KIPIGO cha mabao 6-1 ilichopata KenGold kutoka kwa Yanga kinaiuma timu hiyo iliyosema hasira na machungu wanatarajia kumalizia kwa Fountain Gate watakaoumana nao Jumatatu kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
KenGold iliyofanya usajili wa kishindo katika dirisha dogo, ilikamuliwa na Yanga kwa kipigo hicho kilichowekwa rekodi msimu huu kwa kuwa kikubwa zaidi, huku baadhi ya wachezaji waliosajiliwa wakishindwa kuonekana uwanjani ukiondoa wachache akiwamo Zawadi Mauya walioonekanpale KMC.
Timu hiyo ambayo imepanda daraja msimu huu na inaburuza mkia ikiwa na pointi sita baada ya mechi 17, imesema mechi ijayo ndio kipimo kizuri kama wamezaliwa upya, huku mabosi wa klabu hiyo wakiwatuliza mashabiki kwamba chama hilo halishuki daraja.
KenGold itakutana na Fountain iliyotoka kulazimisha sare ya 1-1 dhidi ya Simba, huku katika mchezo baina yao duru lililopita, Wachimba Dhahabu hao walichezea kichapo cha 2-1 mjini Manyara na hivyo Jumatatu itakuwa na kazi ya kulipa kisasi ikiwa nyumbani, jijini Mbeya.
Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Omary Kapilima alisema katika mechi iliyopita dhidi ya Yanga wamebaini kuwa, mabeki walipoteza umakini, lakini wapo baadhi ya mastaa ambao hawakucheza, hivyo mchezo ujao lazima kieleweke.
Alisema katika michezo 13 iliyopbaki, watatumia vyema mechi nane watakazocheza nyumbani kutafuta pointi 24 ambazo zitaweza kuwaondoa mkiani na kubaki salama Ligi Kuu.
“Tunaenda kuanza na Fountain Gate, tuna mechi nane nyumbani ambazo kwa hesabu zetu zitaweza kutuvusha kubaki salama Ligi Kuu msimu ujao, suala la kushuka daraja halipo kwa Ken Gold,” alisema Kapilima.