Mara. Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Stephen Wasira amewakosoa wanaosema chama hicho hakijafanya lolote tangu kiingie madarakani, akisema hata elimu waliyonayo imetokana na chama hicho.
Akizungumza na wanachama wa chama hicho leo Jumamosi Februari 8, 2025 katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Wilaya Tarime mkoani Mara, Wassira amesema kwa miaka 60 iliyopita Watanzania wamekuwa na hali bora zaidi kimaisha.
“Tunataka kufanya mapinduzi ya maisha ya watu na tunafanya, ndiyo maana watu wa Tarime sasa ni watu tofauti na waliokuwepo miaka 60 iliyopita.
“Unasimama unasema hatujafanya kitu, tumefanya, tumesomesha watu wengi sana hata wanaosema hatujafanya chochote tumewasomesha na uhuru wa kusema hatujafanya chochote tumewapa,” amesema Wasira.
Amesema chama hicho ndicho kinajenga maono ya vyama vya TANU na ASP na ndiyo wanachama wake walijitoa mhanga kuondoa uonevu wa wakoloni kwa lengo la kubadilisha maisha ya wananchi.
Amesema katika kipindi cha miaka minne pekee ya uongozi wa Serikali ya awamu ya sita, mabadiliko makubwa yameonekana yakiwemo ndani ya Wilaya ya Tarime ambako imejenga madarasa bila ya kuwachangisha wananchi kama ambavyo ilikuwa ikifanyika awali.
“Wako wengine wanasema miaka 60 eti hatujafanya kitu, naomba muwasamehe kwa kuwa hawajui wanachosema, kwa sababu mimi kwa umri wangu nilikuwepo niliijua Tarime kabla ya uhuru na nawaona wapo wazee hapa pia waliijua.
“Hii sura mnayoiona leo haikuwa sura ya Tarime, ukiwarudisha watu wa Tarime wa mwaka 60 ukachukua na waliopo sasa hawawezi kuelewana, watu wa Tarime wa sasa wote wanajua kusoma na kuandika, lakini wa wakati ule walikuwa hawajui.
“Kina mama wa Tarime sasa wanang’aa, kina mama wa Tarime wa wakati ule walikuwa wanatawaliwa na matatizo, hawakuwa na nguo za kuvaa,” amesema Wasira.
Amesema vyama vinavyokosoa CCM vimejaa lugha za matusi, akiwataka wanachama wa chama hicho kupuuza maneno yao.
“Juzi juzi wamefanya mkutano wao Dar es Salaam pale wamegawana fito, mmoja kaenda na wake na mwingine kaenda na wake, kuna chama hapo? Sasa wanakuja kukwambieni Tarime muwapigie kura wamefanya kitu gani, maana mtu hupigi kura bila ya sababu,” amesema Wasira bila kutaja chama anachodai kimegawanyika.
Katika hatua nyingine, Wasira amewataka wajumbe wa vikao mbalimbali vya CCM wajikite kusikiliza kero za wananchi ili kuangalia njia ya kuzitatua.
“Ikiwa watu wanadhulumiwa sisi tunaweza kudumu? Chama kitadumu vipi wakati watu wanadhulumiwa?” amehoji Wasira.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi ametumia fursa hiyo kumuomba Wasira kusaidia kuhakikisha uwanja wa ndege wa Musoma na Serengeti unakamilika.
Uwanja huo unajengwa kwa gharama ya zaidi ya Sh35 bilioni ambapo hivi karibuni ujenzi wake ulisimama kutokana na ukosefu wa fedha.
“Ili mkoa uweze kunufaika na rasiliamli zilizopo ni lazima tuwe na wawekezaji wa kutosha hivyo miundombinu kama uwanja wa ndege ni moja ya kichocheo cha wawekezaji, tunakuomba Makamu Mwenyekiti usaidie kuhakikisha hili linakamilika,” amesema Mtambi.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Tarime, Marwa Ngicho amesema wana CCM wanapaswa kuvumuliana na siyo kuvuana nguo wakati huu kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba, 2025.
Amesema wilaya hiyo yeye majimbo mawili imejipanga kushinda kata zote upande wa madiwani pamoja na wabunge.
Nao, Wabunge wa Tarime Mjini, Michael Kembaki na Tarime Vijijini, Mwita Weitara wamepongeza Serikali kwa kupeleka miradi ambayo imetatua kero za wananchi ukiwemo wa ujenzi wa soko la kisasa na miradi ya maji.