Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA) imetangaza bei mpya za mafuta kwa mwezi Febuari 2025 ambapo bei hizo zimetajwa kupanda.
Akitoa taarifa hiyo kwa Waandishi wa Habari Kaimu Meneja Kitengo cha Uhusiano Shara Chande Omar kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA) katika ukumbi wa ZURA uliopo Maisara Mjini Unguja ambapo bei hizo zitaanza kutumika kesho tarehe 09/02/2025.
Amesema bei ya mafuta kwa mwezi Febuari imepanda kulinganisha na mwezi Januari, Akizitaja bei hizo amesema Petrol imepanda kutoka Mwezi Januari 2,775 hadi Febuari 2,819 bei ya Dizel imepanda kutoka mwezi Januari 2,892 hadi Febuari 2,945 wakati mafuta ya ndege yamepanda kutoka mwezi Januari 2,414 hadi Febuari 2,423 wakati mafuta ya taa yatabaki na bei ileile ya 3200 kwa mwezi Febuari.
Hata hivyo amesema ZURA inapanga bei kwa kuzingatia mambo mbalimbali ikiwemo Wastani wa mwenendo wa Mabadiliko ya bei za mafuta Duniani, Gharama za uingizaji wa Mafuta katika Bandari ya Tanga, gharama za mabadiliko ya fedha za kigeni zinazotumika kununulia mafuta, Gharama za Usafiri, Bima na ‘Preminium’ hadi Zanzibar, Kodi za Tozo za Serikali na Kiwango cha faida kwa Wauzaji wa Jumla na Reja Reja.
Aidha amesema Sababu za kuongezeka kwa Bei za Mafuta kwa Mwezi Febuari, 2025 ni kuongezeka kwa gharama za Mafuta katika Soko la Dunia, kuongezeka kwa gharama za uingizaji wa mafuta na kuongezeka kwa wastani wa thamani ya Dola ya Kimarekani ukilinganisha na Shilingi ya Tanzania.
Mamlaka inawahimiza Wananchi kununua Mafuta katika Vituo halali vya kuuzia Mafuta na kudai Risiti za Kielectroniki kila wanaponunua mafuta hayo ili zinapotokezea changamoto zozote wapate kusaidiwa.