Watoto waliotekwa Mwanza wapatikana, watuhumiwa wa utekaji wauawa

Mwanza. Wanafunzi Magreth Juma (8) wa darasa la pili na Fortunata Mwakalebela (5) wa Shule ya Blessing Modern, iliyopo Nyasaka wilayani Ilemela mkoani Mwanza waliotekwa wamepatikana.

Tukio la kutekwa watoto hao lilitokea Februari 5, 2025, saa 12:30 asubuhi eneo la Capri Point, jijini Mwanza wakiwa kwenye basi lililokuwa linawapeleka shuleni.

Akizungumza leo Jumamosi Februari 8, 2025 akiwa eneo walikopatikana watoto hao, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa amesema taarifa za kikachero zilifanikisha kubaini kuwa watekaji wamewaficha watoto ndani ya nyumba namba nane iliyopo Mtaa wa Nyaburogoya, Kata ya Nyegezi jijini Mwanza.

Kamanda Mutafungwa amesema baada ya kuonekana wakitishia usalama wa maofisa wa polisi waliofichua maficho yao kutokana na watuhumiwa hao (wawili) kuwa na silaha, yakiwamo mapanga na nondo, polisi waliwarushia risasi zilizowajeruhi na kusababisha vifo vyao.

“Walipoona wamebainika wakataka kupambana na askari wetu, kwa sababu askari wamefunzwa namna ya kulinda usalama wao na wananchi wengine walilazimika kutumia risasi za moto na watu wawili ambao walikuwa na silaha hizo walijeruhiwa kwa risasi kisha kufariki dunia,” amesema.

Endelea kufuatilia Mwananchi.

Related Posts