Unasihi kwa wanafunzi watajwa kuwa suluhisho la ajira

Dar es Salaam. Katika kukabiliana na mdondoko wa wanafunzi shuleni na janga la ajira kwa vijana nchini, unasihi kwa wanafunzi umetajwa kuwa suluhisho la kuwaelekeza kwenye ndoto za maisha yao.

Hoja hiyo imekuja wakati Serikali ikiboresha mitalaa na Sera ya Elimu ikilenga kuwapa nafasi wanafunzi nafasi ya kuchangua fani za kusomea zitakazowawezesha kujiajiri au kuajiriwa.

Hayo yameelezwa leo Jumamosi Februari 8, 2025 katika kongamano la kikanda lililoandaliwa na Taasisi ya Huduma za Elimu ya Aga Khan Tanzania (AKES, Tanzania) jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika mkutano huo, mshauri wa wanafunzi Taasisi ya Elimu ya Afrika Mashariki, Dk Jane Rarieya amesema kuna umuhimu wa kuwanasihi wanafunzi, kwa kuwa kusoma peke yake hakuwapi mwanga wa maisha.

“Kwa Afrika ikiwamo Tanzania, ukosefu wa ajira umeonekana kuwa janga, umuhimu wa uongozi wa kitaaluma unabaki kuwa jambo la msingi.

“Wanafunzi wamekuwa wakifanya uamuzi wa mustaabali wa maisha yao wakiwa gizani, hawana taarifa, ukweli na uwezo wa kung’amua mambo yaliyo mbele. Wanafuzu masomo, lakini hawaelewi waende wapi, kuna fursa gani ziko mbele yao? Au kupata kazi wanazopaswa kuwa nazo,” amesema Dk Rarieya.

Amesema katika kazi yake kwa kiasi kikubwa amekuwa akiwanasihi wanafunzi kuchagua mustakabali wa maisha yao kwa busara wangali bado shuleni.

“Wanasihi katika shule wanapaswa kuonyesha mwanga kwa wanafunzi, wawape wafafanuzi wa ndoto na uhalisia, hapo ndipo unasihi unaleta maana,” amesema Dk Rarieya.

Mkurugenzi wa Ubunifu na Mwandaaji wa Vifaa vya Elimu katika Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE), Fixion Mtelesi aliyezungumza kwa niaba ya Mkurugenzi mkuu wa taasisi hiyo, Dk Annet Komba amesema suala hilo ni muhimu na wamelisisitiza kwenye maboresho ya mitalaa.

“Huduma ya unasihi kwa wanafunzi ni muhimu hasa walimu wanapokuwa nayo ili kuwasaidia wanafunzi kuepukana na changamoto wanazokutaka katika masiha yao zikiwamo za uchumi, uhusiano na changamoto za kujua wanataka kuwa kina nani maishani mwao.

“Wanafunzi wanatakiwa kuanza masomo yao tangu darasa la kwanza hadi la sita, kwa hiyo wakifika huko ndipo watachagua ama waende mkondo wa amali au wa jumla. Uamuzi huu kwa kuwa bado wanakuwa wadogo, wanaweza wasifanikiwe peke yao bila walimu kuwaongoza,” amesema Mtelesi.

Mwalimu wa Hisabati na Tehama katika shule za Aga Khan, Veronica Sarungi amesema pamoja na kufundisha wanafunzi masomo hayo, analazimika kuwashauri.

“Unakuta mwanafunzi anakwambia, mwalimu mimi sioni umuhimu wa kusoma hisabati, kwani itanisaidiaje? Mwingine anakuja kuomba ushauri, je nichukue masomo ya sayansi au nichukue ya biashara? Au nataka kusoma fizikia, kemia na hisabati (PCM), sasa unamuuliza unataka kuwa nani? Au unaweza kufanya kitu gani? Kwa hiyo tunakaa tunashauriana,” amesema Sarungi.

Naye Mwalimu Lynette Kaylo wa Shule ya Msingi ya Aga Khan jijini hapa amesema ushauri wa wanaunzi unaanzia tangu wakiwa wadogo.

“Mwalimu ni kama mama au baba akiwa darasani, sasa hapa tunapata uzoefu wa kutusaidia kuwa walimu bora darasani.

“Tuna umuhimu wa kuwa karibu na wanafunzi, kwani wakati mwingine wanaweza kukosa kazi, kwa hiyo wasizingatie tu kazi moja waliyosomea, bali wajue kuna mambo mengi ya kufanya kwa kuchangamana na kufanya kazi tofauti,” amesema Kaylo.

Mtendaji Mkuu wa AKES Tanzania, Dk Shelina Walli amesema wameandaa kongamano hilo kutokana na changamoto za mdondoko wa wanafunzi shuleni na janga la ukosefu wa ajira.

“Tunajua umuhimu wa elimu kwa mwanafunzi ni kumwezesha kupata maisha bora, hivyo tumeona kuna umuhimu kwa kuwapa walimu mafunzo yatakayowawezesha kuwapa uzoefu, kujifunza kutoka kwa wenzao jinsi ya kunasihi,” amesema Dk Walli.

Kongamano hilo limeshirikisha walimu kutoka shule 81 za Serikali na za binafsi kutoka Kenya, Tanzania, Rwanda, Burundi, Uganda Msumbiji.

Related Posts