya wiki sasa hawana maji na hata yakitoka yanatoka usiku wakiwa wamelala.
Katika ziara hiyo, Bwire amesema kuna mchakato wa kuunganisha mifumo ya vyanzo vya Ruvu Juu na Ruvu Chini ili kupunguza changamoto kwenye usambazaji wa maji.
“Italazimika kuwa na pampu za kusukuma kulingana na eneo moja kuwa juu lingine chini. Tukishaunganisha maji yatakuwa yanatoka eneo moja kwenda lingine,” amebanisha.
Wateja waombwa kuwa na matenki
Aidha katika hatua nyingine Dawasa imewaomba wateja wake kuwa na tabia ya kuwa na matenki kwaajili ya kuhifadhi maji ili kusudi itakapotokea changamoto yoyote waweze kuwa nayo.
Bwire ametoa rai hiyo ili wakazi wawe na maji muda wote kwaajili ya matumizi yao na wasitetereke pale kunapotokea changamoto.
Hata hivyo, amesema Serikali inaendelea kujenga matenki mengine mengi ya kuhifadhi mamilioni ya lita za maji maeneo mbalimbali.
“Mtunzaji wa kwanza ni yule wa nyumbani wito wangu angalau kaya ikiwa na tenki la lita 5000 kwasababu unakua na uhakika wa kutumia hadi siku tatu endapo huduma ya maji ikiwa haipatikani,” amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile ameishukuru Dawasa kwa juhudi za kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo muhimu.
Aidha, ametoa rai kwa mamlaka hiyo kuwapeleka viongozi wa Serikali za mitaa katika maeneo ya kuzalisha maji ili kuwa mabalozi kwa wakazi wao.
“Kikubwa huu umoja mlionao muendelee nao pia tunaamini mnadhibiti uvujaji wa maji na usimamizi bora wa miundombinu,” amesema Balile.
Ziara hiyo ya TEF na waandishi ilianzia katika mradi wa Bwawa la Kidunda lilikoko Morogoro ambalo kukamilika kwake litaondoa changamoto ya ukosefu wa maji katika Jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani.
Bwawa hilo linajengwa kwaajili ya kutunza maji yatakayozalishwa na kusambazwa pale yatakapopungua katika mitambo ya uzalishaji ya Ruvu Juu na Chini