Wakuu wa nchi EAC, SADC waazimia mapigano yasitishwe DRC

Dar es Salaam. Wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) wamepitisha azimio la pamoja la kutaka mapigano yasitishwe ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Ili kufanikisha hilo, wamewataka wakuu wa majeshi wa nchi za jumuiya hizo za kikanda kukutana haraka ndani ya siku tano ili kutoa mwongozo wa namna ya kumaliza mapigano hayo.

Viongozi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)

Wakuu hao wa majeshi watatakiwa kutoa mwongozo wa namna ya kutoa msaada wa kibinadamu, mpango wa usalama huko Goma na maeneo ya jirani, kufungua uwanja wa ndege wa Goma na kufungua njia nyingine zikiwemo Goma – Sake – Bukavu.

Mkutano huo wa siku moja, umehudhuriwa na viongozi mbalimbali chini ya uenyekiti wa Rais wa Kenya, William Ruto ambaye pia ni mwenyekiti wa EAC na Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa ambaye ni mwenyekiti wa SADC pamoja na marais wengine saba, akiwemo wenyeji wao, Rais Samia Suluhu Hassan. Pia walikuwepo wawakilishi wa marais watano.

Miongoni mwa marais hao alikuwemo Rais wa Rwanda, Paul Kagame huku mwenzake wa DRC, Felix Tshisekedi akishiriki kwa njia ya mtandao, licha ya kuwakilishwa na Waziri Mkuu wake, Judith Tuluka.

Akisoma maazimio jioni ya leo Februari 8, 2024, Katibu Mkuu wa EAC, Veronica Nduva amesema wakuu hao wa nchi wameazimia kuhuisha majadiliano kati ya nchi na makundi mengine (ya kijeshi na yasiyo ya kijeshi) likiwemo la M23, chini ya mpango wa michakato Luanda na Nairobi.

Pia, viongozi hao wamekubaliana mawaziri wa EAC na SADC kukutana ndani ya siku 30 ili kutoa mwongozo katika masuala tofauti, ikiwemo ripoti ya mkutano wa wakuu wa majeshi kuhusu kusitisha mapigano na kuanzisha sekretarieti ya kuratibu utekelezaji wa maazimio ya wakuu hao.

Wakuu wa nchi wamekubaliana kuandaliwa kwa njia za kuviondoa vikosi vya majeshi yote ya kigeni ambavyo hayajaalikwa katika ardhi ya DRC.

Nduva ameongeza kuwa wakuu wa nchi za EAC na SADC wametaka mbali na kusitishwa kwa mapigano, ufanyike ukarabati wa miundombinu kwa ajili ya ufikishaji wa misaada ya kibinadamu kufikia azimio la amani.

Wakuu hao wa nchi wamethibitisha kuendeleza mshikamano na kujitolea kuendelea kuiunga mkono DRC na kuhakikisha inapata uhuru wa eneo lake.

“Kuwepo kwa majadiliano kama haya mara moja kila mwaka ili kufanya tathmini ya mzozo huo na kuwaalika viongozi wa Afrika Mashariki kila mwaka kupitia masuala hayo ya DRC,” imeeleza taarifa ya pamoja ya wakuu wa nchi za SADC/EAC.

Wakuu wa nchi hizo wamempongeza Rais William Ruto, Mwenyekiti wa EAC kwa kuitisha na kuongoza majadiliano hayo huku wakimpongeza Rais Samia kwa kukubali kuwa mwenyeji wa mkutano huo.

Related Posts