Tume Huru ya Uchaguzi mguu sawa uchaguzi mkuu 2025

Unguja. Wakati uzinduzi wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga kura ukitarajiwa kufanyika Julai Mosi, 2024, Sh418 bilioni zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya kazi hiyo.

Uzinduzi huo utafanyika mkoani Kigoma ambapo mgeni rasmi atakuwa  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Akizungumza na waandishi wa Habari leo Mei 15, 2024, mjini Unguja,  Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji Jacobs Mwambegele, amesema Tume ina wajibu wa kuboresha daftari kabla ya siku ya uteuzi wa wagombea kwenye uchaguzi unaofuata wa mwaka 2025.

Amesema siku ya uzinduzi ndiyo uboreshaji utaanza mkoani Kigoma na mingine ya Katavi, Rukwa na Tabora na utafanyika kwa mizunguko 13 kulingana na ratiba itakayotolewa.

Majukumu yatakayofanywa katika uboreshaji, amesema ni kuandikisha wapiga kura wapya raia wa Tanzania wenye umri wa miaka 18 na kuendelea na ambao hawajapoteza sifa kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi au nyingine.

Uboreshaji wa daftari hilo unaotarajiwa kukamilika Machi 2025, utatoa fursa kwa wapiga kura walioandikishwa awali lakini wamehama kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine kujiandikisha.

“Kutoa kadi mpya kwa wapiga kura waliopoteza au kadi zao kuharibika na kuondoa wapiga kura waliopoteza sifa ikiwa ni pamoja na kuukana uraia au kufariki dunia,” amesema.

Kwa kuzingatia matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, amesema daftari linatarajiwa kuwa na wapiga kura 34,746,638 kutoka wapiga kura 29,754,699 wa mwaka 2020 sawa na ongezeko la wapiga kura 5,586,433 ambayo ni  asilimia 18.7

Kati ya hao, wapiga kura 4,369,531 wanatarajia kuboresha taarifa zao na 594,494 wataondolewa katika daftari kwa kupoteza sifa za kuwa wapiga kura.

Kwa mujibu wa Jaji Mwambegele, Tume tayari imekamilisha maandalizi kwa ajili ya shughuli hiyo ikiwa ni pamoja na uhakiki wa vituo vya kuandikisha wapiga kura. Amesema vituo 40,126 vitatumika katika uboreshaji huo.

Kati ya vituo hivyo, 39,709 ni vya Tanzania Bara na 417 ni vya Zanzibar.

Amesema Tume imefanya usanifu wa kuboresha mfumo wa uandikishaji wapiga kura (VRS) ili kuendana na BVR kits za sasa ambazo zitatumia programu endeshi ya android tofauti na BVR kits za awali, zilizokuwa zikitumia programu endeshi ya window.

“Tume imeanzisha mfumo wa uboreshaji kwa njia ya mtandao (OVRS) ambao utamwezesha mpiga kura aliye kwenye daftari kuanzisha mchakato wa awali wa kuboresha taarifa zake kwa njia ya mtandao kwa kutumia simu ya mkononi au kompyuta,” amesema.

Baada ya kukamilisha mchakato kwa njia ya mtandao mpiga kura atalazimika kufika kituo cha mpiga kura kukamilisha mchakato na kupewa kadi yake ya kura.

Katika uboreshaji huo, amesema umeandaliwa utaratibu maalumu kwa wafungwa walipo magerezani ambako kuna vituo 130 kwa Tanzania Bara na 30 kwa Zanzibar.

Hata hivyo, amesema kwa mujibu wa kifungu cha 10 (1) (C) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani namba moja ya mwaka 2024 hakitoi nafasi ya kuandikishwa mfungwa aliyetiwa hatiani au ambaye kifungo chake kinazidi miezi sita.

Amesema Tume imenunua vifaa zikiwemo BVR 6,000 zinazotumia vishkwambi kuchukua taarifa za wapiga kura, ikiwamo picha saini na alama za vidole.

Amesema tayari Tume imeandaa nyaraka zenye maelekezo na miongozo kwa ajili ya kutumika wakati wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga kura.

Amesema kabla ya kuanza uboreshaji huo, Tume itafanya mikutano na wadau wa uchaguzi ngazi ya Taifa na katika kila mkoa kwa mujibu wa ratiba.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC,  Ramadhani Kailima amesema vifaa vitakavyotumika kwenye shughuli hiyo vimezingatia aina zote za wenye ulemavu.

Related Posts