Dar es Salaam. Kukosekana umeme wa uhakika na kutokuwapo usawa sokoni kumetajwa kuwa sababu ya viwanda, vikiwamo vya chuma kushindwa kufanya kazi kwa kiwango kinachotakiwa nchini.
Kutokana na hilo, imependekezwa kuangaliwa namna kituo cha kupoza umeme Mkuranga kinavyoweza kupewa kipaumbele badala ya kile cha Chalinze ili kuhudumia viwanda, vinavyochangia ukuaji wa uchumi.
Wamiliki wa viwanda vya chuma wamependekeza pia, adhabu kwa wanaokiuka vigezo vya uzalishaji ianzie Sh100 bilioni ili kukomesha michezo hiyo sokoni, wakidai faini zinazotozwa haziwafanyi waumie.
Mapendekezo hayo yametolewa leo Februari 8, 2025 mbele ya wajumbe wa Kamati ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo waliotembelea kiwanda cha Lodhia Industries kilichopo wilayani Mkuranga, mkoani Pwani, kinachozalisha nondo, mabati, nyaya na bomba za plastiki.
Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Sailesh Pandit amezungumzia upatikanaji umeme akisema ili wazalishe kwa kiwango kinachotakiwa wanalazimika kuwasha mashine kwa awamu.
Amesema tangu mwaka jana walipowasilisha suala hilo serikalini walipewa ahadi ya kufungwa transfoma kuwezesha upatikanaji umeme wa uhakika.
“Ni miezi sita hadi minane sasa tunapewa ahadi hii, tuangalie kwa undani hili, kwani ili tuzalishe, tunalazimika kuwasha mashine kwa awamu, kama tunaingia kuzalisha nondo tunasimamisha upande wa chuma, tukihami bati tunazima huku. Ni hasara kubwa, tunaomba kupewa msaada katika hili,” amesema.
Ili kuzalisha kwa kiwango kinachotakiwa, amesema wanahitaji megawati 25 za umeme kwa siku lakini wanapata wastani wa megawati 12 pekee.
Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Khadija Nassir Ali akizungumzia malalamiko hayo amesema wanatengeneza miundombinu ya usafirishaji umeme ili kuufikisha unapotakiwa.
“Tumepokea Sh79 bilioni kwa ajili ya kujenga miundombinu, transfoma inayozungumziwa ni kweli ilikuwa na changamoto hasa mtu aliyepewa kazi hiyo alikuwa na changamoto za kikodi. Awali, ilizuiwa lakini baadaye mkuu wa mkoa aliunda kamati na ilisaidia ikatolewa,” amesema Khadija.
Amesema transfoma hiyo itakapotolewa itachukua si zaidi ya miezi miwili kuifunga, akieleza hadi sasa ni mwezi mmoja na wiki mbili zimebaki ili kazi ikamilike.
Makamu mwenyekiti wa kamati hiyo, Mariam Ditopile ametaka kuangaliwa kwa umakini suala hilo na kuweka mipango ya kutatua suala la umeme hasa katika Wilaya ya Mkuranga iliyo na viwanda vingi.
Ameitaka Serikali kupanga vipaumbele vyake vyema hasa inapojenga vituo vya kupoza umeme unaozalishwa katika Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP).
“Iangaliwe namna ambayo kituo cha kupoza umeme cha Mkuranga kinaweza kupewa kipaumbele katika ujenzi badala ya kile cha Chalinze kutokana na umuhimu uliopo huku, kuna viwanda vingi na Serikali inapata fedha nyingi,” amesema.
Kuhusu kutokuwapo usawa sokoni, Mwenyekiti na Mmiliki wa Lodhia Industries, Arun Lodhia ameitaka Serikali kusimamia ubora wa bidhaa zinazozalishwa na kuingizwa sokoni ili kulinda viwanda vya ndani.
Amesema kukosekana kwa usawa kumeweka mazingira magumu kwa wawekezaji wa Tanzania dhidi ya wale wanaoingiza bidhaa kutoka nje.
“Kama mtu anaiba, anaiba tu, hata mkienda kumfungia analipa faini kesho anaendelea, faini yenyewe ni ndogo, mtu anaiba mabilioni ya hela lakini anaambiwa alipe faini Sh20 bilioni, siyo hela ni vyema mtu alipishwe Sh100 bilioni na kuendelea lakini mtu kulipa Sh10 bilioni na anauza kitu ambacho kiwango chake ni kidogo ni hela nyingi sana anapata,” amesema.
Ametaka miradi ya ndani inayotekelezwa kutoa kipaumbele kwa bidhaa zinazozalishwa nchini ili kuchochea ukuaji wa viwanda.
Mwenyekiti wa kamati hiyo ya Bunge, Deodatus Mwanyika ameahidi kwenda kukaa na Waziri wa Viwanda, Suleimani Jafo ili waweke mikakati ya pamoja kushughulikia changamoto zinazokabili viwanda.
“Tujue linalofanyika ni nini na hatua za haraka zipi zinachukuliwa, uwekezaji mkubwa kama huu ni fahari kwa nchi yetu na una mategemeo kuwa utapata faida, ili uipate lazima uwe na mazingira mazuri,” amesema.
Amesema kama biashara imeanza na kunakuwa na mabadiliko ya vitu ambavyo havikuwapo wakati uwekezaji unafanyika, ikiwamo kuruhusu kampuni za nje kuvamia soko inaweza kuwa na athari.
Inaelezwa zaidi ya tani 3,500 za bati zinazozalishwa na kiwanda hicho, haziendi sokoni kwa sababu ya kutokuwapo usawa.
“Tukae na wizara tuyajadili haya kwa sababu ni mambo ambayo hayana tija kwa Taifa. Hatuwezi kuwa tunalamika, mwekezaji analalamika, ikija kamati inalalamika, waziri akija analalamika, nani amshike mwenzake, lazima tuyafanyie kazi haya,” amesema.
Naibu Waziri wa Biashara na Viwanda, Exhaud Kigahe amesema suala la umeme linafanyiwa kazi.
“Sisi kama wizara tumepokea maelekezo yote na tunakwenda kufanyia kazi, tumepokea pia maagizo tutakaa pamoja tuone namna ya kuwasaidia,” amesema.
Kigahe amesema tayari hatua zimeanza kuchukuliwa kuhakikisha kunakuwa na ushindani wa haki katika sekta zote, ikiwamo kulinda viwanda vya ndani ili vipate faida.