Uhaba wa fedha wakwamisha vikao vya Bunge la Afrika Mashariki

Arusha. Bunge la Afrika Mashariki (EALA) limetangaza kuahirisha vikao vyake kwa muda usiojulikana kutokana na changamoto za kifedha.

Upungufu huo wa kifedha umetokana na baadhi ya nchi wanachama kushindwa kulipa michango yao, jambo lililosababisha kushindwa kufanyika kwa vikao vya Bunge vilivyokuwa vimepangwa kuanza Januari hadi Juni 2025.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana, Februari 7, 2025 jijini Arusha na Ofisa Habari wa EALA, Nicodemus Ajak Bior, uamuzi huo umefikiwa baada ya kikao cha Kamisheni ya EALA na viongozi wa kamati kilichofanyika jana Februari 6, 2025.

“Uamuzi huu ambao unahusisha shughuli zilizopangwa kutoka Januari hadi Juni 2025, umetokana na tathmini ya hali ya kifedha ya Bunge iliyofanywa katika kikao cha Kamisheni ya EALA na viongozi wa kamati kilichofanyika Februari 6, 2025,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza.

“Kusitishwa kwa shughuli hizi kumechagizwa na upungufu wa kifedha ambao umekwamisha utekelezaji wa majukumu ya kisheria na ya usimamizi ya Bunge,” amesema Bior.

Kutokana na hali hiyo, Spika wa EALA, Joseph Ntakarutimana amesema amefanya majadiliano na Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la EAC, Beatrice Asukul Moe na Katibu Mkuu wa EAC, Veronica Nduva ili kuhimiza nchi wanachama ambazo bado hazijalipa michango yao kulipa haraka ili kuwezesha Bunge kuendelea na shughuli zake.

Spika Ntakarutimana amesema wana matumaini suala la kifedha litakuwa limetatuliwa kwa haraka wiki tatu zijazo.

Taarifa hiyo inasisitiza kwamba, EALA itaendelea kujitolea katika kutimiza jukumu lake la kukuza umoja wa kikanda kupitia sheria, usimamizi na uwawakilishi.

“Tunatumaini kwamba, mashauriano yanayoendelea yatatoa matokeo chanya na hivyo Bunge kuendelea na majukumu yake muhimu pindi itakapokuwa inawezekana,” inaeleza taarifa hiyo.

Jumla ya nchi nane zinazounda jumuiya hiyo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Somalia.

Related Posts