Rais wa Marekani Donald Trump rasmi ametia saini amri ya kufungia msaada wa kifedha kwa Afrika Kusini, baada ya kutishia kufanya hivyo mapema wiki hii.
Trump alisema anaweka amri hiyo kwa sababu ya sheria mpya ya ardhi ya Afrika Kusini, ambayo anasema inakiuka haki za watu, na pia kwa sababu ya kesi yake ya mahakama ya kimataifa inayoishutumu Israel kwa mauaji ya halaiki.
“Afrika Kusini inanyakua ardhi na matabaka fulani ya watu yalikuwa yakitendewa vibaya sana,” amesema Tramp.
Mshauri wa karibu wa Trump Elon Musk, ambaye alizaliwa nchini Afrika Kusini, pia alijiunga na ukosoaji huo akiuliza kwenye mtandao wa X kwa nini Ramaphosa (Rais wa Sauz) alikuwa na sheria za umiliki za kibaguzi.
Rais Cyril Ramaphosa bado hajatoa kauli yake lakini hapo awali alitetea sera ya ardhi ya Afrika Kusini baada ya tishio la Trump siku ya Jumapili.
Alisema serikali haijanyakua ardhi yoyote na sera hiyo inalenga kuhakikisha wananchi wanapata ardhi kwa usawa.
Sheria ya Rais Ramaphosa ilitiwa saini mwezi uliopita, na inaruhusu unyakuzi wa ardhi bila kulipwa fidia katika mazingira fulani. Umiliki wa ardhi kwa muda mrefu umekuwa suala la kutatanisha nchini Afrika Kusini huku mashamba mengi ya binafsi yakimilikiwa na watu weupe, miaka 30 baada ya kumalizika kwa mfumo wa kibaguzi wa ubaguzi wa rangi.