Dar es Salaam. Raia wa China, Weng Jianjin amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka matatu, yakiwamo ya kukusanya na kuendesha biashara ya upatu na kujipatia Sh34.7 bilioni kwa njia ya udanganyifu.
Jianjin (42), mfanyabiashara na mkazi wa Msasani alifikishwa mahakamani jana Februari 7, 2025 na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali, Frank Rimoy, mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Franco Kiswaga.
Kabla ya kusomewa mashtaka, Hakimu Kiswaga alimweleza mshtakiwa hatakiwi kujibu chochote mahakamani hapo kwa kuwa kesi inayomkabili ni ya uhujumu uchumi na mahakama hiyo haina uwezo wa kuisikiliza, isipokuwa kwa kibali maalumu.
Baada ya maelezo hayo, Rimoy alimsomea mashtaka, la kwanza akidaiwa kati ya Januari 2023 na Mei 2023 katika nchi za Botswana na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alikusanya fedha za Botswana (Pula) 188.6 milioni sawa na Sh34.7 bilioni kutoka kwa watu tofauti wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zambia.
Anadaiwa kwa makusudi aliwaahidi watu hao kuwa fedha walizopanda zitaenda kuongezeka maradufu na watapata fedha nyingi zaidi, wakati akijua si kweli.
Katika shtaka la pili anadaiwa kujipatia fedha kwa udanganyifu, kosa analodaiwa kulitenda kati ya tarehe hizo na maeneo yaleyale.
Anadaiwa alijipatia Sh34.7 bilioni kutoka kwa watu tofauti raia wa Tanzania na Zambia kwa ajili ya kuwekeza kibiashara katika kampuni ya Ecoplexus, wakati akijua si kweli.
Katika shtaka la tatu anadaiwa kutakatisha fedha, tukio analodaiwa kulitenda katika tarehe hizo na maeneo ya nchi hizo mbili.
Mshtakiwa anadaiwa alijipatia Sh34.7 bilioni, wakati akijua fedha hizo ni zao tangulizi la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Baada ya mshtakiwa kusomewa mashtaka, upande wa Jamhuri ulidai upelelezi unaendelea, hivyo uliomba terehe nyingine kwa ajili ya shauri hilo kutajwa.
Hakimu Kiswaga aliahirisha kesi hadi Februari 20, 2025. Mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha linalomkabili kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.