Unguja. Jaji Mkuu wa Zanzibar, Khamis Ramadhan Abdalla amewataka mawakili wapya waliopatiwa vyeti vya uwakili kuzingatia uadilifu na weledi kama inavyotaka sheria namba moja ya mwaka 2020 ili kuimarisha imani ya wananchi katika mfumo wa haki.
Pia, amewataka kutumia busara katika kutoza fedha wateja wao, kwa kuwa, kumekuwa na vilio vingi vinayotokana na wananchi wanyonge kushindwa kuwafikia mawakili kwa sababu ya viwango vikubwa vya fedha wanavyotozwa.
Jaji Khamis amesema hayo katika hafla ya kuwakabidhi vyeti mawakili wapya 17 Mahakama Kuu Tunguu, leo Jumamosi, Februari 8, 2025.
Amesema kwa sasa kuna uhitaji mkubwa wa mawakili kwa jamii, hivyo akawataka watumie fursa hiyo kuhakikisha wanatoa haki kwa uadilifu kwa wananchi.
Amesisitiza umuhimu wa mawakili kuhakikisha haki na utawala wa sheria inatekelezwa ipasavyo.
“Mawakili ni nguzo muhimu katika mfumo wa haki za binadamu na utawala wa sheria, hivyo ni jukumu lenu kuhakikisha haki za wananchi zinaheshimiwa na sheria inatekelezwa ipasavyo. Twende kwanza tukaioseme na kuilewa sheria inayotuongoza,” amesema Jaji Khamis.
“Niwasihi kuwa vyeti mlivyopewa si vya kwenda kutambia huko mitaani, mtambue kuwa Zanzibar tuna mawakili zaidi ya 1,000, tumebaini kuwa mawakili wengi wanachukua vyeti hivi kama kuongeza CV zao katika kazi,”amesema Jaji Khamis.
Amesema kumekuwapo wananachi wanaohitaji mawakili lakini waliopo hawatoshi, hivyo ni vyema kutumia fursa hiyo kuwasaidia kupata haki zao.
Pia, Jaji Khamis amewataka kuongeza maarifa ya elimu hususani katika kada za kodi, sheria za kazi na sheria za mafuta na gesi ambazo zinauhitaji mkubwa wa wataalamu hao.
“Tunapokuwa na mawakili ambao wanaweza kudadavua mambo mbele ya majaji na mahakimu kwetu ni faraja kubwa,” amesema.
Jaji Khamis amesema ni vyema mawakili wakajitolea kufanya kazi ndogo-ndogo hatua itakayowasaidia kufahamika sehemu mbalimbali, hivyo kushirikishwa katika utetezi wa haki.
Mrajisi wa Mahakama Zanzibar, Valentina Andrew Katema amesema mchakato wa kuwapata mawakili hao ulianza tangu mwaka jana 2024 ambapo vigezo mbalimbali vilitumika.
Naye, Rais wa Chama cha Mawakili Zanzibar (ZLS), Joseph Shaaban Magazi amewasihi mawakili wapya kuheshimu viapo vyao, kuvisimamia, kuviheshimu na kutenda haki.
Amesema wakati wa kutekeleza majukumu yao watakutana na changamoto nyingi ambazo zinaweza kuwafanya kushindwa kusimamia vyema majukumu yao na kazi za Mahakama.
Amesema Mahakama ni chombo cha kutenda haki, hivyo kila mmoja ana wajibu wa kuisadia ifikie lengo lililokusudiwa juu ya kuwasaidia wananchi.
Amewakumbusha kwamba, kuna chombo maalumu kinachotoa adhabu iwapo kuna wanaokwenda kinyume cha matakwa ya kazi hiyo ya usimamiaji haki.
“Tumeanza hii safari ya kuwa mawakili wasomi na jamii inafahamu kuwa mawakili wanajua kila kitu, hivyo mna wajibu wa kuwathibitishia wananchi kuwa dhana zao ziko sahihi. Nataka mjiendeleze kusoma ili mfikie malengo yenu na ya jamii,” amesema.
Makamu Mkuu wa Shule ya Sheria na Taaluma, Msemo Mavare amesema idadi kubwa ya mawakili ni kutoka katika Shule ya Sheria Zanzibar.
Amesema mafanikio wanayoyapata katika chuo chao ni kuona wanafunzi wanapata nafasi za kuwa mawakili katika taasisi mbalimbali, ikiwamo Mahakama.
Akizungumza kwa niaba ya mawakili hao, Nildat Ahmed Omar amesema watahakikisha wanaitumia vyema fursa waliyopata kutenda haki za wananchi na kuahidi kujitoa kwa kila mmoja.